WAZAZI CCM WILAYA YA ILALA WAASWA KUEPUKA MAKUNDI

WAZAZI CCM WILAYA YA ILALA WAASWA KUEPUKA MAKUNDI

 Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Ilala, Mtiti Mbassa, akimkabidhi cheti za pongezi Mwenyekiti wa Wazazi Kata ya Vingunguti, Rukia Wawila.

........................................

Na Mwandishi Wetu.  

VIONGOZI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ngazi ya matawi na kata wameaswa vikali kuepuka kujiingiza katika makundi ambayo  yanaweza kusababisha mpasuko ndani ya chama hicho.

Hayo yalisemwa na Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Wilaya ya Ilala, Mtiti Mbassa, akiwa katika ziara ya kuimarisha uhai wa jumuiya na chama iliyofanyika Kata ya Vingunguti na Kisukuru, Aprili 24, mwaka huu, jijini Dar es Salaam. 

Ziara hiyo ambayo ya kiutendaji zaidi, Mtiti alisema imebarikiwa na mwenyekiti wake wa jumuiya hiyo, Mohamed Msofe.         

"Nimeagizwa na mwenyekiti wangu komredi Mohamed Msofe, niwape salamu,  kuwapongeza na kuwapa cheti cha shukurani kwa kujitokeza kwa wingi kumchagua Rais Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana," alisema Mtiti. 

Mtiti ambaye alimkabidhi cheti  Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Vingunguti, Rukia Wawila, kwa niaba ya wanachama wote wa kata hiyo, alisema jumuiya ya wazazi  inafuata kanuni na katiba ya CCM kufanya majukumu yake. 

Alisema jumuiya ya wazazi inafuata mwongozo wa katiba ya CCM ambayo ina kanuni zake.                  

Alisema kutokana na hilo, viongozi wa jumuiya ya wazazi CCM inayo majukumu ya kufanya ikiwamo kutembelea shule za awali, msingi na sekondari kwa lengo la kusikiliza kero na wao kushauri ili ziweze kutatuliwa.  Pia, jumuiya ya wazazi ina jukumu la kusimamia maadili ya taifa, afya, malezi na mazingira, utamaduni.

Katibu huyo, alisema kazi ya jumuiya ya wazazi haipo kwa ajili ya kusubiri uchaguzi, kwani inayomajukumu ya kufanya kwa kipindi hiki.

Alisema kwa kueleweka hilo, viongozi wa jumuiya CCM ngazi ya matawi na kata mnatakiwa kufanya kazi na kuachana na makundi ya kupanga safu ya viongozi katika uchaguzi wa mwakani 2027.                 

Mtiti alisema  kufanya vikao visivyofuata utaratibu vinaweza kusababisha mpasuko ndani ya jumuiya na chama.        "Achaneni na makundi yatasababisha mpasuko, tuondoe makundi," Tusiingie kwenye makundi, tutagawanyika, tutathimini namna ya kujenga chama," alisema.

Katibu huyo, alisema viongozi wa matawi na kata wakionyeshana makundi kuelekea uchaguzi wa 2027  watakigawa chama katikati na kusababisha mpasuko.

Alisema ukihujumu jumuiya ya wazazi utakuwa umewahujumu baba na mama ambao ni wanachama wa jumuiya hiyo. 

"Ondoeni makundi kuepuka mpasuko ndani ya jumuiya ya wazazi CCM," alisema katibu huyo.                     

 Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Vingunguti, Rukia alimpongeza Mtiti na kamati ya utekelezaji ya wilaya kutokana na uwepo wa ziara hiyo, ambayo kwao imekuwa ni somo kubwa. 

Rukia alisema kuwa wamepokea kwa shukurani cheti na maagizo yote na wao kama chama watayatekeleza kwa mujibu wa kanuni.  Naye, Mwenyekiti wa kamati ya shule ya Mtakuja, Mussa Kassim Ahmed,  alimshukuru katibu wa wazazi CCM, wilaya, Mtiti na kusema hajawahi kuwapo kwa katibu kama huyo kutokana na uhodari wake wa kufanya kazi. 

Ahmed alisema kama mwenyekiti wa kamati ya shule hawajawahi kupewa mafunzo kuhusu kanuni za jumuiya ya wazazi, hivyo ni jambo la kumshukuru katibu huyo kwa kufanya ziara katika kata 36 za Ilala.      "Tumepewa somo sahihi lina maantiki sana shuleni," alisema Ahmed. 

Katika ziara hizo, kamati ya utekelezaji ya jumuiya ya wazazi CCM wilaya ya Ilala, inakutana na viongozi wa jumuiya ngazi ya matawi na kata, watendaji wa mitaa na kata, wenyeviti wa mitaa na kamati zake. 

Wengine walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari, kamati za shule, Ofisa elimu kata, afya na mazingara.  

Post a Comment

0 Comments