Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Tanga Rajabu Abdurahman Abdallah (kushoto), akikabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi 500 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Watumishi wa CCM mkoaani humo Mei 31, 2026.
.........................................
Na Mashaka Kibaya, Tanga
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdurahman Abdallah, amekabidhi hundi ya Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa nyumba za watumishi wa Chama hicho mkoani Tanga.
Hundi hiyo imekabidhiwa wakati wataalamu wakiendelea kufanya tathmini katika maeneo ya ujenzi kwa lengo la kuandaa utekelezaji wa mradi wa nyumba za watumishi wa CCM katika wilaya za mkoa huo
“Fedha hizi tayari ziko benki na zitaanza kutolewa wilayani muda si mrefu. Wataalamu wako maeneo ya mradi wakifanya tathmini. Wale wanaotamani kuzitafuna fedha hizi waangalie sana, kwani sitavumilia ubadhirifu,” alisema Ustaadh Rajabu akihimiza hali ya uwajibikaji.
Ujenzi wa nyumba za watumishi wa CCM ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi alizozitoa Rajabu wakati akiwania nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga. Mradi huo unalenga kuongeza hadhi ya chama na kuboresha mazingira ya makazi kwa watumishi wake.
Sambamba na mradi huo, Rajabu aliwakumbusha viongozi na wanachama wa CCM umuhimu wa kujenga ofisi zenye hadhi inayolingana na nafasi na majukumu ya chama hicho tawala.
Alisema kwamba, uwepo wa ofisi zenye ubora unasaidia kuongeza hamasa kwa viongozi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na huwajengea wananchi imani zaidi kwa chama katika kuwahudumia.
Akizungumzia hali ya kisiasa mkoani Tanga, Ustaadh Rajabu alisema ahadi yake ya kuimarisha nguvu ya CCM imeendelea kuzaa matunda, kwa maelezo kuwa hivi sasa upinzani umepungua kwa kiwango kikubwa katika mkoa huo.
“Niliahidi kuwa upinzani utatafutwa kwa tochi. Leo uko wapi? Tanga ni ngome ya CCM, na kama kuna watakaojaribu kujitokeza, tunazo mbinu za kuhakikisha chama kinaendelea kuwa imara,” alisema.
Kwa mujibu wa Rajabu, Mkoa wa Tanga unahitaji nyumba 36 za watumishi wa CCM, ambapo kila wilaya zitajengewa nyumba nne kwa ajili ya Katibu wa Chama na viongozi wa jumuiya zake. Mkoa huo una wilaya tisa za chama.
“Katika Mkoa wa Tanga tutajenga nyumba 36. Kila wilaya itakuwa na nyumba nne kwa ajili ya Katibu wa Chama na viongozi wa jumuiya zake. Tunatarajia ifikapo hapo mwezi Desemba mwaka huu ujenzi uwe umekamilika,” alisema.
Aliwataka wanachama wa CCM Mkoani Tanga kuendelea kuchangia maendeleo ya chama kwa nafasi zao ili kukiwezesha kuendelea kuwahudumia wananchi kwa ufanisi na kuongeza tija zaidi.
Kabla ya makabidhiano ya hundi hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, aliwasalimu washiriki wa hafla hiyo na kumpongeza Ustaadh Rajabu pamoja na viongozi wenzake kwa maboresho yaliyofanyika katika ofisi za CCM mkoani Tanga.
Alisema Ustaadh Rajabu na timu yake wamefanya kazi kubwa inayostahili kuigwa na mikoa mingine, huku akiwataka wanachama wa CCM na wananchi wa Tanga kuendelea kutoa ushirikiano kwa uongozi wa chama.
Katika hafla hiyo, watumishi saba wa Serikali walitunukiwa vyeti vya kutambua mchango wao katika kuimarisha ushirikiano kati ya Chama Cha Mapinduzi CCM na Serikali na kufanikisha utekelezaji majukumu ya kimaendeleo.









0 Comments