ZANZIBAR, TUME YA TAIFA YA UNESCO, TAASISI YA SANZE CONNECT KUANDAA KONGAMANO LA KIMATAIFA LA UTAMADUNI

ZANZIBAR, TUME YA TAIFA YA UNESCO, TAASISI YA SANZE CONNECT KUANDAA KONGAMANO LA KIMATAIFA LA UTAMADUNI

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Khamis Abdalla Said (katikati), akiwa  na viongozi mbalimbali baada ya kikao cha kuratibu maandalizi ya Kongamano la Kimataifa la Utamaduni.

.......................

Na Dotto Mwaibale

SERIKALI ya Mapinduzi (SMZ), Tume ya Taifa ya UNESCO pamoja na Taasisi ya Sanze Connect kuandaa kongamano la Kimataifa la Utamaduni.

Lengo la kongamano hilo ambalo litafanyika kuanzia Mei 16 hadi 21, 2026 limelenga kuitangaza Zanzibar kama kitovu cha urithi na diplomasia ya utamaduni duniani.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Khamis Abdalla Said  akiongoza kikao cha kuratibu maandalizi ya Kongamano hilo alisema ni la muhimu sana.

“Kongamano hilo la Kimataifa la Utamaduni (International Cultural Summit) ni la muhimu sana nan i hatua inayolenga kuitangaza Zanzibar kama kitovu cha urithi na diplomasia ya utamaduni duniani,” alisema Said.
 

Katika kikao hicho kilichofanyika Aprili 15,  2026 katika ofisi za wizara, kilihusisha wadau wa kimataifa na kitaifa wakiwemo Tume ya Taifa ya UNESCO na Taasisi ya Sanze  Connect, pamoja na watendaji wa idara mbalimbali za wizara hiyo.

Ili kuhakikisha ufanisi wa maandalizi hayo, kikao kiliangazia maeneo kadhaa muhimu :

Ushirikiano wa Kimataifa: Kuimarisha mahusiano kati ya Zanzibar na jumuiya ya kimataifa kupitia nyanja za sanaa, utamaduni, na michezo kama nyenzo ya kukuza uchumi wa buluu na utalii.

Maingiliano ya Kitaasisi: Kujenga mfumo thabiti wa mawasiliano kati ya Tume ya UNESCO na SANZE Connect katika kufanikisha malengo ya Summit hiyo.

Usimamizi wa Idara: Kuhakikisha idara zote za wizara zinafanya kazi kwa ushirikiano ili kuleta taswira chanya ya nchi wakati wa kongamano hilo.

"Kikao hiki ni dira katika kuhakikisha Zanzibar inatumia fursa ya International Cultural Summit kuonesha utajiri wake wa kiutamaduni na vipaji vya vijana wetu katika jukwaa la kimataifa," alieleza Naibu Katibu Mkuu wakati wa kikao hicho.

Kikao hicho kilihitimisha hatua ya kwanza ya upangaji mikakati, kikisisitiza dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza sekta za ubunifu na michezo kama nguzo muhimu za maendeleo ya kijamii 


 

Post a Comment

0 Comments