CHATO INAZIKA WATU, LAKINI KUMBUKUMBU ZAKE HAZIFI

CHATO INAZIKA WATU, LAKINI KUMBUKUMBU ZAKE HAZIFI

“Picha ambayo leo imebaki kuwa kumbukumbu ya upendo wa mama na mwana… Chato ikilia, Tanzania ikikumbuka.”
Loyce “Alikuwa akihangaika kuokoa maisha ya wengine… leo naye amebaki kuwa kumbukumbu.”

..............................

Kuna maeneo duniani yakitajwa, watu hukumbuka utalii.

Mengine hukumbusha biashara.

Lakini kuna maeneo ambayo yakitajwa tu, moyo wa mtu huanza kubeba historia, siasa, machozi na kumbukumbu kwa wakati mmoja.

Na kwa Tanzania… Chato ni moja ya maeneo hayo.

Kwa sababu Chato haikubeba jina la kawaida.

Ilibeba simulizi ya mtu aliyeifanya dunia isimame imsikilize.

John Pombe Magufuli.

Mwanaume ambaye wengine walimuita dikteta.

Wengine wakamuita mzalendo.

Wengine wakamuita chuma cha pua.

Lakini wote wakakubaliana jambo moja:

Hakuwa rais wa kawaida.

Na leo, miaka michache baada ya taifa kumzika, Chato imelia tena.

Mama yake mzazi, Bi. Suzana Magufuli, ameondoka duniani.

Mama aliyemzaa mtoto aliyekuja kubadili mjadala wa Tanzania.

Mama aliyemlea kijana wa kawaida wa Chato mpaka akaja kutikisa Ikulu, Afrika na dunia.

Lakini ndani ya msiba huu, kuna majonzi mengine yaliyofufuka kimya kimya.

Maana kabla hata machozi ya familia ya Magufuli hayajakauka vizuri…

taifa lilikuwa bado linamkumbuka mwanamke mwingine aliyeliacha jina lake ndani ya nyumba hiyo.

Loyce Alexander Ndimuhela.

Muuguzi.

Lakini si muuguzi wa kawaida.

Alikuwa mmoja wa watu waliokuwa karibu sana na Mama Suzana katika kipindi chake cha kuugua.

Na sasa jambo la kuumiza ni hili:

Muuguzi aliyekuwa akihangaika kuokoa afya ya mama wa Magufuli… naye leo ni marehemu.

Jaribu kuwaza ukimya wa nyumba hiyo.

Kwanza wakaondokewa na mwana aliyekuwa rais.

Baadaye wakaondokewa na mtu aliyekuwa akiuguza mama yao kwa moyo mkubwa.

Leo wameondokewa na mama mwenyewe.

Ni kama historia imeamua kuandika sura zake kwa wino wa machozi.

Na ndiyo maana msiba huu haupo kawaida.

Kwa sababu haujaibua tu kumbukumbu za mama aliyefariki.

Umeibua tena enzi nzima ya Magufuli.

Enzi ambazo watu walikuwa wakiamka alfajiri kusikiliza hotuba zake.

Enzi ambazo mawaziri walitetemeka.

Enzi ambazo uzembe uliogopa kutajwa hadharani.

Enzi ambazo Tanzania ilionekana kuwa na rais anayependa matokeo kuliko maelezo.

Ukilitaja jina la Magufuli leo, bado kuna watu macho yao hubadilika.

Wengine hujaa furaha.

Wengine huzama kwenye mjadala.

Wengine hukaa kimya kana kwamba wamekumbuka jambo zito moyoni.

Hiyo ndiyo nguvu ya viongozi wanaoacha alama.

Hawaondoki kirahisi kwenye akili za watu.

Na pengine ndiyo maana hata kifo cha mama yake hakijabaki kuwa taarifa ya kawaida ya msiba.

Kimekuwa kama mlango uliorudisha taifa nyuma.

Nyuma ya zile safari za kushtukiza bandarini.

Nyuma ya zile kauli zilizotikisa mikutano.

Nyuma ya zile siku ambazo watu walihisi nchi inaendeshwa kwa kasi ya tofauti.

Lakini katikati ya historia hiyo yote kubwa, kulikuwa na watu wa kawaida waliobeba maumivu ya kimya kimya.

Mmoja wao akiwa Loyce.

Wengi walimjua akiwa muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Chato.

Lakini walio karibu naye walimjua kama mtu mwenye moyo uliovuka mshahara wake.

Alihudumia wagonjwa kwa upendo.

Aliwahudumia wazee kwa moyo.

Na kwa mujibu wa ushuhuda wa familia ya Magufuli, alikuwa mmoja wa watu waliokuwa mstari wa mbele kufuatilia hali ya Mama Suzana.

Ndiyo maana wakati wa msiba wake, familia ya Magufuli ililia kama iliyopoteza ndugu wa damu.

Kwa sababu huduma ya kweli huwa haibebi cheo.

Hubeba moyo.

Na pengine huo ndio ukweli mchungu ambao taifa huuchelewa kuuelewa.

Kwamba wakati mwingine, watu wakubwa sana duniani huokolewa na watu wadogo sana kwenye mfumo.

Muuguzi. Dereva. Mlinzi. Mtumishi wa kawaida.

Watu ambao majina yao hayaingii kwenye headlines kila siku… lakini wakiondoka, pengo lao haliwezi kuzibwa kirahisi.

Leo ukiiangalia familia ya Magufuli, unaweza kuona zaidi ya siasa.

Unaweza kuona simulizi ya maisha.

Mama aliyemzaa rais ameondoka.

Muuguzi aliyekuwa karibu naye ameondoka.

Na rais mwenyewe aliondoka kabla yao.

Ni kama Chato imebaki kuwa makumbusho ya kumbukumbu ambazo hazitaki kuisha.

Lakini pengine ndani ya huzuni hii yote, kuna somo kubwa kwa taifa.

Kwamba mwisho wa maisha, kinachobaki siyo cheo pekee.

Kinachobaki ni namna ulivyowagusa watu.

Magufuli aliacha alama kwenye taifa.

Mama Suzana akaacha historia kupitia mwana aliyemlea.

Na Loyce akaacha heshima kupitia huduma yake.

Hiyo ndiyo sababu leo watu wanawalilia kwa namna tofauti.

Maana kuna watu ukisikia wamefariki, unasema:

“Pole.”

Lakini kuna watu ukisikia wameondoka… moyo wako hukaa kimya kwa sekunde kadhaa kwanza.

Kwa sababu unajua kuna zama zimeguswa.

Na leo, Tanzania haigusi tu msiba wa mama wa Magufuli.

Inagusa kumbukumbu nzima ya enzi ambayo bado haijaondoka kabisa kwenye mioyo ya watu.

Pengine ndiyo maana mpaka leo, ukilitaja jina la Magufuli mahali popote Tanzania, watu hawaulizi kwanza alikuwa nani.

Wanaanza kukumbuka walikuwa wapi wakati akiwa hai.

...............................

Imeandaliwa na: Victor Bariety — 0757-856284 Mwandishi wa Habari na Mchambuzi wa Masuala ya Jamii

Post a Comment

0 Comments