...............................
Na Mwandishi Wetu.
KAMATI ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ilala, jijini Dar es Salaam, imeanza ziara ya kikazi kwa mbwembwe katika Kata 36 za wilaya hiyo.
Kamati hiyo ilianza ziara leo Jumanne Aprili 7, mwaka huu, katika Kata ya Zingiziwa, ikiongozwa na katibu wa jumuiya hiyo, Mtiti Mbassa ambaye alipiga marufuku michango holela isiyofuata utaratibu shuleni.
Akizungumza na viongozi mbalimbali wa CCM na Serikali, Mtiti alisema suala la michango holela isiyofuata taratibu sasa basi na ikome.
Alisema kuwa mchango unaokubalika ni ule ambao upo kwenye utaratibu wa serikali, lakini sio vinginevyo.
Katibu huyo wa jumuiya ya wazazi alisema kazi yao ni kupokea kero mbalimbali kwa upande wa elimu, afya, malezi na mazingira na utamaduni, pia kushauri jinsi ya kuzitatua.
Mtiti aliyetanguzana na wajumbe wa kamati ya utekelezaji ya jumuiya hiyo, alisema siku ya Aprili 7, ilikuwa ya Kumwezi Hayati Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Abeid Aman Karume.
Alisema kuwa Hayati Abeid Karume alisisitiza masuala ya malezi, elimu, afya, ustawi wa jamii na mazingira.
Pia Mtiti alisema kutokana na hilo, jumuiya ya wazazi inawajibu wa kwenda kusikiliza kero katika shule za msingi na sekondari.
"Leo nimeanza ziara hapa Zingiziwa, kesho nitakuwa Chanika, Buyuni....lengo ni kupokea na kusikiliza kero na sio kutoa uamuzi, sisi kazi yetu ni kushauri baada ya kuzipokeai," alisema Mtiti.
Pia, Mtiti alisema viongozi wa jumuiya ya wazazi ngazi ya matawi wanaojukumu la kutembelea shule kwa lengo la kusikiliza kero mbalimbali na kuzipeleka kwa uongozi wa CCM kata husika ili uweze kuja na ushauri kwa serikali.
Katika ziara hiyo iliyohusisha walimu wakuu wa shule ya msingi na sekondari, wenyeviti wa mitaa, mtendaji kata, ofisa elimu kata, ofisa afya, ustawi wa jamii na viongozi wa CCM ngazi ya matawi na kata, Mtiti alipongeza kwa kazi nzuri inayofanywa na viongozi wa jumuiya ya wazazi kwa ngazi ya matawi kwa kutembelea shule na kusikiliza kero.
Akifungua mkutano katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Wazazi wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Zingiziwa, Benedictor Madhifu, alisema kuwa walimu wanajitahidi kufundisha, kwani shule zao zinafaulisha vizuri.
Mwenyekiti huyo alisema ufaulu mzuri katika shule ya. Sekondari Zingiziwa umewafanya wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali kutaka kusoma katika shule hiyo.









0 Comments