MAVETERANI WA UVCCM DAR WAMUENZI BABA WA TAIFA

MAVETERANI WA UVCCM DAR WAMUENZI BABA WA TAIFA

Na Mwandishi Wetu

KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  CCM  Jeremiah Wambura,  amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuwaenzi  maveterani wa Umoja  wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM) kwa kutambua mchango wao hasa katika kupigania  uhuru wa Tanganyika.

Wambura,ambaye alikuwa Mjumbe wa Baraza Kuu la Wazazi Taifa, amesema  ni muhimu jamii kutambua na kuenzi mchango wa maveterani  ambao waliandika historia ya  ambayo inatakiwa kuendelezwa  kwa vizazi vijavyo.

Ameyasema hayo, leo katika  kumbukizi ya  miaka 27 ya kifo cha hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julis Nyerere,  iliyoandaliwa na Maveterani wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Dar es Salaam.

Kumbukizi hiyo imefanyika katika Ofisi za UVCCM Taifa, Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo maveterani kutoka wilaya zote za mkoa huo, wamekusanyika kufanya dua na kumuenzi hayati Baba wa Taifa kwa kusikiliza hotuba zake na kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu  maisha ya Mwalimu enzi za uhai wake.

Wambura ambaye  pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mazingira na Ufugaji Tanzania (CHAMAUTA)  ameeleza,  ni kumbukizi ya hayati Baba wa Taifa  ambaye ni mwasisi wa taifa na kiongozi wa harakati za ukombozi  ni ya kipekee huku  maveterani hao  ambao walijitolea maisha yao kupambania taifa wanapaswa kuenziwa hasa katika dhifa za mashujaa.

Katika  kuenzi  mchango wao, Wambura alikabidhi kiasi cha sh. 200,000 kwaajili ya kufungua akauti maalumu ya maveterani wa UVCCM, ambayo itawafanya kujiendesha na kuratibu shughuli zao  kwa urahisi na ufanisi.

Wambura ametaka akaunti hiyo kufunguliwa mara moja huku pia akiahidi kuwakatia bima ya afya mavetenari watu ambao wako hai, walioshiriki kikamilifu katika mapambano ya kudai uhuru ili wapate huduma za afya kwa urahisi.

"Pia nitajitolea kuandaa mkutano wa maveterani wa UVCCM wa kitaifa.,"amebainisha kada huyo.

Awali Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Stanley Mkandawile, aliwataka maveterani na viongozi wa Chama  kuendelea kuwaelimisha vijana kuhusu umuhimu wa kudumisha amani, umoja na mshikamano wa taifa, huku wakipinga udini na migawanyiko inayoweza kuligawa taifa.

Ameeleza  Hayati Baba wa Taifa  ameacha urithi wa amani, upendo na umoja uliowawezesha Watanzania wa makabila  tofauti  kuishi pamoja kama familia moja.

Alisema misingi hiyo imejenga taifa lenye lugha moja ya Kiswahili na Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar, hivyo ni wajibu wa Watanzania wote kuuenzi na kuulinda.

Mkandawile amebainisha  Mwalimu Nyerere alikuwa mtetezi wa haki za wanyonge, aliyeshiriki katika kuunga mkono harakati za ukombozi katika nchi mbalimbali za Afrika hivyo Watanzania wanapaswa kuendeleza misingi yake ya upendo, haki, umoja na mshikamano kuhakikisha amani inaendelea kudumu nchini.

Kwa upande wake, Katibu wa Veterani wa UVCCM, Yahya Ngoma, ameeleza  vijana waliojitolea katika kukitumikia Chama na kupigania uhuru hawakulipwa mishahara, bali walifanya kazi hizo kwa uzalendo na dhamira ya kuona taifa linapata uhuru  hivyo aliwataka vijana wa sasa kujifunza kutoka kwao kuheshimu maadili na misingi ya taifa na kuepuka makundi yanayoweza kuhatarisha amani na mshikamano wa nchi.

Naye Mwenyekiti wa Veterani wa UVCCM Wilaya ya Kinondoni, Ahmad Mhando amesema  vijana wanapaswa kuwasikiliza wazee kwa kuwa wana uzoefu unaoweza kuwaongoza katika maisha.

Mwalimu wa Nyerere alizaliwa mwaka 1922 na kufariki dunia Oktoba 14, mwaka 1999.

Picha ya pamoja
Picha ya pamoja
Wakimuombea dua Baba wa Taifa
 

Post a Comment

0 Comments