LUHANGA WAPELEKA KILIO KWA MBUNGE MASABURI

LUHANGA WAPELEKA KILIO KWA MBUNGE MASABURI

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Luhanga, Ally Likali aliyevaa kofia akishiriana na wananchi kung'oa visiki kwa lengo la kupanua barabara.
.........................................

Na Mwandishi Wetu.      

WANANCHI wa Luhanga, Kata ya Msongola, Ilala,  Dar es Salaam, wameiomba Serikali kupitia Mbunge wa Jimbo la Kivule, Ojambi Masaburi, wakitaka  kuwawezesha kupata  greda ili waweze kutengeneza miundo mbinu ya barabara.

Tayari wananchi wa Luhanga wamejitolea kuchanga fedha kwa ajili ya kununua mafuta zaidi ya lita 200, lakini changamoto waliyonayo ni greda la kuchonga barabara zao. 

Akizungumza Agosti 13, mwaka huu, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Luhanga, Ally Likali, alisema kuwa  changamoto kubwa  wanayokabiliwa kwa sasa ni miundombinu mibovu ya barabara.    Likali alisema kuwa baadhi ya barabara hazipitiki, licha ya wananchi kujitolea nguvu zao  kutengeneza sehemu korofi.

  Alisema kuwa pamoja na wananchi wake kujitolea nguvu zao kwa ajili ya kutengeneza barabara, lakini wamenunua mafuta zaidi ya lita 200,  changamoto iliyokuwapo ni kupata greda la kuchonga barabara hizo za mitaa. 

"Tunaiomba Serikali itusaidie kupata greda ili kuunga mkono juhudi za wananchi za kujitolea," alisema Likali.

Mwenyekiti huyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema kuwa tayari amewasiliana na diwani wa Kata ya Msongola, Madagalena Nyandole na ofisi ya mbunge wa jimbo lao la Kivule  ili waweze kuwasaidia kupata greda la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Alisema kuwa kwa sasa wanasubiri jitihada zinazofanywa na waheshimiwa hao katika upatikanaji wa gari hilo, kwa mafuta wanayo. 

Mwenyekiti huyo ambaye juzi aliungana na wananchi wake kung'oa visiki kwa ajili ya kupitisha barabara, alisema kuwa kumekuwapo uharibifu mkubwa wa miundombinu unaochangiwa na magari makubwa ya kubeba mchanga.

Likali alisema kuwa kutokana na magari hayo kubeba mzigo mkubwa wa mchanga kuna sababisha barabara kuchimbika na kuweka matuta.

Alisema kuwa kutokana na sababu hiyo, bajaji na magari madogo hayawezi kupita, hivyo usafiri kuwa mgumu.

  Kwa upande wake, Mohammed Matiku alimpongeza  m wenyekiti wao wa serikali ya mtaa kutokana na kazi nzuri ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Matika alisema kuwa hawakufanya makosa kumchagua mwenyekiti huyo, kwani wamekuwa ni mfano wa kuigwa na kujifunza.
 

Post a Comment

0 Comments