CCM YAJITOSA KUKABILIANA NA UKOSEFU WA MAFUTA NCHINI

CCM YAJITOSA KUKABILIANA NA UKOSEFU WA MAFUTA NCHINI

Yaishauri Serikali kutoa ruzuku kupunguza gharama

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo,Kenani Kihongosi  wakati akizungumza na waandishi wa habari  Aprili 7, 2026, Jijini Dodoma.

.........................................

CHAMA Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeingilia kati ukosekanaji wa mafuta nchini ambapo kimeishauri  Serikali  kutoa ruzuku ili kupunguza gharama za mafuta kama alivyofanya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan mwaka 2022 nchi ilipokuwa kwenye changamoto kama ilivyo hivi sasa.

Hayo yamebainishwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo,Kenani Kihongosi  wakati akizungumza na waandishi wa habari  Aprili 7, 2026, Jijini Dodoma.

“Tumeiagiza Serikali itoe ruzuku ili kupunguza gharama za mafuta kama ilivyofanywa mwaka 2022  wakati wa vita vya Urusi na Ukraine ambapo ilitoa Sh.Bilioni 100   hatua itakayo saidia kupunguza makali ya bei ya mafuta,” alisemaKihongosi.

Kihongosi aliongeza kuwa Serikali ipo katika mchakato wa kuanzisha Mfuko Maalumu utakaosaidia kupunguza makali ya bei ya mafuta ambayo imepanda kufuatia vita vinavyoendelea baina ya Israel, Marekani na Irani.

Alisema CCM na Serikali wamejipanga kuhakikisha  mafuta yanapatikana wakati wote na kwa bei nafuu ambapo alihimiza kubana matumizi ya safari za magari na kuelekeza katika kipindi hiki magari ambayo yapo katika mfumo wa matumiziya gesi yatumie nishati hiyo.

Alisema kuwa sababu ya kuongezeka kwa bei ya mafuta imetokana na kufungwa kwa mkondo wa bahari  unaotumika kusafirisha mafuta kutoka Mashariki ya Kati kuja Afrika Mashariki.

Kihongosi alieleza kuwa njia hiyo ya bahari hubeba takribani asilimia 20 ya mafuta duniani hivyo kufungwa kwake kunaleta changamoto ya moja kwa moja ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta.

Alisema kutokana na hali hiyo imesababisha bei ya mafuta katika soko la dunia kupanda kwa kiasi kikubwa, kutoka dola za Marekani 700–800 hadi kufikia dola 1,700–1,800 ongezeko ambalo  limeathiri  bei za ndani kwa kupanda kwa zaidi ya shilingi 800 hadi 1,000 kwa lita.

Kihongosi aliongeza kuwa gharama ya “premium” imeongezeka kutoka dola 80–110 hadi kufikia dola 270–300, hali iliyochangia ongezeko la zaidi ya shilingi 200 kwa lita, na kufanya jumla ya ongezeko kufikia zaidi ya shilingi 1,000.

Aidha, Kihongosi alisema kupanda kwa bei ya mafuta siyo kwa Tanzania pekee bali ni pamoja na baadhi ya nchi kama Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Afrika Kusini ambapo bei imefikia takribani shilingi 5,000 kwa lita huku nchini Kenya, bei ikiwa kati ya shilingi 3,500 hadi 4,000 kwa lita. 

Kihongosi alisema   ukosekanaji wa mafuta haupo kwa nchi za Afrika pekee, bali pia katika nchi za Ulaya na Asia, akitolea mfano Uswisi akieleza kuwa bei ni kati ya shilingi 5,000 hadi 6,000 kwa lita, na Uingereza kati ya shilingi 5,500 hadi 6,500 kwa lita.

Waandishi wa habari wakichukua taarifa hiyo.

Taarifa hii imeandaliwa na Dotto Mwaibale simu namba 0754362990

Post a Comment

0 Comments