WAZIRI MKUU DK. MWIGULU AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI JENGO LA TAALUMA TIA SINGIDA

WAZIRI MKUU DK. MWIGULU AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI JENGO LA TAALUMA TIA SINGIDA

AIPONGEZA BODI YA USHAURI  TIA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mwigulu Nchemba (kulia), akivuta pazia kuashiria uwekaji wa Jiwe la Msingi Ujenzi wa Jengo la Taaluma Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Kampasi ya Singida Juni 27, 2026. Kushoto ni Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde.
....................................

WAZIRI MKUU, Dk. Mwigulu Nchemba ameweka jiwe la msingi la jengo la Taaluma na ameipongeza Bodi ya Ushauri ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kwa hatua kubwa ya ujenzi wa Jengo la Taaluma linalojengwa mkoani Singida.

Dk. Mwigulu ametoa pongezi hizo Juni 27, 2026) alipokuwa akiweka jiwe la msingi la Jengo la Taaluma la TIA,  Kampasi ya Singida wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Singida.

“Jengo hili la chuo chetu lipo Singida ni hatua kubwa sana. Hongereni bodi, hongereni chuo, hongereni wanafunzi,  Tunawatakia kila la heri," alisema Dk. Mwigulu.

Mwigulu alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika elimu ya juu kwa kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia ili kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi na uwezo wa kuchangia maendeleo ya Taifa.

Alisema ujenzi wa jengo hilo ni dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na  Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuboresha mazingira ya elimu ya juu na kusogeza huduma hizo kwa wananchi. 

Dk. Mwigulu alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wahandisi, washauri na wakandarasi wazawa wanaotekeleza mradi huo na kueleza kuwa ushiriki wao unaonesha uwezo mkubwa katika kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo.

Waziri Mkuu Dk. Mwigulu aliongeza kuwa amefurahishwa kuona wahandisi wanaojenga mradi huo ni wazawa na Rais Samia alielekeza lazima tujenge uchumi unaomilikiwa na Watanzania na kujenga sekta binafsi ya ndani sambamba na uwekezaji kutoka nje.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde, alisema Serikali imeendelea kuipa kipaumbele sekta ya elimu kwa kuwekeza katika vyuo vya elimu ya juu ili kuongeza upatikanaji wa elimu bora, kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, kuimarisha tafiti, ubunifu na matumizi ya teknolojia pamoja na kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika utekelezaji wa dira ya maendeleo ya Taifa.

Alisema Wizara ya Fedha itaendelea kuhakikisha rasilimali za Serikali zinaelekezwa katika miradi yenye tija kwa wananchi, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA).

Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa. William Pallangyo akitoa taarifa ya ujenzi huo.

......................................

Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa. William Pallangyo, alisema jengo hilo la taaluma lina ukubwa wa mita za mraba 9,250 na litakuwa na kumbi za mafunzo, madarasa, kumbi za mihadhara, ukumbi wa mikutano pamoja na ofisi za watumishi.

Alisema kumbi za mafunzo zitakuwa mbili zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 325 ambapo ukumbi wa kwanza ukiingiza wanafunzi 175 na wa pili 150.

Aidha, Pallangyo alisema kuwa katika jengo hilo kutakuwa na madarasa 9 kati ya madarasa hayo manane yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 250 na darasa moja wanafunzi 300 kwa wakati mmoja.

"Katika jengo hilo kutakuwa na kumbi za mihadhara mbili na kila ukumbi utakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 450 na kufanya jumla ya wanafunzi 900 kwa wakati mmoja," alisema.

Akizungumzia ofisi alisema ni 15 na zitakuwa na uwezo wa kuchukua watumishi wawili kwa kila moja hivyo kuwa na watumishi 30 kwa wakati mmoja na pia kutakuwa na ukumbi mmoja wa mikutano ambao utakuwa na uwezo wa kuchukua watu 25.

Alisema mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 13.5 umefikia asilimia 63 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba, 2026.

Aidha, Pallangyo ameiomba Serikali kuendelea kuwekeza katika ujenzi wa mabweni ili kukidhi ongezeko la wanafunzi litakalotokana na kukamilika kwa mradi huo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TIA, Prof. Jehovaness Aikaeli, amesema bodi itaendelea kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa kuzingatia thamani ya fedha na kukamilika kwa wakati, huku akieleza kuwa mradi huo utachangia kuzalisha rasilimali watu yenye ujuzi kwa maendeleo ya Mkoa wa Singida na Taifa kwa ujumla.

Hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi wa jengo hilo ikiendelea.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TIA, Prof. Jehovaness Aikaeli.

......................................... 

Mhandisi Mkazi Mshauri wa Mradi huo, Henry Chundu, akizungumza kwenye hafla hiyo alisema jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi wapatao 3,500 kwa wakati mmoja na limejengwa kwa kuzingatia viwango vya kisasa, ikiwemo mifumo ya usalama dhidi ya moto, matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.Hafla hiyo ikiendelea.

Wageni waalikwa wakiwa kwenye hafla hiyo.

Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba, akielekeza jambo wakati wa ziara hiyo. Kushoto ni  Naibu Waziri wa Fedha, Mhandisi Mshamu Ali Munde na Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa. William Pallangyo.

Waziri Mkuu Dk.Mwigulu akiwa katika picha ya pamoja na Wanafunzi wa TIA Kampasi ya Singida ambao ni wanufaika wa Mradi huo.
Muonekano wa Jengo hilo.

.........................

Habari hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale Simu namba 0754362990
 

Post a Comment

0 Comments