𝗠𝗪𝗘𝗡𝗬𝗘𝗞𝗜𝗧𝗜 𝗦𝗛𝗜𝗩𝗬𝗔𝗪𝗔𝗧𝗔 𝗗𝗔𝗥 𝗔𝗔𝗟𝗜𝗞𝗪𝗔 𝗗𝗢𝗗𝗢𝗠𝗔 𝗞𝗨𝗦𝗜𝗞𝗜𝗟𝗜𝗭𝗔 𝗕𝗔𝗝𝗘𝗧𝗜

𝗠𝗪𝗘𝗡𝗬𝗘𝗞𝗜𝗧𝗜 𝗦𝗛𝗜𝗩𝗬𝗔𝗪𝗔𝗧𝗔 𝗗𝗔𝗥 𝗔𝗔𝗟𝗜𝗞𝗪𝗔 𝗗𝗢𝗗𝗢𝗠𝗔 𝗞𝗨𝗦𝗜𝗞𝗜𝗟𝗜𝗭𝗔 𝗕𝗔𝗝𝗘𝗧𝗜

Ni bwana harusi mtarajiwa, aomba sapoti ya harusi

Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Dar es Salaam (SHIVYAWATA), Charles Matemba  (Bwana harusi mtarajiwa), akiwa na Mbunge wa Viti Maalumu wa Kundi la Wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa katika mkutano wa shughuli za kichama.
....................................

MWENYEKITI wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Dar es Salaam (SHIVYAWATA), Charles Matemba ni miongoni mwa wananchi 25 walioalikwa jijini Dodoma kusikiliza hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ya mwaka 2025/2026.

Matemba ambaye pia ni bwana harusi mtarajiwa, amepata mwaliko huo kupitia Taasisi ya Lete Mabadiliko Chanya Ulipo (LeMaChU), inayoshirikiana na wizara hiyo katika kuwahusisha wananchi na makundi maalum katika masuala ya maendeleo ya taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu wa Taasisi hiyo, Vaileth Mwazembe, alisema maandalizi ya safari ya washiriki hao tayari yamekamilika na wanatarajiwa kuwepo Dodoma Jumatatu asubuhi kwa ajili ya kufuatilia hotuba hiyo muhimu bungeni.

Alisema msafara huo utaongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Taasisi hiyo, Dkt.Tomic Simbeye.

“Mchakato wa kuwapata washiriki ulikamilika mapema na tayari 
wamepewa taarifa zote muhimu za safari yao kwenda Dodoma,” alisema Mwazembe.

Mbali na mwaliko huo wa kitaifa, Matemba pia yupo katika maandalizi ya tukio kubwa zaidi maishani mwake — kufunga ndoa na mchumba wake, Fatuma Ally Makame, Juni 27, 2026 katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Kinachovutia wengi ni kwamba wanandoa hao watarajiwa wote ni watu wenye ulemavu, lakini wameamua kuonyesha kuwa ulemavu si kikwazo cha upendo, ndoto wala maisha ya familia.  

Akizungumza kwa hisia, Matemba alisema anaamini ndoa yao itakuwa mfano wa matumaini kwa watu wengine wenye ulemavu wanaodhani hawawezi kufikia ndoto zao za maisha.

“Tunataka jamii itambue kuwa sisi pia tuna haki ya kupenda, kuoa, 
kuolewa na kujenga familia kama watu wengine,” alisema Matemba.

Kutokana na maandalizi ya harusi hiyo, bwana harusi huyo amewaomba ndugu, jamaa, marafiki na wadau mbalimbali kuwachangia ili kufanikisha siku yao muhimu.

Kwa upande wake, Fatuma alisema ameamua kuwa na Matemba kwa sababu ameona ndani yake upendo wa kweli, utu na maono ya maisha.

“Niliona ni mtu mwenye moyo mzuri na anayeniheshimu,  Ulemavu 

hauondoi ubinadamu wa mtu,”  alisema Fatuma.

Kwa yeyote atakayeguswa kuwasaidia wanandoa hao watarajiwa, michango inaweza kutumwa kupitia: Tigo Pesa: 0676701819 au M- Pesa: 0766101802 kwa jina la Charles Matemba.

Bibi harusi Mtarajiwa, Fatuma Ally Makame. aakiwa amepozi.

Bi. Fatuma akiwa nyumbani kwake.
Bwana harusi mtarajiwa akiwa katika ubora wake.

........................................

Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990

Post a Comment

0 Comments