MTITI AHIMIZA USAJILI, ULIPAJI ADA JUMUIYA YA WAZAZI CCM ILALA DAR ES SALAAM

MTITI AHIMIZA USAJILI, ULIPAJI ADA JUMUIYA YA WAZAZI CCM ILALA DAR ES SALAAM

   Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Ilala (CCM), Mtiti Mbassa, akizungumza na viongozi ngazi ya matawi na Kata ya Buyuni Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam Aprili 9, 2026.

....................................

Na Mwandishi Wetu.

UONGOZI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam,  umekutana na viongozi ngazi ya matawi na Kata ya Buyuni, kwa lengo la kuimarisha uhai wa jumuiya hiyo.

Katika kikao hicho, kilichofanyika leo, Aprili 9, mwaka huu, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Ilala (CCM), Mtiti Mbassa, alisisitiza usajili wa wanachama wapya ufanyike kupitia mfumo wa TEHAMA kwa lengo la kuimarisha chama na Jumuiya zake. 

Alisisitiza kwamba kila wiki ndani ya siku moja, viongozi wa matawi wa jumuiya hiyo wanatakiwa kufanya usajili wa wanachama wapya.

Katika kikao hicho kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Maramasha, Buyuni, Mtiti alisisitiza kwamba pamoja na usaji wa wanachama, lakini wanatakiwa kulipa ada ya uanachama  kama kanuni inayoelekeza.

Kikao hicho ambacho ni mwendelezo wa ziara ya viongozi wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya Ilala, chini ya katibu Mtiti kililenga kuwakumbusha viongozi wa matawi na kata kuhusu uwajibikaji wa uongozi.

Katika kikao hicho, Mtiti aisema Jumuiya ya wazazi ni pana katika kiutendaji, hivyo wafanye kazi kwa ajili ya kuleta maendeleo.

Katibu huyo alisema kupitia vikao Jumuiya ya wazazi walimu wanaweza kuwatumia viongozi wa matawi wa Jumuiya na chama ili kujadii masuala mbalimbali yanayohusu elimu ya msingi na sekondari.

Mtiti alisema baada ya uchaguzi hiki ni kipindi cha kufanya kazi, hivyo viongozi wa Jumuiya ngazi ya tawi na kata wanajukumu la kutembelea shule za awali, msingi na sekondari kama kanuni inayoelekeza.

Pia, Mtiti aliwataka walimu ya shule za msingi na sekondari kuwashirikisha viongozi na wanachama jumuiya hiyo katika mipango yao ya maendeleo ya shule. 

Katibu huyo alisema  jumuiya ya wazazi inatakiwa kufanyakazi kwa kushirikiana na jumuiya nyingine ya wanawake na vijana, hivyo hatakubali kuona ukitokea mgawanyiko.

"Sitakubali Jumuiya ya Wazazi igawanyike, niko tayari kuchukua hatua kwa mujibu ya kanuni zetu," alisema Mtiti.

 "Niwaombe walimu kuwapokea viongozi wa jumuiya ya wazazi, watakapotoa taarifa ya kuwatembea shuleni kwa kufuata utaratibu wa chama," alisema.

Katika kikao hicho cha kiutendaji kilihudhuriwa na Ofisa elimu kata ya Buyuni, Mtendaji kata, wenyeviti wa serikali ya mitaa, viongozi wa matawi, kata na wanachama wa chama hicho.                             

Wakati huo huo, Mtiti amewataka viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ngazi ya tawi, kata na wanachama wote kujitokeza siku ya kukimbiza Mwenge wa Uhuru.

Mtiti alisema Mwenge huo unatarajia kuingia Ilala Aprili 13, mwaka huu.

Alisema kwa kufanya hivyo watakuwa wamemuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Wilaya Ilala, Edward Mpogolo katika suala nzima la ukimbizaji wa Mwenge wa Uhuru. 

Katika kikao hicho viongozi ngazi ya tawi na kata walifurahia  na kuahidi kuanza utekelezaji ili kuendana na mpangokazi na ratiba za vikao.

Post a Comment

0 Comments