Katika mpira wa miguu, kuna kitu kimoja ambacho ni muhimu kuliko hata vikombe, fedha au umaarufu wa klabu.
Kitu hicho ni haki.
Mashabiki wanaweza kukubali kufungwa. Wanaweza kuvumilia matokeo mabaya. Wanaweza hata kukubali makosa ya waamuzi ndani ya dakika tisini.
Lakini kuna jambo ambalo mashabiki hulipokea kwa uchungu mkubwa kuliko yote: kuamini kwamba mfumo wenyewe umechagua upande.
Na kwa sasa, hilo ndilo jambo linalozidi kutikisa soka la Tanzania.
Baada ya Klabu ya Young Africans Sports Club kutozwa faini ya shilingi milioni 30 kufuatia kutotumia chumba rasmi cha kubadilishia nguo katika dabi dhidi ya Simba, mjadala haukuishia kwenye kanuni za mchezo. Badala yake, umefungua ukurasa mkubwa wa malalamiko, hisia na maswali kuhusu usawa wa maamuzi ndani ya soka la Tanzania.
Kwa sababu kwa upande wa Wananchi, hili si tukio la kwanza. Wanaamini ni mwendelezo wa kile wanachokiita “mfumo wa upendeleo” ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiuona ukiiumiza timu yao.
Na hapa ndipo mambo yanapokuwa mazito zaidi.
Kwa sababu historia ya soka duniani inaonyesha jambo moja la wazi: Mashabiki wakianza kupoteza imani na mfumo, madhara yake huwa makubwa kuliko matokeo ya uwanjani.
Mfano maarufu ulitokea nchini Italia mwaka 2006 kupitia sakata kubwa la Calciopoli, ambapo klabu kadhaa — hasa Juventus — zilihusishwa na tuhuma za ushawishi wa waamuzi na mfumo wa upendeleo ndani ya ligi. Kilichofuata hakikuwa tu adhabu za kawaida. Soka la Italia lilipitia kipindi kigumu cha kuporomoka kwa imani ya mashabiki, taswira ya ligi kuharibika na watu wengi kuanza kuamini kuwa ushindani haukuwa wa haki tena.
Nchini Ugiriki pia, kulikuwa na miaka ambayo mashabiki waliandamana wakilalamikia kile walichokiita “soka la watu wachache,” wakidai baadhi ya timu zilikuwa na ushawishi mkubwa kuliko nyingine. Matokeo yake yakawa vurugu, migogoro na kuongezeka kwa chuki miongoni mwa mashabiki.
Hata Afrika Kusini, miaka iliyopita kulikuwa na mijadala mikubwa kuhusu baadhi ya timu kuonekana kupata “ulinzi wa mfumo,” jambo lililosababisha mamlaka za soka kuongeza uwazi kwenye maamuzi ya kinidhamu ili kurejesha imani ya mashabiki.
Na hapa ndipo Tanzania inapaswa kujifunza mapema.
Kwa sababu kinachoumiza mashabiki wengi wa Yanga si tu faini yenyewe. Kinachowaumiza ni kile wanachoamini kuwa ni tofauti ya namna sheria zinavyotumika.
Ndiyo maana kila tukio linalofanana lakini likaonekana kupewa uzito tofauti huongeza hasira zaidi.
Na katika sakata hili la vyumba vya kubadilishia nguo, kuna ukweli ambao wengi wanaogopa kuusema wazi.
Tatizo hili si la Yanga pekee.
Kwa miaka ya karibuni, timu mbalimbali — ikiwemo Simba — zimewahi kulaumiwa au kuhusishwa na kutoridhishwa na mazingira ya baadhi ya vyumba vya kubadilishia nguo wanapokuwa ugenini. Hofu kubwa ambayo imekuwa ikizungumzwa mara nyingi ndani ya soka la Afrika ni suala la usalama wa wachezaji, ikiwemo madai ya mazingira yasiyo salama au hata hofu za hujuma za aina mbalimbali.
Hata kama baadhi ya hofu hizi huwa hazina ushahidi wa moja kwa moja, ukweli ni kwamba zipo ndani ya akili za timu nyingi.
Na hapo ndipo swali muhimu linapaswa kuulizwa:
Je, suluhisho ni kuongeza faini pekee… au kutafuta mfumo bora wa kuondoa hofu hizi kabisa?
Kwa sababu ukweli mwingine ambao wengi hawausemi ni huu: Hakuna kanuni ya asili ya mpira inayosema timu lazima ijisikie salama kwa kulazimishwa kubadilishia nguo sehemu ambayo haina imani nayo.
Ndiyo maana badala ya kila tukio kugeuzwa vita ya adhabu, mamlaka za soka zinapaswa kuanza kufikiria suluhisho la kudumu.
Labda ni wakati wa kuwa na ukaguzi huru wa vyumba vya kubadilishia nguo kabla ya mechi kubwa. Labda ni wakati wa kuweka kamera za usalama kwenye maeneo hayo. Labda ni wakati wa timu zote mbili kuruhusiwa kukagua mazingira kabla ya mchezo. Au hata kuwa na maeneo ya kisasa yenye viwango sawa kwa kila timu bila tofauti yoyote.
“Kutoka kwa mastaa hadi mashabiki wa kawaida, Wananchi waliigeuza faini kuwa alama ya mshikamano"
......................................
Kwa sababu adhabu inaweza kumaliza tukio. Lakini haitamaliza hofu.
Na hofu ikiendelea kuwepo, migogoro itaendelea kujirudia.
Lakini pamoja na yote hayo, jambo moja ambalo limeifanya Tanzania isimame na kushangaa ni namna mashabiki wa Yanga walivyoamua kujibu sakata hili.
Kwa hasira zote walizokuwa nazo, hawakujibu kwa vurugu. Hawakujibu kwa fujo.
Walijibu kwa umoja.
Ndani ya masaa machache, mamilioni ya fedha yalichangwa kwa hiari kabisa ili kuisaidia klabu yao kulipa faini hiyo.
Hilo pekee ni somo kubwa kwa soka la Tanzania.
Kwamba nyuma ya Yanga kuna watu ambao hawaioni timu hiyo kama burudani tu. Wanaiona kama sehemu ya maisha yao.
Na hiyo ndiyo sababu kila wanapohisi timu yao imeonewa, huungana kwa nguvu ambayo si rahisi kuivunja.
Lakini pamoja na mapenzi hayo yote ya mashabiki, mamlaka za soka zinapaswa kuelewa jambo moja muhimu sana:
Haki isiponekana, hata sheria nzuri huanza kuchukiwa.
Na mashabiki wakifika hatua ya kuamini kuwa mfumo hauwasikilizi tena, mpira huanza kupoteza maana yake halisi.
Kwa sababu mwisho wa siku, soka haliishi kwa kanuni pekee.
Soka linaishi kwa imani ya watu. 
“Ndani ya masaa machache, mamilioni yalikuwa tayari yamekusanywa — ishara ya mapenzi makubwa ya Wananchi kwa klabu yao.”
......................................
Imeandikwa na: Victor Bariety Simu: 0757856284 maujikovb@gmail.com










0 Comments