Rais Dkt. Mwinyi ametangaza ongezeko hilo la mshahara leo, tarehe 01 Mei 2026, katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho ya Kilimo Kizimbani, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Dkt. Mwinyi amesema kiwango hicho kipya cha mshahara kitaanza kutolewa kuanzia mwezi Januari 2027 na kufahamisha kuwa hatua hiyo imezingatia hali ya uchumi wa nchi, gharama za maisha, na kuwapatia motisha wafanyakazi ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi.
Aidha, ameeleza kuwa uamuzi huo unaenda sambamba na dhamira ya Serikali ya kuimarisha mazingira ya kazi na kuhakikisha kuwa watumishi wanapata stahiki zao kwa wakati, pamoja na kutoa wito kwa watumishi wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii, juhudi, nidhamu na uzalendo ili kuleta maendeleo endelevu Zanzibar.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na wafanyakazi wa sekta ya umma na sekta binafsi, na itaendelea kushirikiana na vyama vya wafanyakazi kukabiliana na changamoto zote zinazowakabili wafanyakazi hapa nchini.
Amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Nane imepata mafanikio makubwa tangu ilipoingia madarakani mwaka 2020, kwa kufanikiwa kuimarisha maslahi ya wafanyakazi kupitia kurekebisha na kuongeza mishahara, kufanya mapitio ya posho na marupurupu ya watumishi, pamoja na kuimarisha mafao ya hifadhi ya jamii na kuanzisha mfuko wa bima ya afya kwa wafanyakazi wote pamoja na familia zao.
Amepongeza dhana ya utatu inayoendelezwa baina ya Wizara ya Kazi na Uwekezaji, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (ZATUC), na Chama cha Waajiri Zanzibar (ZANEMA) kwa kuzipatia ufumbuzi changamoto za wafanyakazi na waajiri kwa ujumla, ambapo changamoto 24 kati ya 29 tayari zimepatiwa ufumbuzi.
Rais Dkt. Mwinyi ametangaza kuwa Serikali imetenga nafasi za ajira 7,500 katika mwaka wa fedha 2026–2027, pamoja na kuendelea kuimarisha maslahi ya wafanyakazi.
Akihitimisha hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa vyama vya wafanyakazi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi changamoto za wafanyakazi, na kuwataka wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii, uzalendo, na kutanguliza maslahi ya umma.













0 Comments