.........................
Na Mwandishi Wetu. Dar es Salaam
VIONGOZI wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Wilaya Ilala, jijini Dar es Salaam, wanatarajiwa kuanza ziara ya kikazi Aprili 7, 2026.
Akizungumza jana, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi (CCM), Ilala, Mtiti Mbassa, alisema kuwa baada ya uchaguzi mkuu wa urais, wabunge na madiwani kufanyika Oktoba 29, mwaka jana wamejipanga kuendelea kujenga na kukimarisha chama katika nyanja zote za uongozi.
"Mwaka huu wa 2026 ni wa kufanya kazi baada ya kufanyika uchaguzi mkuu mwaka jana," alisema Mbassa.
Katika uchaguzi mkuu huo, ambao Dk. Samia Suluhu Hassan alichaguliwa kuwa rais, Mbassa alisema kamati ya utendaji ndani ya jumuiya hiyo itafanya ziara kwenye kata 36 na matawi 224 ya CCM, wakianzia Kata ya Zingiziwa.
Katibu huyo wa jumuiya ya wazazi, alisema katika ziara yao watasikiliza kero za jamii na kuona namna ya kuzitatua.
Mbassa alisema kuwa jumuiya ya wazazi, inawajibu ya kusimamia masuala elimu kwa shule za msingi na sekondari, malenzi, afya na mazingira, hivyo ziara yao itaelemisha jamii na kutoa ushauri pale patakapokuwapo na changamoto.
Alisema kuwa kamati ya utendaji ya jumuiya hiyo, ambayo inabeba jukumu la elimu itakutana na kamati na bodi za shule husika.
Pia, Mbassa alisema kuwa katika ziara hiyo, wanatarajia kukutana na viongozi mbalimbali wa jumuiya ya wazazi ngazi ya matawi na kata, wenyeviti wa serikali ya mitaa, madiwani, ofisa ustawi wa jamii na wengineo, lengo kubwa kukimarisha chama, lakini kusikiliza kero za jamii na namna ya kuzishughulikia.
"Tunawaambia, jumuiya ya wazazi inafuata katiba na kanuni, tunawatembelea wanachama wote na kuelimisha jamii ambao ni wananchi kuhusu elimu," alisema Mbassa.
Wakati huo huo, Mbassa amewaomba wananchi kujitokeza kukimbiza mwenge wa Uhuru unaotarajia kuingia Wilaya ya Ilala, Aprili 13, mwaka huu.
Mbassa alisema mwenge wa Uhuru unaangaza maendeleo na kila unapopita unazindua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Katibu huyo alitoa rai kwa wananchi wa Ilala kujipanga barabarani wakati mwenge wa Uhuru utakapopita.









0 Comments