MBUNGE DAVID KIHENZILE ATOA MILIONI 3 KUUNGA MKONO UJENZI WA OFISI YA CCM IDETE

MBUNGE DAVID KIHENZILE ATOA MILIONI 3 KUUNGA MKONO UJENZI WA OFISI YA CCM IDETE

NA DENIS MLOWE,  IRINGA 

MBUNGE wa Jimbo la Mufindi Kusini, David Kihenzile, ametoa mchango wa Shilingi milioni 3 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Idete, wilayani Mufindi. Mchango huo umetolewa wakati wa ziara yake ya siku nne jimboni humo ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha miundombinu ya ofisi za chama katika ngazi zote.

Akiwa katika eneo la ujenzi, Mbunge Kihenzile alikagua maendeleo na kuunga mkono jitihada za wanachama wa kata hiyo, akibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kurahisisha utendaji wa viongozi na kuwasogezea wanachama huduma za chama karibu zaidi.

Mbunge huyo amepongeza uongozi wa CCM ngazi ya taifa, mkoa na wilaya kwa kusimamia mageuzi ya kimfumo ya ujenzi wa ofisi, na kumshukuru Mwenyekiti wa Mkoa wa Iringa kwa kuandaa ramani na mpango kazi wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi mkoani humo. Aidha, alimtaja mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Salim Abri Asasi, kuwa mstari wa mbele katika kusukuma juhudi hizo ndani ya mkoa.

Katika jimbo la Mufindi Kusini, Kihenzile amesema kata nyingi zimeanza ujenzi wa ofisi mpya, huku akitolea mfano Kata ya Kiawela ambayo ilikamilisha ujenzi wa ofisi yake tangu mwaka 2020 baada ya ushindi wa asilimia 100 kwenye nafasi za urais, ubunge na udiwani.

Akipongeza uongozi wa CCM Wilaya ya Mufindi, alisema kuwa mpango maalumu wa wilaya kwa mwaka huu kuhusu ujenzi wa ofisi utawezesha utekelezaji wa maono ya chama bila changamoto kubwa. Kwa mujibu wake, jumla ya ofisi 15 zinatarajiwa kujengwa upya, kukarabatiwa au kukamilishwa kwenye kata mbalimbali.

Mbunge Kihenzile amewahimiza wanachama ndani na nje ya jimbo kuendelea kuchangia upatikanaji wa vifaa vya ujenzi kama bati, tofali, mbao, mchanga pamoja na fedha, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kutimiza maono ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Samia Suluhu Hassan, ya kuona chama kinaboresha miundombinu yake nchi nzima.

Post a Comment

0 Comments