TANZANIA YALENGA KUZALISHA ASILIMIA 60 YA MAHITAJI YA DAWA NA VIFAA TIBA

TANZANIA YALENGA KUZALISHA ASILIMIA 60 YA MAHITAJI YA DAWA NA VIFAA TIBA

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa alipokuwa akiwasilisha taarifa ya Serikali kuhusu mkakati wa uzalishaji wa dawa na vifaa tiba nchini mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Oktoba 13, 2026 Jijini Dodoma.

....................

Na Shaban Juma, WAF – Dodoma

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, amesema Serikali inalenga kuongeza uzalishaji wa dawa na vifaa tiba nchini ili kufikia zaidi ya asilimia 60 ya mahitaji ya taifa ifikapo mwaka 2030, kutoka kiwango cha sasa cha takribani asilimia 20, hatua inayolenga kupunguza utegemezi wa bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.

Dkt. Samizi ameyasema hayo leo, Oktoba 13, 2026, jijini Dodoma, wakati akiwasilisha kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, taarifa ya Serikali kuhusu mkakati wa uzalishaji wa dawa na vifaa tiba nchini mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI.

Amesema Serikali, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika uzalishaji wa bidhaa za afya ili kuongeza uwezo wa viwanda vya ndani na kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa mahitaji ya wananchi.

"Kwa sasa, Tanzania ina viwanda 19 vinavyohusika na bidhaa za afya, vikiwemo viwanda 13 vya dawa za binadamu na sita vya dawa za mifugo, pamoja na viwanda vitatu vya vitendanishi vya maabara na vitano vya vifaa tiba. Uwezo wa uzalishaji wa ndani unakadiriwa kukidhi takribani asilimia 20 ya mahitaji ya taifa" amesema Dkt.Samizi

Amesema katika kuharakisha uwekezaji, Serikali ilianzisha Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji katika Sekta ya Dawa (PIAT) Desemba 23, 2025, kwa lengo la kuratibu uwekezaji na kuondoa vikwazo vinavyoweza kuchelewesha utekelezaji wa miradi.ameeleza kuwa hadi Agosti 2026, wawekezaji 83 walikuwa wameonesha nia ya kuwekeza, 57 walikuwa wamefanyiwa tathmini na majadiliano ya kina, huku sita wakifikia hatua za kuelekea utekelezaji wa miradi.

Aidha, Serikali imetenga eneo la ekari 400 kwa ajili ya Hifadhi ya Viwanda vya Dawa na Vifaa Tiba Mloganzila, ambapo ekari 386 zimetengwa kwa wawekezaji 11 waliokidhi vigezo.amesisitiza  hatua hiyo inalenga kuimarisha uzalishaji, utafiti na mafunzo, sambamba na kuvutia wawekezaji wengine katika sekta hiyo.

Hata hivyo, amesema utekelezaji wa mkakati huo bado unakabiliwa na changamoto zinazohusiana na miundombinu ya maeneo ya uwekezaji, upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu, gharama za teknolojia na malighafi, pamoja na ushindani kutoka kwa bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi. Katika kukabiliana na changamoto hizo,ameongeza  Serikali inaendelea kuboresha miundombinu, kurahisisha uratibu wa vibali, kuhamasisha uhamishaji wa teknolojia na kuimarisha soko la bidhaa zinazozalishwa nchini kupitia ununuzi wa bidhaa zenye ubora unaotakiwa.

Dkt. Samizi amesema Serikali itaendelea kutekeleza mikakati hiyo kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Sera ya Afya na mipango ya maendeleo ya taifa, kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa ndani, kupunguza utegemezi wa bidhaa za afya kutoka nje na kuimarisha usalama wa afya nchini.




 

Post a Comment

0 Comments