KIHONGOSI NA DIRA YA TAIFA LENYE MSHIKAMANO

KIHONGOSI NA DIRA YA TAIFA LENYE MSHIKAMANO

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, akizungumza na Wananchi mkoani Iringa katika ziara yake ya kikazi.

..................................

Na Godwin Myovela

Katika safari mbalimbali za kikazi, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenan Kihongosi, ameendelea kuonyesha umuhimu wa viongozi kuwa karibu na wananchi, kusikiliza changamoto zao na kusimamia maono ya maendeleo yenye manufaa kwa taifa.

Ziara hizo zimebeba ujumbe mkubwa wa uwajibikaji, ambapo kiongozi anapotoka ofisini na kwenda kwenye jamii anapata nafasi ya kuona hali halisi, kusikia sauti za wananchi na kutafuta majibu ya changamoto zinazowakabili.

Tanzania yenye maendeleo endelevu inahitaji viongozi wanaosikiliza, wanaowajibika na wanaotanguliza maslahi mapana ya taifa mbele ya maslahi binafsi.

Moja ya mambo yanayojitokeza katika ziara hizo ni msisitizo wa kulinda amani, umoja na mshikamano kama msingi wa kila hatua ya maendeleo ya nchi.

Amani si neno tu, bali ni mazingira yanayowezesha wananchi kufanya kazi, vijana kutafuta fursa, wafanyabiashara kuwekeza na taifa kusonga mbele.

Ujumbe wa kuhamasisha vijana kutumia nguvu zao kujenga uchumi, kuongeza maarifa na kushiriki katika shughuli za maendeleo ni msingi muhimu wa kuandaa kizazi chenye uwezo wa kuiongoza Tanzania ya kesho.

Vijana wanapopewa nafasi na mwelekeo sahihi, wanakuwa nguvu kubwa ya mabadiliko chanya katika jamii na uchumi wa taifa.

Ziara hizi pia zinatoa funzo kwa viongozi wengine kwamba uongozi wa kisasa haujengwi kwa taarifa za mezani pekee, bali kwa kufika kwa wananchi na kuelewa mahitaji yao.

Kusikiliza kero na kuzitafutia majawabu ni sehemu ya kujenga imani kati ya wananchi na viongozi, jambo linaloimarisha ushirikiano wa kitaifa.

Tanzania imejengwa kwenye misingi ya undugu, upendo na kuheshimiana, hivyo kila Mtanzania ana nafasi ya kulinda tunu hizo kwa vitendo.

Pongezi kwako Kenan na CCM kwa jitihada za kuendelea kuwakumbusha wananchi umuhimu wa umoja, kwani taifa lenye mshikamano lina uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto na kutumia fursa zilizopo.

Hatma ya Tanzania tuitakayo inahitaji viongozi na wananchi wanaoshirikiana, wanaolinda amani na wanaojenga taifa kwa moyo wa uzalendo.

Kwa mtazamo mpana, ziara za viongozi kama hizi zinapaswa kuwa chachu ya uwajibikaji, matumaini na kujenga Tanzania yenye amani, maendeleo na undugu wa kweli kwa vizazi vijavyo.

Post a Comment

0 Comments