SHULE YA DR. ALI MOHAMED SHEIN YAJIPANGA KUKABILIANA NA MVUA ZA EL NINO

SHULE YA DR. ALI MOHAMED SHEIN YAJIPANGA KUKABILIANA NA MVUA ZA EL NINO

Mkuu wa shule hiyo, Jackson Maruma akitoa taarifa ya shule hiyo.
.........................................

SHULE ya Sekondari ya Dr. Ali Mohammed Shein iliyopo Kata ya Misughaa, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, imejipanga kukabiliana na mvua za El Niño kwa kuchukua hatua mbalimbali za kuhifadhi mazingira na kujiandaa na athari za mvua hizo. 


Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Shule hiyo, Jackson Maruma, wakati akisoma taarifa ya shule katika mahafali ya 17 ya Kidato cha Nne yaliyofanyika Oktoba 1, 2026. 

👇ANGALIA  VIDEO HAPA

“Hapa shuleni kwetu, pamoja na kujishughulisha na uboreshaji wa mazingira, kufuatia kuwepo kwa taarifa ya uwepo wa mvua za El Niño, sisi tulichukua hatua mapema kwa kupanda miti ya aina mbalimbali, ikiwemo mikorosho na migunga, katika maeneo ambayo yalionekana hayafai kwa kilimo,” alisema Maruma. 


Alisema uwepo wa miti hiyo una nafasi kubwa katika kuzuia mmomonyoko wa ardhi na kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua nyingi. 


Aidha, alisema shule hiyo imejipanga kupanda mazao yanayoweza kustahimili mvua nyingi, yakiwemo kunde na mbaazi, pamoja na kuongeza kilimo cha migomba. 


“Nitumie nafasi hii kuwashauri wananchi wa Misughaa kuwa, kama mvua hizo zitakuja, ni vema tusipande mahindi. Itakuwa hasara kwani hayawezi kustahimili mazingira yenye maji mengi. Hivyo, tuangalie mazao ambayo yatakabiliana na hali ya hewa itakayojitokeza. Liwake jua au mvua iwe sawa, wapande mihogo, mbaazi, yaani mazao ambayo hayataathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa,” alisema. 

Alisema hatua hiyo itaendelea kusaidia kuhakikisha shule inakuwa na chakula cha kutosha kwa ajili ya wanafunzi, hasa endapo kutatokea changamoto ya upatikanaji wa chakula katika jamii. 


Ufaulu


Akitoa taarifa ya maendeleo ya shule hiyo, Maruma alisema shule imeendelea kufanya vizuri katika ufaulu kwa miaka kadhaa mfululizo, jambo ambalo alisema wanajivunia. 


Alisema mwaka 2019 ufaulu ulikuwa asilimia 94, mwaka 2020 asilimia 97, mwaka 2021 asilimia 100, mwaka 2022 asilimia 100, mwaka 2023 asilimia 96 na mwaka 2024 asilimia 96. 


“Shule yetu haijashuka kiufaulu. Mwaka 2021 na 2022 imeweza kufaulisha kwa asilimia 100 kwa Kidato cha Nne. Hili ni jambo jema,” alisema. 

 

Miundombinu


Akizungumzia miundombinu, Maruma alisema shule hiyo ilipata msaada wa fedha za Uviko-19 na kujenga madarasa mawili pamoja na ofisi moja ya walimu. 


Alisema kupitia Serikali Kuu walifanikiwa kupata chumba kimoja cha darasa na kujenga matundu 10 ya vyoo vya wavulana na wasichana kupitia fedha za tozo. 


“Mwaka wa fedha 2024/2025 tulifanikiwa kupata fedha kwa ajili ya ujenzi wa chumba kimoja cha darasa chini ya Mradi wa SEQUIP na mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali pia ilitupatia Shilingi milioni 30 kwa ajili ya kukamilisha chumba kimoja cha maabara,” alisema Maruma. 

 

Alisema kwa hatua hiyo hawana budi kumshukuru aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa miradi iliyotolewa katika shule hiyo. 


Lishe shuleni


Maruma alisema kwa kushirikiana na wazazi na jamii ya Misughaa, wamefanikiwa kutoa chakula kwa wanafunzi wote kwa miaka mitano mfululizo. 


Alisema mwaka jana walifanikiwa kukusanya magunia 100 ya mahindi pamoja na kilo 1,553 za maharage, huku mwaka huu wakikusanya magunia 124 ya mahindi. 


Alisema hatua hiyo imefanikisha upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi na kuwawezesha kupata muda wa kutosha wa kujisomea. 


Maji


Akizungumzia huduma ya maji, Maruma alisema shule hiyo imefanikiwa kuvuta maji kutoka Parokia ya Mt. Yohanne II Misughaa, ambapo maji hayo yamekuwa yakitumika katika shughuli mbalimbali za shule pamoja na hosteli. 


“Upatikanaji wa huduma ya maji umesaidia kutatua changamoto kubwa iliyokuwa ikiwakabili wanafunzi, ambapo wanafunzi wakiwa shuleni au hosteli walilazimika kusitisha shughuli za masomo na kwenda kuchota maji mtoni. 

 

Hali hiyo ilipelekea kuharibika kwa ratiba za vipindi madarasani na kwa kiasi kikubwa kuathiri shughuli za ufundishaji na ujifunzaji kwa walimu na wanafunzi,” alisema. 


Mazingira


Akizungumzia mazingira, alisema shule hiyo imefanikiwa kuanzisha mradi wa kitalu cha miti kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), ambapo wamezalisha miti zaidi ya 10,000. 


Alisema miti hiyo imesambazwa katika taasisi mbalimbali ndani ya Kata ya Misughaa kwa lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira na kukabiliana na ongezeko la hewa ya ukaa duniani. 


“Katika taasisi yetu tumefanikiwa kupanda miti mbalimbali, mikorosho 228, mipapai 67, miti-maji 60, miarobaini 400, milonge 44 na migunga 363 maalumu kwa ajili ya ufugaji wa nyuki,” alisema. 

 

Michezo


Akizungumzia michezo, Maruma alisema shule hiyo imefanikiwa kufanya ziara mbalimbali za kimichezo ambazo zimewasaidia wanafunzi kukuza vipaji, undugu, upendo na mshikamano baina ya shule hiyo na shule nyingine. 


Alisema katika mashindano ya UMISETA mwaka huu, shule hiyo imefanikiwa kupeleka wanafunzi watatu katika ngazi ya mkoa kuwakilisha wilaya yao. 


Aidha, alisema shule hiyo imefanikiwa kuanzisha kituo cha kukuza na kuendeleza vipaji vya mpira wa miguu chenye usajili namba NSC 13011, MISUGHAA SPORTS CENTRE. 


Alisema malengo ya kituo hicho ni kuinua na kutengeneza vipaji vitakavyotumika shuleni, kitaifa hadi kufikia ngazi za kimataifa. 


Changamoto


Akizungumza kuhusu baadhi ya changamoto zinazowakabili, Maruma alitaja upungufu mkubwa wa nyumba za walimu, hali inayofanya walimu kuishi katika mazingira magumu. 


Changamoto nyingine ni ukosefu wa ukumbi wa kufanyia mikutano na shughuli mbalimbali za shule, zikiwemo mitihani, mihadhara na shughuli nyingine za kitaaluma. 


Alitaja pia uhaba wa samani za kukalia na kujisomea wanafunzi pamoja na ukosefu wa hosteli ya kutosha kukidhi mahitaji ya wanafunzi wanaotakiwa kukaa hosteli, hasa kwa kuzingatia mtawanyiko na jiografia ya Kata ya Misughaa. 


Alisema shule hiyo pia ina madarasa 10 yaliyochakaa ambayo hayakidhi vigezo vya kuendeshea shughuli za ufundishaji na ujifunzaji kwa kuwa hayana madirisha ya kisasa, sakafu imara yenye vigae (tiles), mbao sanifu za kufundishia na mahitaji mengine muhimu. 


Maruma alisema jengo la utawala lililopo ni la muundo wa zamani na linahitaji ukarabati mkubwa. 


Alisema kwa tathmini ya haraka, gharama za ukarabati zinakaribiana na gharama za ujenzi wa jengo jipya na la kisasa la utawala. 


Wahitimu watakiwa kutosubiri matokeo


Mkurugenzi wa Kampuni ya Taish Farm Co. Ltd, Hassan Tatt, akizungumza kwa niaba ya mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Manunuzi wa Bohari ya Dawa (MSD), Hamis Mpinda, aliwataka wahitimu hao kutosubiri matokeo bali matokeo yawakute wakiwa wamejipanga. 


“Wakati umemaliza mtihani, usikutwe huna kitu. Matokeo yakukute una kitu; yakukute una kuku, yakukute una mbogamboga, matuta saba, hata una ng’ombe, lakini yakukute una taaluma ya kutosha wakati unasubiri matokeo,” alisema Tatt. 

 

Tatt aliwauliza wahitimu hao kwa nini wasubiri matokeo, akisema wanapaswa kutumia muda huo kujipanga ili watakapopata matokeo wawe tayari kukabiliana na hatua inayofuata. 


Aidha, Tatt alisema mgeni rasmi ameguswa na changamoto zilizowasilishwa na Mkuu wa Shule, zikiwemo changamoto katika sekta ya michezo. 


Alisema mgeni rasmi atanunua mipira 15, huku mwakilishi wake katika mahafali hayo akiahidi kuongeza mipira mingine mitano. 


Alisema mgeni rasmi atasaidia maombi mengine ya shule kulingana na uwezo na kile atakachojaliwa na Mwenyezi Mungu. 


Wanafunzi 84 wahitimu


Wahitimu hao, wakitoa historia ya shule hiyo, walisema walianza Kidato cha Kwanza mwaka 2023 wakiwa takribani wanafunzi 148, lakini hadi wanahitimu wamebaki wanafunzi 84. 


Walisema hali hiyo imetokana na sababu mbalimbali zilizo nje ya uwezo wao, zikiwemo baadhi ya wanafunzi kuhama shule na wengine kuacha shule. 


Walisema wanafunzi 23 walihama shule, mmoja alifariki dunia, huku wanafunzi 60 wakiacha shule. 


Mahafali hayo yalipambwa na burudani mbalimbali zilizotolewa na wahitimu pamoja na wanafunzi wengine, huku yakihudhuriwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wageni waalikwa na walimu kutoka shule za jirani.

Wahitimu wa kidato cha nne wakiandamana kuelekea eneo la Mahafali ya 17 yaaliyofanyika Oktoba 1, 2026.
Vijana wa Skauti wakiongoza maandamano hayo.
Skauti wakionesha ukakamavu wao wakati wa mahafali hayo.
Vijana wa Skauti wakiongoza maandamano hayo.
Vijana wa Skauti wakimvika Skafu mwakilishi wa Mgeni Rasmi Mkurugenzi wa Kampuni ya Taish Farm Co. Ltd, Hassan Tatt alipowasili kwenye mahafali hayo.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Dr. Ali Mohammed Shein akisalimiana na Mkurugenzi wa Kampuni ya Taish Farm Co. Ltd, Hassan Tatt mara baada ya kuwasili kwenye Mahafali hayo
Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, Athumani Kitiku (kulia), akisalimiana na Mwakilishi wa mgeni rasmi Mkurugenzi wa Kampuni ya Taish Farm Co. Ltd, Hassan Tatt. Katikati Mkuu wa Shule hiyo, Jackson Muruma.
Vijana wa Skauti wakimvika Skafu Mwanzilishi wa Skauti katika shule hiyo, Mwalimu Steven Mwakisole, katika mahafali hayo.
Mgeni rasmi akiwasalimia wananchi
Viongozi wakisubiri kumpokea mgeni rasmi.
Wimbo wa Taifa ukiimbwa.
Mkuu wa shule hiyo, Jackson Maruma akitoa taarifa ya shule hiyo.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Taish Farm Co. Ltd, Hassan Tatt, akisisitiza jambo kwenye mahafali hayo.
Meneja wa Mpinda's Agr Project, Marcoa Kitindi akizungumza kwenye mahafali hayo.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Chaa Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Ikungi Ikimbia  Nkhangaa, akizungumza kwenye mahafali hayo.


Mshereheshaji namba moja Jumanne Maulid Idd (maarufu kwa jina la J4) akiwajibika.
Mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo, Athumani Kitiku, akizungumza.
Mjumbe wa Bodi wa shule hiyo Fidelis Yunde (katikati), akiendesha harambee ya kupata fedha za kumsaidia Mwandishi wa Kitabu cha Binti Jasiri Bi. ni binti aliyesoma Dr Shein (kushoto) ili kupata fedha za kuchapisha kitabu hicho. Kulia ni Afisa Elimu Kata ya Misughaa, Eliaita Simon

Mwandishi wa Kitabu cha Binti Jasiri Bi. Asia na ndugu yake wakilia kufuatia kitendo cha kuchangiwa fedha zaidi ya shilingi 446,000 katika harambee iliyofanyika kwenye mahafali hayo ya kidato cha nne.
Mwandishi wa Kitaabu cha Binti Jasiri Bi Asia, akikabidhiwa fedha alizochangiwa wakati wa mahfali hayo kwa ajili ya kuchapa kitabu hicho.
Wazazi wakitoa nasaha zao
Nasaha zikitolewa kwa wahitimu.
Mwandishi wa Kitabu cha Binti Jasiri, Bi. Asia akionesha kitabu hicho.
Mwandishi wa Kitabu cha Binti Jasiri, Bi. Asia, akimkabidhi kitabu hicho mgeni rasmi
Mkuu wa shule hiyo akisisitiza jambo kwenye mahafali hayo
Meza kuu wakijadiliana namna ya kumsaidia Mwandishi wa Kitabu Jinsi Jasiri, Bi. Asia kupata fedha na kuchapa kitabu hicho. Katika harambee iliyofanyika katika mahafali hayo zilipatikana zaidi ya Shilingi 446,000 na kumfanya mwandishi huyo pamoja na mama yake kutokwa machozi kwa tendo hilo ambalo hawakulitegemea.

Fasheni Shoo ya kijana akiwa amevaa vazi la watu kutoka Unguja Zanzibar likinogesha mahafali hayo.
Skauti Emanuel Salim na Cecilia Bure wakielezea masuala ya mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa.
Wanafunzi wakiimba shairi
Cheti kikikabidhiwa kwa Mwalimu.
Mwalimu Protas Hema aakikabidhiwa cheti.
Mhitimu Hidaya Ramadhani aaakikabidhiwa cheti
Mhitimu Hamisi Ramadhani akikabidhiwa cheti
Mwalimu Jacob Tango akikabidhiwa cheti.
Fasheni Shoo. Mama lishe wakiwa kazini.
Fasheni Shoo. Wahandisi wakiwa kazini.
Fasheni Shoo, Mmachinga akipita mtaani kutafuta wateja.
Fasheni shoo ya Baba na Mama wa Kikristo wakienda kanisani.
Fasheni shoo. Daktari na Muuguzi wakiwa kazini
Fasheni shoo ya wakulima ikipita uwanjani
Burudani likiendelea
Msanii wa Kizazi Kipya ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili wa shule hiyo Gabriel Petro, akiwajibika ipasavyo.
Burudani ikiendelea.
Walimu pamoja na wanafunzi wakiserebuka ngoma ya Asili ya Kabila laa Wahaya.
Mshereheshaji namba moja Jumanne Maulid Idd (maarufu kwa jina la J4) akiwajibika.
Wahitimu wakiimba wimbo maalum wa kuaga. 
Wahitimu wakiimba wimbo maalum wa kuaga. 
Wahitimu wakiwa kwenye mahafali hayo.
Walimu na wageni waalikwa wakiwa kwenye mahafali hayo
Wageni waalikwa wakiwa kwenye mahafali hayo
Wageni waalikwa , wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wa wahitimu hao wakiwa kwenye mahafaali hayo.
Wanafunzi wakiwa kwenye mahafali hayo.
Picha za matukio mbalimbali zikipigwa.
Walimu wa shule hiyo wakiwa kwenye mahafali hayo.
Walimu Wanaume wa shule hiyo wakitambulishwa kwenye mahafali hayo.
Walimu Wanawake wakiwa kwenye mahafali hayo wakijitambulisha, Kutoka kushoto ni Sarah Mafwimbo, Fransisca John, Elineema Mwaya, Rebeca Mataro na Ombeni Samson.
Mgeni rasmi na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja
Picha ya pamoja
Pichaa ya pamoja baada ya kuonesha Fasheni Shoo.
Taswira ya mahfali hayo
Walimu wakijadiliana jambo. Kutoka kushoto ni Protas Hema, Jacob Tango na Pascal Fisso.
Wahitimu wakitoa zawadi kwa walimu wao.
Walimu wakionesha umahiri wa kusakata rhumba baada ya kukabidhiwa zawadi.
-----------------------------
Imeandaliwa na Mtandao wa Singidaniblog

0754362990 / 0787013988

Post a Comment

0 Comments