MBUNGE DK. MECKTRIDIS MDAKU APEWA TUZO YA HESHIMA KWA KUWAWEZESHA VIJANA WA MALINYI

MBUNGE DK. MECKTRIDIS MDAKU APEWA TUZO YA HESHIMA KWA KUWAWEZESHA VIJANA WA MALINYI


 Mbunge wa Jimbo la Malinyi, Dk. Mecktridis Mdaku, ametunukiwa Tuzo ya Heshima na Mkuu wa Chuo cha Ufundi FDC Sofi, Ndugu Sukaku Jacob, kwa kutambua na kuthamini mchango wake katika juhudi za kuwawezesha vijana wa Malinyi kupata ujuzi na fursa za kujikwamua kiuchumi.

Tuzo hiyo imetolewa wakati wa Mahafali ya 48 ya Chuo cha FDC Sofi yaliyofanyika katika chuo hicho, ambapo jumla ya vijana 150 wamehitimu mafunzo ya ufundi katika fani mbalimbali, kati ya vijana 500 wanaonufaika na mpango wa mafunzo unaolenga kuwawezesha kupata ujuzi wa kitaalamu na kujiajiri.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Chuo hicho, Ndugu Sukaku Jacob, amesema tuzo hiyo ni sehemu ya kutambua mchango wa Dkt. Mdaku katika kuunga mkono juhudi za kuwaandaa vijana kwa kuwapatia elimu ya ufundi na ujuzi unaoweza kuwawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

Amesema uwezeshaji wa vijana kupitia elimu ya ufundi ni hatua muhimu katika kukabiliana na changamoto ya ajira na kuongeza fursa za vijana kushiriki katika uzalishaji na maendeleo ya jamii.

Mahafali hayo pia yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi, Mkuu wa Wilaya ya Malinyi pamoja na viongozi wengine wa Serikali na wadau wa maendeleo.

Katika hotuba zake, viongozi hao wameendelea kusisitiza umuhimu wa vijana kutumia fursa za mafunzo ya ufundi na ujuzi wanazopata ili kujiajiri, kuanzisha shughuli za uzalishaji na kuchangia maendeleo ya familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Mahafali hayo yamekuja wakati ambapo juhudi mbalimbali zinaendelea katika Jimbo la Malinyi za kuwawezesha vijana kupata elimu, ujuzi na fursa za kiuchumi, ikiwa ni sehemu ya kujenga msingi wa maendeleo endelevu na kuongeza ushiriki wa vijana katika uchumi. 

Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo Ndugu Eric Mselo amemshukuru Mbunge Dkt Mecktridis Mdaku kwa moyo wake wa upendo wa kuwawezesha vijana kupata fursa mbalimbali za kujiendeleza kiuchumi na kijamii. 

Mafunzo haya yatakuwa na faida kubwa kwangu kwani yatanijengea uwezowa kujiajiri mwenyewe. 

Mafunzo ya ufundi katika Chuo cha FDC - Sofi ni sehemu ya mkakati wa Mhe. Mbunge Dkt. Mecktridis Mdaku katika kuwawezesha vijana wa Malinyi kuweza kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi ili waondokane na utegemezi kwenye familia na kuwa na tija katika maisha yao na jamii yao kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments