𝐑𝐀𝐉𝐀𝐁𝐔 𝐀𝐁𝐃𝐔𝐋𝐑𝐀𝐇𝐌𝐀𝐍 𝐀𝐎𝐍𝐄𝐒𝐇𝐀 𝐌𝐅𝐀𝐍𝐎 𝐌𝐀𝐄𝐍𝐃𝐄𝐋𝐄𝐎 𝐂𝐂𝐌 𝐓𝐀𝐍𝐆𝐀

𝐑𝐀𝐉𝐀𝐁𝐔 𝐀𝐁𝐃𝐔𝐋𝐑𝐀𝐇𝐌𝐀𝐍 𝐀𝐎𝐍𝐄𝐒𝐇𝐀 𝐌𝐅𝐀𝐍𝐎 𝐌𝐀𝐄𝐍𝐃𝐄𝐋𝐄𝐎 𝐂𝐂𝐌 𝐓𝐀𝐍𝐆𝐀

Mwenyekiti  wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Rajabu Abdallah Abdurahman alipokuwa akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa CCM mkoani humo.

.......................................

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Rajabu Abdallah Abdurahman, ameendelea kuonekana kuwa miongoni mwa viongozi wanaoshiriki moja kwa moja katika shughuli za maendeleo ya chama na jamii katika Mkoa wa Tanga.

Katika kipindi cha uongozi wake, amekuwa akihusishwa na shughuli mbalimbali za kijamii, kiuchumi, kidini na michezo zinazolenga kuimarisha ustawi wa wananchi pamoja na maendeleo ya chama. 

Hatua yake ya hivi karibuni ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni 500,  Mei 31, 2026 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa CCM Mkoa wa Tanga imeelezwa kuwa mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya kazi na makazi kwa watumishi wa chama hicho.

Wakati akikabidhi hundi hiyo, Abdurahman alisema tayari wataalamu wameanza kufanya tathmini katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba hizo ambazo zinatarajiwa kujengwa katika wilaya zote za mkoa huo.

Mkoa wa Tanga una wilaya za Handeni, Korogwe, Pangani, Muheza, Tanga Jiji, Mkinga, Kilindi, Lushoto na Bumbuli.

Kwa mujibu wa mpango huo, kila wilaya au halmashauri itajengewa nyumba nne kwa ajili ya Katibu wa Chama na viongozi wa jumuiya zake. 

Alisema fedha hizo tayari zimewekwa benki na taratibu za kuzipeleka kwenye wilaya hizo zinaendelea kuwezesha utekelezaji wa mradi huo kuanza kwa wakati.

Mkoa huo unahitaji nyumba 36 za watumishi wa chama ambapo kila wilaya tajwa itajengewa nyumba nne. Ujenzi huo unatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu. 

“Fedha hizi tayari ziko benki na zitaanza kutolewa wilayani muda si mrefu. Wataalamu wako maeneo ya mradi wakifanya tathmini. Wale wanaotamani kuzitafuna waangalie sana, kwani sitavumilia ubadhirifu,” alisema Abdurahman.

Alieleza kuwa mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi alizozitoa mwaka 2022 wakati akiwania nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa.

Utekelezaji wa ahadi kwa vitendo ni sehemu ya uongozi unaowajibika na unaolenga kuleta matokeo yanayoonekana kwa wanachama na watumishi wa chama.

Aidha, aliwakumbusha viongozi na wanachama wa CCM umuhimu wa kujenga ofisi zenye hadhi inayolingana na nafasi, historia na majukumu ya chama hicho tawala nchini.

Wadau mbalimbali wa maendeleo wanaeleza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya watumishi na ofisi za chama unaweza kusaidia kuongeza ufanisi wa utendaji kazi pamoja na kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa wanachama. Ustadhi Abdurahman alipokuwa akikabidhi basi jipya lenye thamani ya Shilingi Milioni 170 pamoja na fedha taslimu Shilingi Milioni 60 kwa timu ya African Sports (Wanakimanu Manu) kwa ajili ya kurahisisha usafiri.

.........................................

Mbali na mchango huo wa kifedha, Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Tanga amekuwa akishiriki shughuli za maendeleo zinazohusisha wananchi wa mkoa huo kama vile kusaidia miradi ya kijamii na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo.

Hatua ya kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa CCM Mkoa wa Tanga inaonesha namna viongozi binafsi wanavyoweza kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kuimarisha taasisi wanazoziongoza. 

Kadiri shughuli za maendeleo zinavyoendelea kutekelezwa, mradi huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kuboresha ustawi wa watumishi wa chama hicho. 

Mbali na mradi huo, Abdurahman amekuwa akihusishwa na shughuli mbalimbali za maendeleo ndani ya Mkoa wa Tanga zinazogusa sekta za michezo, uwezeshaji wa vijana, miradi ya kijamii na usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo. 

Katika sekta ya michezo, ameshiriki katika jitihada za kuimarisha vilabu vya mkoa huo ikiwemo msaada wa usafiri kwa timu ya African Sports pamoja na kufuatilia maboresho ya miundombinu ya michezo katika Uwanja wa CCM Mkwakwani. 

Kwa upande wa uwezeshaji wa vijana, taarifa zinaonesha kuwa ameshiriki kusaidia vikundi mbalimbali vya vijana, ikiwemo kulipia deni la mkopo wa kikundi cha bodaboda cha Pangani ili kuwawezesha kumiliki pikipiki zao kikamilifu. 

Pia amekuwa akitajwa katika juhudi za kusaidia miradi ya kijamii ikiwemo ujenzi wa zahanati, kusaidia taasisi za dini na kufuatilia utatuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tanga. 

Maoni ya wananchi kuhusu utendaji wake yanatofautiana katika baadhi ya maeneo, lakini wengi waliozungumza wanakubaliana kwamba amekuwa karibu na wananchi na amejitokeza kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Mkazi wa Pangani, Jamali Nasoro, anasema moja ya mambo yanayomtofautisha Abdurahman ni utayari wake wa kutumia muda na rasilimali zake kusaidia miradi ya kijamii inayowanufaisha wananchi. 

Naye Mohamed Shabani wa Kijiji cha Mikinguni anasema mchango wake katika ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho umeleta mabadiliko makubwa kwa wananchi waliokuwa wakisafiri umbali mrefu kupata huduma za afya. 

Jambo linalojitokeza wazi ni kwamba utekelezaji wa ahadi umekuwa moja ya vipimo muhimu vya uongozi katika jamii ya sasa. 

Wachambuzi wa masuala ya uongozi wanaeleza kuwa wananchi wengi hawapimi viongozi kwa maneno pekee, bali kwa uwezo wao wa kubadilisha ahadi kuwa matokeo yanayoonekana katika maisha ya watu. 

Kwa msingi huo, mjadala unaoibuka kutokana na hatua za Rajabu Abdallah Abdurahman si kuhusu siasa pekee, bali kuhusu dhana pana ya uwajibikaji wa viongozi na umuhimu wa kutekeleza ahadi wanazozitoa kwa wananchi na taasisi wanazoziongoza. 

Akizungumzia hali ya kisiasa mkoani Tanga, alisema ahadi yake ya kuimarisha nguvu ya CCM imeendelea kuzaa matunda, kwani hivi sasa upinzani umepungua kwa kiwango kikubwa katika mkoa huo na hiyo inatokana na utekelezaji wa mahitaji ya wananchi. 

“Niliahidi kuwa upinzani utatafutwa kwa tochi. Leo uko wapi? Tanga ni ngome ya CCM,” alisema. 

Muonekano wa Jengo la CCM Mkoa wa Tanga baada ya kukarabatiwa na Ustadhi Rajabu Abdurahman.

........................................

Kwa mujibu wa Abdurahman CCM Mkoa wa Tanga Inahitaji nyumba 36 za watumishi  ambapo kila wilaya zitajengewa nyumba nne kwa ajili ya Katibu wa Chama na viongozi wa jumuiya zake. 

Kabla ya makabidhiano ya hundi hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, alimpongeza  Abdurahman na viongozi wenzake kwa maboresho yaliyofanyika katika ofisi za CCM mkoani humo. 

Katika hafla hiyo, watumishi saba wa Serikali walitunukiwa vyeti vya kutambua mchango wao katika kuimarisha ushirikiano kati ya Chama Cha Mapinduzi CCM na Serikali na kufanikisha utekelezaji majukumu ya kimaendeleo. 

Abdurahman ni kiongozi ambaye amefanya mambo mengi ya maendeleo baadhi ya mambo hayo ni kama ifuatavyo: 

SEKTA YA MICHEZO 

1.   Kuinua na Kuimarisha Sekta ya Michezo Mwenyekiti Abdurahman ameweka kipaumbele kikubwa kwenye michezo akiamini kuwa ni chanzo kikuu cha ajira na kipato kwa vijana: 

2.    Ufadhili wa Timu za Mkoa: Kupitia uongozi wake, chama kimechangia kurejesha hadhi ya soka la Tanga. Mfano wa karibuni ni pale alipokabidhi basi jipya lenye thamani ya shilingi milioni 170 pamoja na fedha taslimu shilingi milioni 60 kwa timu ya African Sports (Wanakimanu Manu) kwa ajili ya kurahisisha usafiri. Ukarabati wa Miundombinu ya Michezo: 

3.   Aliongoza  Kamati ya Siasa ya Mkoa kukagua na kusimamia maboresho ya Uwanja wa CCM Mkwakwani. Mwezi Machi 2026, alichukua hatua kali ya kuelekeza kusimamishwa kazi mara moja kwa meneja wa uwanja huo kutokana na kusuasua kwa utunzaji wa miundombinu na usimaji wa viti vya mashabiki. 

4.   Kuhamasisha Mashabiki na Uzalendo: Amekuwa mstari wa mbele kuwasihi wakazi wa Tanga kujitokeza kwa wingi viwanjani ili kusaidia vilabu vya mkoa huo (kama vile Coastal Union na African Sports) kujipatia mapato na kukua kiushindani. 

5.   Shughuli za Maendeleo ya Jamii na Uchumi kiongozi huyu amekuwa daraja imara kati ya Chama, Serikali, na wananchi kwa kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM:Kusaidia Vijana Kiuchumi: Mwezi Novemba 2025, alitoa kiasi cha Shilingi milioni 13.4 kutoka mfukoni mwake ili kuwalipia salio la deni la mkopo wa asilimia 10 vijana 10 wa kikundi cha bodaboda cha "Hatupoi" cha Pangani baada ya kuvutiwa na nidhamu yao nzuri ya marejesho, na hivyo kuwamilikisha pikipiki zao kikamilifu.Kuboresha Mazingira ya Biashara: 

6.   Amekuwa akifanya ziara za kushtukiza kukagua kero za wananchi. Mwezi Aprili 2026, aliagiza Halmashauri ya Jiji la Tanga kuhakikisha Soko la Mgandini linasafishwa ndani ya siku saba na kuanza ujenzi wa vyoo vya wafanyabiashara, pamoja na kutatua msongamano wa magari sokoni hapo ili kulinda afya na uchumi wao.Kutatua Migogoro ya Kijamii: 

7.   Ameingilia kati na kusitisha ujenzi wa miradi ya kiserikali inayolalamikiwa kuingia kwenye maeneo ya taasisi nyingine (kama vile mgogoro wa ujenzi wa ofisi ya Kata ya Mzizima na Kanisa la KKKT) ili kulinda amani na maelewano. 

8.    Kuimarisha na Kukijenga Chama Ndani ya Mkoa Miundombinu ya Chama: 

9.   Amefanikisha kukarabati Jengo la CCM Mkoa na kuwa la kisasa pamoja na kununua samani. 

Ustadhi Abdurahman alipokuwa akisikiliza kero katika ziara yake ya kikazi mkoani humo.

...............................

Maoni ya Wananchi 

Baadhi ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoani hapa wametoa maoni tofauti kuhusu mchango wa  Abdurahman, katika shughuli za maendeleo ya kijamii, wakitaja hatua mbalimbali alizochukua kusaidia miradi inayogusa maisha ya wananchi. 

Wananchi waliozungumza walisema miradi ya afya, elimu na uwezeshaji wa kiuchumi imeendelea kuwa miongoni mwa maeneo ambayo jamii nyingi bado zinahitaji kupewa kipaumbele ili kuboresha maisha ya wananchi.

 Walisema ushirikiano kati ya viongozi, wadau wa maendeleo na serikali unaweza kusaidia kuharakisha utekelezaji wa miradi inayolenga kuboresha huduma za kijamii katika maeneo mbalimbali nchini.

Mkazi wa Korogwe Mjini, Ibrahim Ahmed alisema kazi anayoifanya ni nzuri na anapaswa kushuka chini kwa wananchi ambao wanamahitaji mengi kama vituo vya afya, zahanati na kuwainua kiuchumi wajasiriamali kwa kuwasaidia mikopo isiyo na riba. 

“Akiwa kama kiongozi wakati anayafanya hayo yote anatakiwa kuitoa wasiwasi jamii anayoizunguka  kwa kuieleza vyanzo vya mapato ya fedha anazo wasaidia,” alisema Ahmed.

Kwa upande wake Jamali Nasoro Mkazi wa Pangani alisema Abdurahman ni kiongozi wa mfano na mtu akitaka kuwa kiongozi mzuri ajifananishe naye, kwanza ana huruma, subra, mwepesi wa kusamehe anapotokea mtu amemkosea. 

“Hizi ni sifa za Mungu, lakini Mungu amewataka watu wajipange na sifa hizo ukiongeza nyingine utaingia pasipo husika, Abdurahman anasifa hizo kidogo alichonacho anataka ale na wenzake yupo tayari kupoteza muda wake kuhakikisha anaenda kuwatetea watu,” alisema Nasoro.

Nasoro alisema katika Kijiji cha Mikinguni Pangani  Abdurahman alinunua kiwanja na kuanza kujenga Zahanati na wakati wapo kwenye mkutano wa hadhara alimpigia simu Mzee Azim Dewj na kumuomba mchango wa kuchangia ujenzi huo ambapo alichangia Shilingi milioni 10 wakiwepo na watu wengine. 

Nasoro aliongeza kuwa fedha hizo zimejenga zahanati hiyo na Serikali ilimalizia ujenzi huo na sasa huduma za afya zinatolewa na wananchi hawaendi tena mbali kupata huduma. 

“Mimi na thubutu kusema anauwezo mkubwa na nafasi aliyonayo naiona ndogo angeweza kupewa nafasi ya kitaifa ili aweze kuwasaidia watanzania tunamuomba Mwenyezi Mungu amzidishie umri,” alisema Nasoro.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Rajab Abdulrahaman alipokuwa akizungumza na wananchi na kutoa kiasi cha Shilingi Milioni 13.4 kuwalipia madeni vijana waliokopeshwa na serikali mikopo ya asilimia 10. 

Vijana 10 wa Kikundi cha bodaboda cha Hatupoi walifanikiwa kupata mkopo wa Shilimgi milioni 27.5 ambazo walinunua pikipiki nane na kufanikiwa kurejesha Sh milioni 14.1katika kipindi cha miezi nane.

.............................................

Mkazi wa Mombo, Nurudin Abubakari ambaye alikuwa mwanachama wa upinzani ambaye alihamia CCM na kupokelewa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho na sasa ni Makamu wa Rais Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema katika harakati zake zote za kisiasa hajawahi kumuona kiongozi ambaye anafanyakazi kubwa za kijamii akiwa mwanasiasa kama Rajabu  Abdurahman. 

“Ukienda kwenye ilani anaisimamia vizuri sana anatembelea miradi na kuhoji pale anapoona haiendi sawa,” alisema Abubakar. 

Alisema CCM Mkoa wa Tanga inajivunia kwa kuwa na Ustadhi Abdurahman na hata wapinzani wanajua kushindana naye ni vigumu kwa sababu anaingia kila mahala kwa mtu mmoja mmoja, makundi, anakisaidia chama na kuwa anafanya mambo mazito. 

Akitoa mfano alisema Mei 29, 2026 alipokuwa kwenye dua eneo la Stahabu Pwani kuwaombea wazazi wake waliotangulia mbele za haki alikuwa na vijana aliowadhamini vyombo kuanzia shilingi 800,000, milioni 1 hadi milioni 10, vinanda viwili, spika na kuwakodishia Coster ambapo alisema ni vigumu kumpata mtu wa aina yake. 

Alisema viongozi wa dini mkoani humo asilimia kubwa wanapokuwa na shughuli zao wanaenda kumuona na kuwa amewahi kushuhudia taasisi moja ya dini ilipofanya  Maulid aliwapa kilo za mchele zaidi ya kilo 1000 na madumu ya mafuta zaidi ya manne. 

“Rajabu Abdurahman kwa Mkoa wa Tanga amegusa kila sehemu, amegusa kwenye michezo alikabidhi Klabu ya Afrcan Sports gari la zaidi yaa milioni 170 na kukabidhi fedha taslimu shilingi milioni 30 utampata wapi mtu kama huyo ambaye siyo mbunge lakini anajitolea tu,” aliuliza Abubakar.

Alisema kwa vijana waliojiunga katika vikundi amewekeza nguvu kubwa kwa kuwapa pikipiki na misaada mbalimbali wakati siyo mbunge ni mwenyekiti tu wa CCM. 

Abubakar alisema ikiwa hiyo haitoshi  Abdurahman amefika katika vijiji vingine ambavyo havijawahi kufikiwa na kiongozi yeyote mkoani humo na kusikiliza kero zao.

Alisema wakizungumza mambo aliyofanya Abdurahman ni mengi na wala hawezi kuyamaliza kwani kulikuwa na taasisi za dini ambazo zilikuwa haziwezi kukaa pamoja na kuzungumza lakini kupitia yeye zinakaa pamoja na kushiriki shughuli mbalimbali. 

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Ustadhi Rajab Abdulrahman (MCC) akipokea Tuzo maalumu kutoka kwa Viongozi wa CCM Wilaya ya Muheza alipokuwa kwenye ziara ya kikazi mwaka 2024.

.......................................

Katibu Mstaafu wa CCM Wilaya ya Nkinga, Stamili Dendego amesema Mwenyekiti wa CCM mkoani humo anasimamia vizuri chama na wakati yupo kazini watu walikuwa wakitamani kwenda kufanya kazi mkoani Tanga. 

“Mwenyekiti alikuwa akitoa misaada mbalimbali ndani na  nje ya chama kwani alipokuwa akitembelea miradi iwe ya ujenzi wa zahanati, shule na mingineyo alikuwa hasubiri fedha zitoke serikalini alikuwa akichangia kutoka mfukoni mwake miradi hiyo ikamilike na ianze kutoa huduma,” alisema Dendego. 

Mkazi wa Kijiji cha Mikinguni wilayani Pangani, Mohamed Shabani anamshukuru Ustadhi Abdurahman kwani tangu wazaliwe katika kijiji hicho hadi anafikisha miaka 47 hawakuwa na zahanati na familia yao ndiyo iliuza kiwanja na kujengwa zahanati hiyo na mwenyekiti huyo wa chama na kumaliziwa ujenzi wake na Serikali. 

“Tunamshukuru Mwenyekiti wa chama ndugu Rajabu, Mwenyezi Mungu aendelee kumuongoza aendelee hivyo hivyo siyo kwetu tu bali na kwa watu wengine kwani misaada anayotoa ni mingi haina mfano,” alisema Shabani. 

Alisema ni sehemu gani utapita mkoani Tanga ambayo hazungumzwi Ustadhi Abdurahman kwa mazuri anayofanya  ndiyo kiongozi bora ambaye wanamuhitaji kwani anasaidia makundi mbalimbali na jinsia zote. 

“Chama kimepata mtu sahihi na mpambanaji, anaye kisaidia na kukitangaza na kuwashawishi watu kukipenda na hata baadhi ya watu kutoka vyama vingine wamevihama vyama vyao na kujiunga na CCM,” alisema Shabani. 

Naye Fatuma Kautuka mkazi wa Muheza Mjini anasema Ustadhi Abdurahman ni kiongozi ambaye anasaidia makundi mbalimbali ya kijamii mkoani Tanga bila ya ubaguzi hususani katika Wilaya ya Muheza. 

Alisema licha ya kuwa katika nafasi hiyo hajawahi kujikweza wala kumdharau mtu ni kiongozi anayeshirikiana na wananchi vizuri katika huzuni na furaha labda hasiwepo mkoani humo.

“Ustadhi Abdurahman ni kiongozi ambaye ikiwepo miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya Mkoa wa Tanga anaisimamia ipasavyo hataki konakona ili ikamilike ipasavyo na kwa gharama halisi,” alisema Kautuka.

 Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Ustadhi Rajabu akishiri kuchimba msingi kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kibaya Kata ya Misima wilayani Handeni.

.............................................

Mkufunzi wa Taifa wa CCM Mkoa wa Tanga kutoka Kambi ya Kikwete na Katibu wa Kata ya Ngamiani Kati, Fatihiya Nyausi anasema kugombea nafasi yoyote ya uongozi ndani ya chama ni demokrasia lakini wakati wa uchaguzi ukiwadia atamshangaa mtu atakayejitokeza kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya uenyekiti kwani kazi kubwa aliyoifanya Ustadhi Abdurahman anatosha kuendelea kuvaa kiatu hicho. 

“Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Ustadhi Abdurahman hajaingia kwenye chama kama kaja tu alitokea kwenye jumuiya ya vijana na alikwishapikwa na chama alipotoka hapo alikuwa mwenyekiti wa chama Wilaya ya Pangani kutokana na kuwa na rekodi yake nzuri aliomba nafasi ya uenyekiti wa mkoa ambapo alipata kura nyingi za kishindo,” alisema Nyalusi. 

Alisema jambo ambalo analifurahia ni la kuwaunganisha wana CCM na kuwa kitu kimoja, kuimarisha chama kwani hivi sasa Wilaya ya Tanga na mkoa kwa ujumla hauna tena upinzani kutokana na utendaji wake kwani kuna wanachama zaidi ya 500 kutoka vyama vingine walihamia CCM. 

Alisema bila ya kumung’unya maneno kwa Mkoa wa Tanga Ustadhi Abdurahman amefanya kazi kubwa kwa asilimia 100 na ni mwenyekiti aliyeonesha mfano kati ya wenyeviti waliyowahi kuhudumu nafasi hiyo mkoani humo. 

“Ustadhi Rajabu amevunja rekodi kwa kukithamini chama, kukarabati ofisi ya CCM Mkoa ambayo haikuwahi kukarabatiwa tangu enzi za kina Bibi Titi Mwinyi ambalo limekuwa la kisasa,” alisema. 

Nyausi aliongeza kuwa Ustadhi Abdurahman amewawezesha vijana kwa kuwakopesha pikipiki, amefungua mashina ya jumuiya zote za chama na kuwa mlezi wa jumuiya hizo. 

Alisema jambo kubwa alilolifanya ni kutafuta fedha kwa wafadhili ili kujenga nyumba za watumishi wa jumuiya hizo ambao walifikia hatua ya kukosa hela ya kulipia pango kwenye nyumba walizopanga lakini sasa hivi wanakwenda kuheshimiwa baada ya kukamilika kwa nyumba hizo. 

“Kwa kifupi Ustadhi Abdurahman ni mwenyekiti ambaye amefanya mengi na kutengeneza historia Mkoa wa Tanga kutokana na uongozi wake usiyo na mfano,” alisema Nyalusi.

Mkazi wa Kabuku Ndani wilayani Handeni, Salim Issa anasema mambo aliyofanya Ustadhi Abdurahman katika mkoa huo ni mengi na hayawezi kuisha kwa muda mfupi akianza kuyazungumzia kwani ameisaidia sana Serikali na kukitangaza chama.

“Moja ya jambo kubwa alilofanya hapa kwetu Kabuku ni kuwatengenezea wazee maskani yao ambayo wamekuwa wakikutana na kupanga mipango yao mbalimbali ambapo aliwawezesha Shilingi 500,000,” alisema Issa.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga akiteta jambo na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa ambaye kwa sasa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Emmanuel Nchimbi alipokuwa kwenye ziara ya kikazi Korogwe Juni 7,2024.Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Ustadhi Rajab Abdulrahman (MCC) akipanda kwenye gari kwa ajili ya kupokea vifaa vya ujenzi wa ofisi ya CCM wilayani Muheza.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Mhe. Rajabu Abdalla akipata maelezo alipotembelea chumba cha Maabara ya Sayansi  katika Shule ya Sekonadari New Bagamoyo iliyopo kata ya Bagamoyo wakati wa ziara yake ya kikazi ambapo pia alikagua Mradi wa Ujenzi wa Bweni la Wanafunzi  katika Shule ya Sekondari Ngombezi iliyoko Kata ya Mgombeziiliyopo Halmashauri ya Mji wa Korogwe  Mei 16, 2025.

Katika ziara hiyo Ustadhi Rajabu alichangia magunia kumi  ya mchele yenye thamani ya Shilingi Milioni 2.5 kwa ajili ya chakula cha Wanafunzi wanaokaa Bweni katika Shule ya Sekondari ya Ngombezi.

................................

Makala haya yameandaliwa na Dotto Mwaibale Msimamizi Mkuu wa Uenezi CCM Blog Simu namba 0754362990

Post a Comment

0 Comments