Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Tanga, Rajabu Abdallah, akizungumza katika 'Hauli' ya kuwaombea dua wazazi wake iliyofanyika Kitongoji cha Stahabu Pwani, Wilaya ya Pangani, mkoani Tanga Mei 29, 2026.
.....................................
Na Mashaka Kibaya, Tanga
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdallah amesema taasisi za dini zina mchango mkubwa katika kujenga jamii yenye maadili mema, jambo ambalo limeendelea kuwa msingi muhimu katika kudumisha amani na maendeleo nchini.
Rajabu, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM (MCC), aliyasema hayo jana katika 'Hauli' ya kuwaombea dua wazazi wake shughuli ambayo ilifanyika huko Kitongoji cha Stahabu Pwani, Wilaya ya Pangani, mkoani Tanga.
Alisema kwamba, viongozi wengi hupitia katika misingi ya dini, hali ambayo inawasaidia kuwa na maadili mema na hivyo kumudu kuiongoza jamii kwa uadilifu.
Aidha, alisema ushirikiano kati ya wazazi, walezi na viongozi wa dini unasaidia kujenga taifa lenye wananchi wenye nidhamu, heshima na maadili yanayokubalika kijamii.
“Wazazi, walezi na viongozi wa dini wakishirikiana, ni dhahiri tutakuwa na jamii yenye maadili mazuri,” alisema Mwenyekiti huyo wa CCM.
Alieleza kuwa mgeni rasmi katika Hauli hiyo alitarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Hamad Masauni, ambaye alipata udhuru kutokana na majukumu ya kitaifa.
Ustaadh Rajabu aliongeza kusema kuwa watanzania wanapaswa aliwataka kuendelea kuilinda na kuienzi amani ya nchi iliyopo kwa maelezo kuwa pasipo amani hawataweza kufanya shughuli zozote za maendeleo kwa ufanisi.
Rajabu aliwataka wananchi kujifunza kutokana na matukio yaliyotokea kipindi cha Oktoba 29, huku akisisitiza umuhimu wa kutatua tofauti kwa njia ya hoja badala ya kejeli, dharau na matusi.
“Tuachane na vitu vinavyotugawa. Tutofautiane kwa hoja bila kejeli, dharau na matusi,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan akieleza kuwa ni kiongozi mkweli, mwenye huruma, mnyenyekevu na anayependa kuona wananchi wanaishi katika misingi ya amani.
“Tunaye Rais anayependa kuona watu wanaishi kwa amani ndani ya mioyo yao; mpenda amani, mnyenyekevu, mkweli na mwenye kujishusha. Tumuunge mkono,” alisema Mwenyekiti Rajabu.
Katika mazungumzo yake, Rajabu alisema pamoja na Waziri Masauni kutohudhuria 'Hauli' hiyo kutokana na majukumu ya kitaifa, ameahidi kuchangia shilingi milioni 10 za ujenzi wa msikiti na madrasa ya kisasa eneo la Stahabu Pwani.
Alisema kwamba, jamii ya Stahabu Pwani imelazimika kuanza ujenzi wa msikiti mpya na madrasa kutokana na ongezeko la waumini pamoja na wakazi wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa Rajabu, mradi huo unalenga kuhakikisha wananchi wanapata mazingira bora ya ibada na malezi ya dini kwa watoto na vijana, huku mahikamano na amani vikiendelea kuimarika katika jamii.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Batilda Salha Burian, akiwasilisha Salamu za Serikali, alipongeza juhudi za utendaji kazi zinazooneshwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, akisema amefanya mambo mengi yenye kuacha tabasamu kwa wananchi katika kipindi chake cha uongozi.
Vilevile, Mkuu huyo wa Mkoa wa Tanga alimpongeza Mwenyekiti Rajabu kwa namna anavyosimamia utekelezaji wa maelekezo ya Rais, jambo ambalo limeendelea kurahisisha shughuli za utendaji kazi katika Mkoa wa Tanga
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa akizungumza kwenye Dua ya kuwambuka wazazi wa Mwenyekiti mwenzake wa Tanga.
Shughuli ya dua ikiendelea.
Shughuli ikiendelea.













0 Comments