“Katikati ya mvutano wa Iran, Marekani na washirika wake, Hormuz imegeuka kitovu cha vita vya uchumi wa dunia.”
....................................
Kuna maeneo duniani ambayo ukubwa wake wa kijiografia hauendani kabisa na ukubwa wa athari zake duniani.
Mlango wa Hormuz ni mmoja wa maeneo hayo.
Kwa macho ya kawaida unaweza kuuona kama njia nyembamba ya maji inayopita kati ya Iran na Oman. Lakini kwa macho ya wachambuzi wa siasa za kimataifa, uchumi na usalama wa dunia, Hormuz ni “mshipa mkuu wa nishati duniani.”
Ndiyo maana kila neno linalotamkwa Tehran kuhusu kuufunga Mlango wa Hormuz huifanya dunia isimame kwa sekunde kadhaa.
Na sasa dunia imerudi tena kwenye hofu hiyo.
Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya bahari, International Maritime Organization (IMO), limethibitisha kuwa zaidi ya mabaharia 20,000 pamoja na takribani meli 1,500 wamekwama katika Ghuba ya Uajemi kufuatia mvutano ulioongezeka kati ya Iran, Israel na Marekani.
Hii si taarifa ya kawaida.
Hii ni alama ya hatari kwa uchumi wa dunia.
Kwa sababu historia inaonyesha wazi:
Hormuz ikitetemeka — bei ya mafuta duniani hupanda.
Hormuz ikifungwa — masoko ya dunia hupanic.
Na Hormuz ikiingia vitani — uchumi wa mataifa mengi hupata mshtuko.
KWA NINI HORMUZ NI MUHIMU KULIKO UNAVYODHANI?
Takwimu za taasisi za kimataifa za nishati zinaonyesha kuwa karibu asilimia 20 ya mafuta yote yanayotumiwa duniani hupita katika Mlango wa Hormuz.
Hapa ndipo mafuta kutoka Saudi Arabia, Iraq, Kuwait, Qatar, UAE na sehemu ya Iran husafirishwa kwenda Asia, Ulaya na sehemu nyingine za dunia.
Kwa lugha rahisi:
Ukisimamisha Hormuz, hujasimamisha Iran pekee — umegusa moyo wa uchumi wa dunia.
Ndio maana kila mgogoro unaohusisha eneo hilo huifanya Marekani, Ulaya, Urusi, China na NATO kuanza kufanya mahesabu mapya ya kiusalama na kiuchumi.
Katika mazingira ya sasa, Iran inaonekana kutumia Hormuz kama “silaha ya kimkakati.”
Si lazima ipige kombora kila siku.
Wakati mwingine tishio la kuzuia meli pekee linatosha kuutikisa mfumo mzima wa biashara duniani.
MELI ZA KIVITA ZINAANZA KUSOGEA — NA DUNIA INAANZA KUHOFU
Taarifa za hivi karibuni zimeonyesha kuwa France imetuma meli yake ya kubeba ndege za kivita kupitia Suez Canal kuelekea ukanda wa Hormuz.
Hii si hatua ndogo.
Mataifa makubwa hayatumi meli za kivita gharama kubwa kwa ajili ya maonyesho ya kawaida ya nguvu.
Yanazituma pale ambapo kuna hofu ya kuvurugika kwa mfumo wa kimataifa wa usafirishaji au uwezekano wa vita kupanuka.
Na hapa ndipo dunia inaanza kuelewa kwamba kinachoendelea si tena mzozo wa Iran dhidi ya Israel pekee.
Huu ni mchezo mkubwa wa nguvu za kimataifa.
Marekani tayari iliwahi kutangaza mpango wa kusindikiza meli katika eneo hilo kabla ya kuahirisha hatua hiyo kwa muda. Lakini ujumbe wake ulikuwa wazi:
Washington haiwezi kuruhusu Hormuz kufungwa kwa muda mrefu bila kujibu.
Kwa sababu kufanya hivyo kungeathiri washirika wake wa Ulaya, Asia na hasa soko la mafuta duniani.
KAMA HORMUZ IKIFUNGWA KABISA, NINI KITATOKEA?
Swali hili linaogopesha wachumi kuliko hata wanajeshi.
Kwa sababu madhara yake hayaishii Mashariki ya Kati.
Yanaweza kufika mpaka Tanzania.
Mafuta yakipanda duniani:
Gharama za usafirishaji hupanda
Bei ya bidhaa huongezeka
Mfumuko wa bei huongezeka
Tiketi za ndege hupanda
Chakula huanza kuwa ghali kutokana na gharama za usafiri
Uchumi wa nchi zinazoagiza mafuta huumia
Ndiyo maana hata nchi ambazo hazipo karibu na Iran zinafuatilia Hormuz kwa wasiwasi mkubwa.
China, ambayo ni mnunuzi mkubwa wa mafuta ya Mashariki ya Kati, ina sababu ya kuwa na hofu.
India pia.
Ulaya pia.
Na Afrika pia.
Kwa sababu dunia ya sasa imeunganishwa na minyororo ya biashara.
Tatizo la mafuta katika Ghuba ya Uajemi linaweza kuonekana kwenye bei ya sukari au usafiri Dar es Salaam siku chache baadaye.
IRAN ANATUMA UJUMBE GANI KWA DUNIA?
Iran inaonekana kusema jambo moja kubwa:
“Ikiwa mnataka kutushinikiza kisiasa na kijeshi, basi dunia nzima italazimika kuhisi maumivu ya mgogoro huu.”
Hii ndiyo nguvu ya jiografia katika siasa za kimataifa.
Iran huenda isiwe na uchumi mkubwa kuliko Marekani, lakini ina kitu ambacho dunia haiwezi kupuuza:
nafasi yake ya kijiografia.
Na hiyo ndiyo sababu mataifa makubwa yanaizungumza Tehran kwa tahadhari kubwa.
Historia pia inaonyesha kuwa kila mvutano mkubwa Hormuz unapoongezeka, masoko ya hisa, mafuta na usafiri wa kimataifa huanza kuyumba hata kabla risasi kubwa hazijaanza kupigwa.
Kwa sababu katika siasa za dunia, wakati mwingine hofu huwa na nguvu kuliko vita yenyewe.
JE, DUNIA INAENDA KWENYE MGOGORO MPYA WA NISHATI?
Hili ndilo swali kubwa sasa.
Ikiwa mazungumzo kati ya Iran na Marekani yatafanikiwa, huenda njia hiyo ikafunguliwa upya na hali ikatulia.
Lakini ikiwa diplomasia itashindwa, dunia inaweza kuingia kwenye kipindi kingine kigumu cha mshtuko wa mafuta, sintofahamu ya biashara na mvutano wa kijeshi.
Na hapo ndipo dunia italazimika kujiuliza swali ambalo imekuwa ikilikwepa kwa miaka mingi:
Kwa nini uchumi wa dunia utegemee mlango mmoja mwembamba wa maji?
NJIA MPYA AMBAZO DUNIA INAPASWA KUZIFIKIRIA SASA
Tatizo kubwa la migogoro mingi ya kimataifa ni kwamba dunia hupenda kuzima moto wa leo bila kujenga kinga ya kesho.
Hormuz imekuwa ikitikisa dunia kwa miongo mingi, lakini bado mfumo wa biashara ya nishati umeendelea kutegemea eneo hilo kwa kiwango hatari.
Na hapa ndipo dunia inahitaji mawazo mapya — si mikakati ileile iliyochoka.
Kwanza, mataifa makubwa yanapaswa kuanzisha “Neutral Energy Corridor” chini ya usimamizi wa kimataifa, si wa kijeshi pekee.
Badala ya kila taifa kupeleka meli zake kivyake na kuongeza presha ya kivita, dunia inaweza kuunda ukanda maalum unaosimamiwa na muungano mpana wa kimataifa kupitia United Nations, ukiwa na wajumbe kutoka mataifa yanayopingana yenyewe.
Lengo lake lisiwe kushinda kisiasa, bali kuhakikisha mafuta, chakula na bidhaa muhimu vinaendelea kupita bila kugeuzwa silaha ya kisiasa.
Pili, dunia lazima iharakishe uwekezaji kwenye njia mbadala za usafirishaji wa mafuta.
Baadhi ya nchi za Ghuba tayari zina mabomba ya mafuta yanayoweza kupitisha sehemu ya mafuta bila kupitia Hormuz, lakini uwezo wake bado ni mdogo ukilinganishwa na mahitaji ya dunia.
Hii ina maana kuwa dunia inahitaji mtandao mkubwa zaidi wa mabomba ya mafuta yanayounganisha maeneo tofauti ya usafirishaji ili kupunguza utegemezi wa mlango mmoja.
Kwa mfano, kuongeza uwezo wa mabomba yanayopita Bahari ya Shamu kuelekea Red Sea au Bahari ya Mediterranean kunaweza kupunguza presha kwa Hormuz.
Tatu, dunia lazima iache kutegemea mafuta kama uti wa mgongo pekee wa uchumi wake.
Kadri dunia inavyochelewa kuwekeza kikamilifu katika nishati mbadala, ndivyo migogoro kama hii itaendelea kuitikisa sayari nzima.
Leo vita vya mafuta vina uwezo wa kuyumbisha uchumi wa dunia kwa sababu dunia bado inategemea mafuta kwa kiwango kikubwa.
Lakini kadri magari ya umeme, nishati jadidifu na teknolojia mbadala zinavyoongezeka, ndivyo nguvu ya “silaha ya Hormuz” itakavyopungua.
Nne, dunia inahitaji diplomasia mpya inayowahusisha wale wanaoumia kimya kimya.
Mazungumzo mengi kuhusu Hormuz hujikita kwa Marekani, Iran au Israel pekee, wakati nchi zinazoathirika kiuchumi zaidi mara nyingi hazipo mezani.
Mataifa ya Afrika, Asia na Amerika Kusini yanapaswa kuwa sehemu ya majadiliano hayo kwa sababu madhara ya mgogoro huu yanafika mpaka kwa wananchi wao wa kawaida kupitia kupanda kwa bei za maisha.
Na huenda hapo ndipo suluhisho la kweli likaanza kupatikana.
Kwa sababu wakati mwingine amani hailetwi na mwenye nguvu zaidi mezani…
Bali na yule anayekumbusha wote gharama ya kuendelea kupigana.
Hormuz ni mdogo kwenye ramani.
Lakini kwenye siasa za dunia — ni mkubwa kuliko mataifa mengi.
“Msongamano wa meli katika Hormuz unaonyesha jinsi dunia ilivyoitegemea njia hii nyembamba ya maji.”
Imeandaliwa na Victor Bariety -0757-856284









0 Comments