KIHONGOSI ASISITIZA AMANI, MAENDELEO NA UMOJA

KIHONGOSI ASISITIZA AMANI, MAENDELEO NA UMOJA

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi, Mafunzo na Uenezi, Kenan Kihongosi, akizungumza na Wananchi wa Mkoa wa Iringa katika ziara yake ya kikazi.

.................................

Na Godwin Myovela, Iringa

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Itikadi, Mafunzo na Uenezi, Kenan Kihongosi, amesisitiza umuhimu wa kulinda amani, umoja na mshikamano wa Watanzania kama msingi wa maendeleo ya taifa.

Akiwa katika ziara mkoani Iringa, Kihongosi amesema amefika kwa ajili ya kusikiliza wananchi, kukagua miradi ya maendeleo na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Amesema ziara hiyo si ya kutembea bali ni ya kazi, ikilenga kuimarisha uhusiano na wananchi pamoja na kuhakikisha kero zao zinapatiwa majawabu kwa wakati.

Kihongosi amewataka vijana kutumia nguvu zao kujenga uchumi wa familia, kutafuta fursa na kuwekeza kwenye shughuli zenye tija badala ya kushawishiwa na mambo yanayoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.

Amesema Tanzania imejengwa kwenye misingi ya uhuru, haki, umoja, upendo na mshikamano, hivyo wananchi wanapaswa kuepuka migawanyiko ya kikabila, kikanda au kisiasa.

Akizungumzia maendeleo, amesema utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo Bwawa la Julius Nyerere unaonyesha juhudi za kuongeza uwezo wa taifa kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Ameongeza kuwa sekta ya utalii ni eneo lenye fursa kubwa kwa vijana, kuanzia huduma za usafiri, malazi, biashara hadi ajira zinazotokana na wageni wanaoingia nchini.

Kihongosi amesema nguvu ya CCM ipo kwenye mfumo wake wa kuwafikia wananchi hadi ngazi za chini, kusikiliza changamoto zao na kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Amesisitiza kuwa amani ni mtaji wa kila maendeleo, hivyo kila Mtanzania ana wajibu wa kuilinda kwa ajili ya ustawi wa taifa na vizazi vijavyo.

Post a Comment

0 Comments