.......................................
Na Mwandishi Wetu
KATIBU wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam, Mtiti Mbassa, amesema kwamba watakaobainika wanapanga safu ya viongozi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2030 watachukuliwa hatua dhidi yao kwa mujibu wa kanuni.
Mtiti aliyasema hayo katika mwendelezo wa ziara ya Kamati ya Utendaji ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM, Ilala, iliyofanyika Aprili 14, mwaka huu, akiwa Kata ya Kipawa, Ilala.
Kamati hiyo ipo katika ziara ya Kata 36 za Wilaya ya Ilala lengo ni kuwakumbusha viongozi wa matawi na kata kuhusu kuimarisha uhai wa jumuiya na chama CCM
Akizungumza katika kikao hicho, Mtiti alisema jumuiya ya wazazi imeanzishwa na CCM kwa ajili ya kufanya kazi za kiutendaji zaidi na si kupanga safu za viongozi.
Alisema jumuiya ya wazazi ina jukumu la kusimamia mambo mengi ikiwamo elimu, afya, maadili ya Taifa, utamaduni, malezi na mazingira.
Mtiti alisema jumuiya ya wazazi CCM ni ya kiutendaji zaidi na si ya kusubiri uchaguzi, hivyo atakayebainika kuendesha vikao kiholela vya kupanga safu ya viongozi 2030 watachukuliwa hatua kwa mujibu wa kanuni za jumuiya hiyo.
"Mnaopanga safu za viongozi 2030 kwenye matawi na kata, naomba nitoe maelekezo kama mtendaji wa Jumuiya ya Wazazi, nitachukua hatua kwa mujibu wa kanuni," alisema Mtiti.
Katibu huyo alisema hatakubali kuona ndani ya jumuiya kuwapo kwa vikao visivyofuata utaratibu.
Pia, alisema wazazi wakiwa ni sehemu ya jumuiya wanatakiwa kukaa na watoto wao kwa lengo la kuwafundisha maadili ya Taifa.
Mtiti alisema wazazi wanajukumu kubwa la kushirikiana na walimu kuwalea watoto wao ili waweze kupata maadili mema ambayo mara nyingi yanaanzia nyumbani.
"Watoto wetu wanapata shida, wanahangaika jinsi ya kupata elimu, maendeleo ya mtoto ni elimu," "Mzazi anapata mtoto jukumu lake ni kumsimamia asome, lakini akienda shuleni awe nadhifu muda wote," alisema Katibu huyo.
Alisema kuna baadhi ya wazazi wanashindwa kuwanunulia watoto wao nguo za ndani, kitu ambacho si kizuri, hivyo wanatakiwa kuwanunulia.
Mtiti alisema viongozi wa jumuiya ya wazazi wanajukumu la kutembelea shule za awali, msingi na sekondari kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali ikiwamo michango holela isiyofuata utaratibu wa serikali.
Alisema michango inayoruhusiwa na serikali ni ile ya wazazi kuchangia chakula na si vingine, labda kama wazazi watakubaliana katika kikao kitakachokuwa kimehitishwa na kamati ya shule.
Aidha, Mtiti aliwapongeza viongozi wa jumuiya ya wazazi CCM ngazi ya matawi, kata na wanachama wote wa Kata ya Kipawa kwa kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan, mbunge na madiwani katika uchaguzi mkuu uliopita.
Naye, Mjumbe wa Baraza la (UWT), Wilaya ya Ilala, Dk. Elizabeth Kilili, aliwaomba wazazi kushirikiana kwa pamoja na walimu katika malezi na maadili ya Taifa kwa watoto, kwani kuna mmonyoko mkubwa wa kimaadili.
Pia Dk Elizabeth aliwapongeza walimu kwa majukumu makubwa ya kufundisha watoto huku akiahidi kutekeleza maelekezo yote ya Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Ilala.
Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Kata ya Kipawa, Alice Hwai, alipongeza ziara ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Ilala, chini Katibu mtendaji Mtiti kwa kuwapa somo kuhusu kuwashirikisha wazazi katika suala nzima la elimu na wamepokea maelekezo na kuahidi kuyafanyia kazi.
Katika kikao hicho, kilihudhuriwa na mtendaji kata, ofisa elimu, afya na mazingira, alimu, kamati za shule za msingi na sekondari na wenyeviti wa serikali za mitaa.
Wengine ni viongozi wa jumuiya ya wazazi ngazi ya matawi, wanachama, wenyeviti mashina na kata.









0 Comments