TABATA WAFURIKA MKUTANO JUMUIYA YA WAZAZI ILALA

TABATA WAFURIKA MKUTANO JUMUIYA YA WAZAZI ILALA

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Ilala, Mtiti Mbassa akimkabidhi Kitabu cha Kanuni Afisa Elimu Kata ya Tabata, Hadija Karia  wakati wa mkutano maalum wa kiutendaji uliofanyika juzi Kata ya Tabata, jijini Dar es Salaam. 

..............................

Na Mwandishi Wetu.  

WANACHAMA na viongozi wa ngazi ya matawi na kata wa Jumuiya ya  Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Ilala, wamefurika katika mkutano maalum wa kiutendaji uliofanyika juzi Kata ya Tabata, jijini Dar es Salaam. 

Mkutano huo ambao ulihudhuriwa na watu wengi wakiwamo walimu wakuu na kamati zao za shule ni mwendelezo wa ziara ya uongozi wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Ilala chini ya Mwenyekiti wake,  Mohammed Msofe  yenye lengo la kuimarisha uhai, usajili wa wanachama wapya na ulipaji ada ya uanachama wa jumuiya hiyo. 

Akizungumza katika mkutano huo, katibu wa  jumuiya hiyo, Mtiti Mbassa, alisema kwa mujibu wa kanuni wana majukumu mapana ya kusimamia masuala elimu, afya, malezi, mazingira, utamaduni na maadili ya Taifa kwa watoto wa shule za awali, msingi na sekondari. 

Mtiti alisema kamati ya utekelezaji ya jumuiya hiyo ina kazi ya kufanya kwa kushirikiana na kamati za shule za msingi na sekondari kwa kuzitembelea shule kwa kufuata utaratibu kwa lengo la kujua changamoto na baadaye kutoa ushauri. 

Katika mkutano huo, Mtiti alisema jumuiya ya wazazi CCM si ya kusubiri uchaguzi, bali inayokazi kubwa ya kufanya kwa mujibu wa kanuni. 

Pia, Mtiti alisema jumuiya hiyo ambayo imeundwa na CCM,  inamajukumu ya kuunganisha nguvu wazazi kuanzia ngazi ya matawi, kata na wilaya kwa ajili ya kuendeleza elimu ya awali, msingi na sekondari. 

Mtiti alisema viongozi wa jumuiya hiyo ngazi ya matawi haipo kwa lengo la kupanga safu ya viongozi, bali ipo kiutendaji zaidi.

Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza Kuu la Jumuiya ya Wazazi Taifa, Sudi Kasim Sudi, alimpongeza Mtiti kwa kufanya nzuri ya kutoa elimu kwa viongozi wa matawi na kata. 

Sudi ambaye ni diwani wa Kata ya Tabata alisema amefarajika na utendaji wa Mtiti, ambaye anashuka chini kufanya kazi kwa kujitolea na halipwi chochote katika ziara zake. 

Kamati ya utekelezaji ya jumuiya hiyo  inaendelea na ziara ya kiutendaji katika kata 36 za wilaya ya Ilala.  

Mkutano ukiendelea.
 

Post a Comment

0 Comments