MENEJA HOTELI YA MOUNT USAMBARA TANGA AHIMIZA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UWEKEZAJI

MENEJA HOTELI YA MOUNT USAMBARA TANGA AHIMIZA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UWEKEZAJI

Meneja wa Hoteli ya Mount Usambara, Jijini Tanga,  Juma Mhando, akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani), Septemba 10, 2026, kuhusu fursa mbalimbali wanazozipata kutokana na miradi mikubwa ya kimkakati iliyopo mkoani humo. 

............................

MENEJA wa Hoteli ya Mount Usambara Jijini Tanga, Juma Mhando, amewataka wananchi na wafanyabiashara kuchangamkia fursa za kiuchumi kutokana na uwekezaji mkubwa wa kimkakati unaoendelea mkoani humo. 

Mhando aliyasema hayo Septemba 10, 2026, katika mkutano maalumu na waandishi wa habari ambao walitaka kujua namna hoteli zinavyonufaika na wageni na wawekezaji waliopo mkoani Tanga. 

“Kwa upande wa Serikali tunaipongeza kwani imetuwekea mazingira mazuri na wezeshi kutokana na miradi mikubwa ya kimkakati inayoendelea mkoa wetu,” alisema Mhando. 

Alisema viongozi mbalimbali wa kitaifa na wa mkoa wamekuwa wakiwahimiza wananchi na wafanyabiashara wa Mkoa wa Tanga kuchangamkia fursa za kiuchumi kutokana na uwekezaji huo. 

“Kutokana na uwekezaji huo, hali ya kibiashara siyo mbaya ukilinganisha na hapo awali kabla ya kuanza kwa uwekezaji wa maboresho ya Bandari na Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi EACOP kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga.” 

Alisema wageni ambao wapo na wanaofikia kwenye hoteli yao kutoka nchi mbalimbali ni wengi, jambo ambalo limeongeza uchumi wao. 

Mhando alisema kutokana na wingi wa wageni hao kumekuwa na upungufu wa bidhaa za chakula, kwani unaweza kufika sokoni ukazikosa, ambapo alitoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara kuleta kwa wingi bidhaa ili kukabiliana na uhitaji. 

“Unaweza kwenda sokoni ukakosa mayai na nyama na mahitaji mengine. Ni fursa ya wakulima na wafugaji kuongeza ufugaji wa kuku wa nyama na wa mayai,” alisema. 

Alitaja baadhi ya changamoto kuwa Mkoa wa Tanga bidhaa inaweza kuwepo, lakini ukifika dukani unakuta duka limefungwa zaidi ya saa tatu, hivyo aliomba wafanyabiashara kuweka utaratibu fulani ambao utafanya maduka hayo kuendelea kuwa wazi ili watu waendelee kupata mahitaji na wao kukuza biashara zao.

Mhando alisema kuwa uwekezaji wa Bomba la mafuta na maboresho ya bandari vimechangia kwa kiasi kikubwa mji kuchagamka kibishara kwa wananchi na wafanyabiashara wa mahoteli kwa kuwapata wageni kutoka nchi mbalimbali duniani.

.................

Habari hii imeandikwa na Dotto Mwaibale namba ya simu 0754362990.

Post a Comment

0 Comments