𝐓𝐔𝐙𝐎 𝐘𝐀 𝐌𝐀𝐆𝐄𝐑𝐄𝐙𝐀 𝐊𝐖𝐀 𝐑𝐀𝐈𝐒 𝐒𝐀𝐌𝐈𝐀 𝐈𝐋𝐈𝐕𝐘𝐎𝐀𝐊𝐈𝐒𝐈 𝐌𝐀𝐆𝐄𝐔𝐙𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐅𝐔𝐌𝐎 𝐖𝐀 𝐇𝐀𝐊𝐈 𝐉𝐈𝐍𝐀𝐈 𝐓𝐀𝐍𝐙𝐀𝐍𝐈𝐀

𝐓𝐔𝐙𝐎 𝐘𝐀 𝐌𝐀𝐆𝐄𝐑𝐄𝐙𝐀 𝐊𝐖𝐀 𝐑𝐀𝐈𝐒 𝐒𝐀𝐌𝐈𝐀 𝐈𝐋𝐈𝐕𝐘𝐎𝐀𝐊𝐈𝐒𝐈 𝐌𝐀𝐆𝐄𝐔𝐙𝐈 𝐘𝐀 𝐌𝐅𝐔𝐌𝐎 𝐖𝐀 𝐇𝐀𝐊𝐈 𝐉𝐈𝐍𝐀𝐈 𝐓𝐀𝐍𝐙𝐀𝐍𝐈𝐀


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya kuwa Kinara wa Dhana ya Urekebishaji wa Wafungwa Magerezani kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Patrobas Paschal Katambi pamoja na Kamishna Jenerali wa Magereza Jeremia Yoram Katungu kwenye hafla ya hafla ya kuhitimisha Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Kozi namba 28 na Uongozi Daraja la Pili Kozi namba 48 ya mwaka 2025/2026 katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) Ukonga Jijini Dar es Salaam Mei 9, 2026.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akionesha tuzo hiyo.

.......................................... 

KWA mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Magereza Tanzania, mkuu wa nchi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan ametunukiwa Tuzo Maalumu ya Kinara wa Dhana ya Urekebishaji wa Wafungwa Magerezani (Champion of Prisoner Rehabilitation Concept Award) hatua inayotajwa kuwa ishara ya mageuzi makubwa ya kifalsafa, kiutendaji na kimaendeleo ndani ya mfumo wa haki jinai nchini.

Tuzo hiyo aliyokabidhiwa Rais Samia, Mei 9, 2026 katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania haionekani tu kama pongezi kwa uongozi wa Serikali, bali kama alama ya mabadiliko ya kihistoria yanayoibadilisha falsafa ya magereza kutoka mfumo wa adhabu kwenda mfumo wa urekebishaji, elimu na maendeleo ya binadamu.

Mageuzi hayo yanasimamiwa kwa karibu na Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, CGP Jeremiah Yoram Katungu, ambaye chini ya uongozi wake jeshi hilo limeendelea kufanya maboresho makubwa ya kiutendaji, matumizi ya teknolojia na utoaji wa mafunzo ya kisasa ya urekebishaji.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa maendeleo, hatua hiyo inaonesha Tanzania inaanza kuachana na mfumo wa kikoloni ulioliona gereza kama sehemu ya mateso na kuingia katika mfumo mpya unaomtazama mfungwa kama binadamu mwenye uwezo wa kubadilika na kuchangia maendeleo ya taifa.

KUTOKA MFUMO WA ADHABU KWENDA MFUMO WA UTU

Katika kipindi cha ukoloni, mfumo wa Tanganyika Prisons Service ulijikita zaidi katika kazi ngumu na matumizi ya wafungwa kama nguvu kazi ya bei nafuu kwenye mashamba ya serikali, ujenzi wa barabara, useremala na shughuli nyingine za mikono.

Lakini baada ya uhuru, hasa kuanzia mwaka 1974, Tanzania ilianza rasmi mageuzi ya kifalsafa yaliyolenga kubadili mfumo wa magereza kutoka adhabu kwenda urekebishaji tabia.

Mageuzi hayo yalienda sambamba na kutenganishwa kwa Magereza na Jeshi la Polisi pamoja na kuanzishwa kwa taasisi maalumu za taaluma ya urekebishaji.

Hapo ndipo falsafa ya Humanism au utu wa binadamu ilipoanza kuonekana ndani ya mfumo wa haki jinai nchini.

Katika falsafa hiyo, hata mfungwa ana haki ya kupewa elimu, kuheshimiwa na kuandaliwa kurejea katika jamii akiwa mtu bora zaidi.

Ndiyo maana kwa sasa Jeshi la Magereza limejikita katikamafunzo ya ufundi, elimu ya tabia, kilimo, uzalishaji na stadi mbalimbali za maisha.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikagua Gwaride mara baada ya kuwasili katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) Ukonga.

......................................

CHUO CHA UREKEBISHAJI NA UJENZI WA RASILIMALI WATU

Miongoni mwa taasisi zilizopewa jukumu kubwa la kusimamia mageuzi hayo ni Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania ambacho kimeendelea kutoa mafunzo ya Sayansi ya Urekebishaji kuanzia ngazi ya Astashahada hadi Stashahada.

Kupitia chuo hicho, maafisa wa Magereza wanafundishwa taaluma za kisasa zinazolenga kubadili tabia za wahalifu na kuwaandaa kurejea katika jamii kama raia wema.

Wataalamu wa maendeleo kama vile Theodore Schultz na Gary Becker wanaeleza kuwa maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana bila kuwekeza katika elimu, maarifa na stadi za watu.

Kupitia Nadharia ya Maendeleo ya Rasilimali Watu (Human Capital Theory), wasomi hao waliamini kuwabinadamu ndiye mtaji mkubwa wa taifa, hivyo hata watu waliowahi kufanya makosa wanaweza kubadilishwa na kuwa nguvu kazi yenye mchango katika uchumi ikiwa watapatiwa elimu, mafunzo na mazingira ya kujitegemea.

Kwa mtazamo huo, gereza linaanza kubadilika kutoka eneo la kufungia watu kwenda kituo cha kuandaa nguvu kazi yenye maarifa, nidhamu na uwezo wa kujitegemea baada ya vifungo.

Mfumo huo tayari umetumiwa kwa mafanikio katika baadhi ya nchi zilizoendelea. Mfano, nchini Norway, Gereza la Halden hutumia falsafa ya urekebishaji badala ya adhabu kali.

Wafungwa nchini Norway hupewa elimu, mafunzo ya kazi, ushauri wa kisaikolojia na mazingira yanayofanana na maisha ya kawaida ya jamii.

Kutokana na mfumo huo, Norway imekuwa miongoni mwa nchi zenye kiwango kidogo zaidi cha wafungwa kurudia uhalifu baada ya kutoka gerezani.

Sweden mfumo wa magereza umejengwa katika falsafa ya kurejesha utu wa binadamu na kuwaandaa wafungwa kurudi kwenye jamii wakiwa raia wema.

Kupitia elimu ya ufundi, ushauri nasaha na programu za kazi, taifa hilo limefanikiwa kupunguza msongamano wa wafungwa na viwango vya uhalifu wa kujirudia.

Ni wazi kuwa mageuzi yanayoendelea ndani ya Jeshi la Magereza Tanzania yanaanza kufuata mkondo huo wa kimataifa wa kuyafanya magereza kuwa vituo vya ujenzi wa rasilimali watu badala ya maeneo ya adhabu pekee.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiangalia kiatu ambacho kimetengenezwa na Kiwanda cha viatu cha Gereza la Karanga, Moshi mkoani Kilimanjaro wakati alipotembelea mabanda ya maonesho katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) Ukonga Jijini Dar es Salaam.

....................................... 

MAOFISA WA MAGEREZA WABEBA DIRA YA MAGEUZI

Mbali na sera za Serikali, mafanikio hayo yanaelezwa kuchangiwa pia na maofisa wa Jeshi la Magereza wanaotekeleza kwa vitendo maono ya mageuzi hayo.

Akifungua mafunzo ya matumizi ya mfumo wa GAMIS Mei 19, 2026, Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, CP Nicodemus Tenga, kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Magereza Tanzania, alisema matumizi ya TEHAMA ni sehemu ya maboresho yanayolenga kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika usimamizi wa mali za Serikali.

“Ni matarajio ya Jeshi baada ya mafunzo haya wataalamu wa ununuzi watakuwa na maarifa mapya ya kutumia mfumo wa GAMIS na kuongeza uwajibikaji pamoja na kuboresha utunzaji wa kumbukumbu,” alisema CP Tenga.

Kauli hiyo inaonyesha namna Jeshi la Magereza linavyoingia katika falsafa ya Modern State Theory inayosisitiza matumizi ya teknolojia, uwazi na taasisi imara katika kuleta maendeleo ya kisasa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi Jeshi la Magereza, ACP Henry Masawe, alisema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha wagavi kusimamia kwa ufanisi mali zote za kudumu za Serikali kupitia mifumo ya kidigitali.

Kauli za viongozi hao zinaonyesha kuwa mageuzi ya Magereza hayapo tu kwenye maneno ya kisera, bali yanatekelezwa kwa vitendo kupitia mafunzo, usimamizi wa kisasa na ujenzi wa uwezo wa watendaji wake.

MAGEUZI KUTOKA ADHABU HADI UREKEBISHAJI

Wataalamu wa sera za maendeleo wanaamini kuwa mfumo mpya wa Magereza Tanzania unaendana na falsafa ya Rehabilitation versus Punishment ambayo imeanza kupewa nafasi kubwa duniani.

Katika mfumo huo, gereza halionekani tena kama sehemu ya kuumiza au kulipiza kisasi, bali mahali pa kubadili tabia na kuandaa maisha mapya.

Ndiyo maana chini ya uongozi wa Rais Samia, Serikali imeagiza kuanzishwa kwa mfuko maalumu wa mitaji kwa wafungwa wanaomaliza vifungo vyao wakiwa na ujuzi wa ufundi.

Hatua hiyo imepokelewa kama utekelezaji wa Nadharia ya Uwezeshaji Jamii (Empowerment Theory) inayosisitiza kuwa maendeleo ya kweli yanahitaji kuwawezesha watu kujitegemea kiuchumi.

WADAU WAUNGA MKONO MAGEUZI

Wakili Hassan Kiangio amesema mfumo huo mpya unaonyesha kuwa mtu aliyepo gerezani hayupo kwa ajili ya kuadhibiwa pekee, bali kurekebishwa ili aweze kurejea katika jamii akiwa na maadili na stadi za maisha.

Naye Wakili Msomi Aloyce Komba amesema mageuzi hayo yanaendeleza juhudi za muda mrefu za kuboresha haki za wafungwa na mazingira ya magereza nchini.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mstaafu Jamal Rwambow amesema matumizi ya nishati safi, utoaji wa vyeti vya ufundi na kujitegemea kwa magereza ni ushahidi kuwa jeshi hilo linaendana na maono ya maendeleo endelevu.

Mdau wa maendeleo Majaliwa Mbassa amesema wafungwa wanapopata elimu na stadi mbalimbali wanageuka kuwa nguvu kazi yenye tija kwa taifa badala ya kuwa mzigo kwa jamii.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Wahitimu wa Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Kozi namba 28 na Uongozi Daraja la Pili Kozi namba 48 ya mwaka 2025/2026 katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) Ukonga Jijini Dar es Salaam.

.......................................

TASWIRA MPYA YA MAGEREZA TANZANIA

Kwa ujumla, mageuzi yanayoendelea ndani ya Jeshi la Magereza yanaonyesha Tanzania inaanza kujenga mfumo mpya wa haki jinai unaounganisha utu wa binadamu, elimu, teknolojia, uzalishaji na maendeleo ya kijamii.

Katika mfumo huo mpya, maofisa wa Magereza hawabaki tena kuwa walinzi wa wafungwa pekee, bali wanageuka kuwa walimu, washauri na wajenzi wa mabadiliko ya kijamii. Hii ni tofauti kubwa na mfumo wa zamani wa magereza uliorithiwa kutoka ukoloni ambapo askari alionekana zaidi kama msimamizi wa adhabu na nidhamu.

Katika falsafa ya kisasa ya urekebishaji, askari wa Magereza anatakiwa kumsaidia mfungwa kubadili mtazamo wa maisha, kupata maarifa mapya na kujiandaa kurejea katika jamii akiwa mtu mwenye mchango chanya.

Kwa mfano, Japan, mfumo wa magereza umejengwa katika misingi ya nidhamu, elimu na malezi ya tabia.

Maofisa wa Magereza hushiriki moja kwa moja katika kufundisha maadili ya kazi, usafi, muda na uwajibikaji. Wafungwa wengi hupewa ratiba maalumu za kazi, elimu na mafunzo ya ufundi chini ya usimamizi wa karibu wa maofisa wa Magereza wenyewe.

Mfumo huo umeisaidia Japan kuwa na kiwango cha chini cha uhalifu wa kujirudia ukilinganisha na mataifa mengi duniani.

Mfano mwingine ni nchini Canada ambapo mfumo wa Correctional Service Canada unawataka maofisa wa Magereza kuwa sehemu ya mchakato wa marekebisho ya wafungwa.

Askari hupatiwa mafunzo ya saikolojia ya tabia, ushauri nasaha na namna ya kushughulika na watu wenye changamoto tofauti za kijamii. Ndani ya mfumo huo, askari si mtu wa kutoa amri pekee, bali anakuwa mshauri anayemsaidia mfungwa kujenga mpango wa maisha ya baada ya kifungo.

Katika baadhi ya magereza ya Canada, maofisa hushiriki pamoja na wafungwa kwenye programu za elimu, mafunzo ya kazi na hata mijadala ya kijamii inayolenga kujenga uwajibikaji na kuondoa tabia ya vurugu.

Nchini Singapore, mfumo wa magereza umejengwa katika falsafa inayojulikana kama “Captains of Lives”. Kupitia mfumo huo, maofisa wa Magereza wanafundishwa kuona kazi yao si kufunga watu pekee, bali kusaidia kubadili maisha yao.

Serikali ya Singapore inaamini askari wa Magereza ni viongozi wa mabadiliko ya kijamii wanaoweza kusaidia kupunguza uhalifu kwa kuwajenga wafungwa kitabia na kitaaluma.

Kutokana na mfumo huo, wafungwa wengi nchini humo hupata mafunzo ya teknolojia, biashara ndogo, ufundi na elimu ya kawaida kabla ya kutoka gerezani.

Mfano mwingine unaotajwa sana ni nchini Netherlands ambako baadhi ya magereza yamepunguza matumizi ya mfumo mkali wa kufungia wafungwa muda wote na badala yake kuwekeza katika elimu, ushauri wa kisaikolojia na maandalizi ya maisha ya baada ya kifungo.Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Mkunda na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camillius Wambura wakiwa kwenye hafla hiyo.

.....................................................

Maofisa wa Magereza katika mfumo hufanya kazi karibu sana na wafungwa kama walezi na wasimamizi wa maendeleo yao binafsi.

Kutokana na mafanikio ya mfumo huo, baadhi ya Magereza nchini humo yamefungwa kutokana na kupungua kwa idadi ya wafungwa na viwango vya kurudia uhalifu.

Hata Tanzania sasa inaanza kuelekea katika mfumo huo wa kimataifa.

Kupitia Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania, maofisa wa Magereza wanafundishwa sayansi ya urekebishaji, usimamizi wa wafungwa kwa kuzingatia utu wa binadamu na mbinu za kisasa za marekebisho ya kijamii.

Hivyo, Askari wa Magereza wa sasa anaanza kuwa zaidi ya mlinzi wa gereza. Anakuwa:

 mwalimu wa stadi za maisha,  mshauri wa kitabia,

 mlezi wa matumaini ya mfungwa, na daraja la kumrudisha mfungwa katika jamii akiwa raia mwema na mwenye uwezo wa kujitegemea.

Kwa mtazamo wa maendeleo, huu ndiyo mfumo ambao mataifa mengi yaliyoendelea yameanza kuutumia kwa sababu unaamini kuwa usalama wa jamii haupatikani kwa adhabu kali pekee, bali kwa kujenga binadamu mwenye maadili, elimu na matumaini ya maisha mapya.

Na huenda hiyo ndiyo sababu kubwa iliyofanya Jeshi la Magereza Tanzania kuona umuhimu wa kutoa tuzo hiyo kwa mara ya kwanza katika historia yake — kama ishara ya kuthamini mageuzi yanayobadili si tu magereza, bali pia falsafa nzima ya maendeleo ya binadamu Tanzania.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na viongozi mbalimbali mara baada ya kuwasili katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) Ukonga.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mfungwa Bi. Irene Mseluka ambaye amepata ujuzi wa kushona bidhaa mbalimbali za ngozi na vitambaa akiwa gerezani katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) Ukonga Jijini Dar es Salaam.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikagua Gwaride. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mfungwa Bi. Grace Chiduo ambaye amepata ujuzi wa kushona bidhaa mbalimbali akiwa gerezani katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) Ukonga Jijini Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mfungwa Clemensia Cosmas Mirembe (20) kwenye hafla hiyo. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama wakati wimbo wa Taifa ukiimbwa kwenye hafla hiyo.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Wafungwa waliopata ujuzi wa ushonaji Gerezani Bi. Grace Chiduo (kulia) na Bi. Irene Mseluka (kushoto) katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) Ukonga Jijini Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na viongozi mbalimbali mara baada ya kuwasili katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) Ukonga Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Mei, 2026 kwa ajili ya kuhitimisha Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Kozi namba 28 na Uongozi Daraja la Pili Kozi namba 48 kwa Mwaka 2025/2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Kamishna Jenerali wa Magereza Jeremia Yoram Katungu kwenye hafla hiyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoa vyeti kwa Wahitimu waliofanya vizuri kwenye Mafunzo hayo. 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoa vyeti kwa Wahitimu waliofanya vizuri kwenye Mafunzo hayo. 
Gwaride likipita mbele kwa mwendo wa pole kabla ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhitimisha Mafunzo hayo. 
Gwaride likipita kwa mwendo wa haraka mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhitimisha Mafunzo hayo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mfungwa Bw.  Lista Chisoma ambaye amepata ujuzi wa kushona bidhaa mbalimbali za ngozi na vitambaa wakati akiwa gerezani, katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) Ukonga Jijini Dar es Salaam.Viongozi wakishuhudia matukio mbalimbali katika uwanja wa Gwaride wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) Ukonga Jijini Dar es Salaam. 
Kikundi cha Wanawake wa Jeshi la Magereza kikionesha onesho Maalumu katika uwanja wa Gwaride wakati wa kuhitimisha Mafunzo hayo. 
Onesho maalumu likiendelea kuoneshwa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiangalia zawadi ya mabegi aliyopewa ambayo yametengenezwa na Wafungwa katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) Ukonga Jijini Dar es Salaam.
Wahitimu wa Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Kozi namba 28 na Uongozi Daraja la Pili Kozi namba 48 ya mwaka 2025/2026 wakiwa kwenye mkutano katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) Ukonga Jijini Dar es Salaam.
Wahitimu wa Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Kozi namba 28 na Uongozi Daraja la Pili Kozi namba 48 ya mwaka 2025/2026 wakiwa kwenye mkutano katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) Ukonga.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na kikundi cha burudani cha Wafungwa na Askari Magereza kwenye hafla ya kuhitimisha Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Kozi namba 28 na Uongozi Daraja la Pili Kozi namba 48 ya mwaka 2025/2026 katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) Ukonga Jijini Dar es Salaam.Wahitimu wa Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Kozi namba 28 na Uongozi Daraja la Pili Kozi namba 48 ya mwaka 2025/2026 wakivalishana vyeo katika hafla hiyo.

.................................
Makala haya yameandaliwa na Dotto Mwaibale 
Msimamizi Mkuu wa Uenezi CCM Blog
  simu namba 0754362990.

Post a Comment

0 Comments