Na Mashaka Kibaya,Kilindi.
DIWANI wa Kata ya Kikunde kupitia (CCM), Daniel Emmanuel Sembela, amepongeza utendaji kazi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa juhudi anazozifanya katika kusimamia na kutekeleza miradi ya maendeleo zinaonesha dhamira ya dhati ya kuharakisha maendeleo ya Watanzania.
Akizungumza na Mwandishi Wetu, Sembela alisema Serikali imeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo yenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kuwaondolea kero zinazowakabili katika shughuli zao.
Alitaja baadhi ya miradi inayoendelea kutekelezwa kuwa ni ile ya sekta ya afya, maji, miundombinu ya barabara, elimu pamoja na hata nishati ya umeme.
Alisisitiza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaleta ukombozi mkubwa kwa wananchi, hasa wale wa maeneo ya vijijini ambao kwa muda mrefu wamekumbwa na changamoto za huduma hizo muhimu za kijamii.
Kwa mujibu wa Sembela, uboreshaji wa huduma za afya utaongeza upatikanaji wa matibabu kwa wakati, huku miradi ya maji safi na salama ikisaidia kupunguza adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta huduma hiyo muhimu.
Pia Sembela alitumia fursa aliyoioata kuzungumzia miundombinu ya barabara na umeme, Diwani huyo alisema kuwa sekta hizo ni mhimili mkubwa wa maendeleo ya kiuchumi, hususan katika maeneo yenye rasilimali za madini.
Alifafanua kuwa Kata ya Kikunde ina maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu ambayo yanahitaji miundombinu bora ili wananchi waweze kuweza kunufaika huku tija ikiongezeka.
“Endapo barabara zitaimarishwa na huduma ya umeme kupatikana kwa uhakika katika maeneo yote ya kata yetu, hasa Seita kwenye wachimbaji wadogo wa madini, uchumi wa wananchi utakua kwa kasi kubwa,” alisema Sembela.
Aliongeza kuwa barabara bora zitawawezesha wananchi kusafirisha mazao yao kwa urahisi kutoka shambani hadi sokoni, jambo pia itakalosaidia kuongeza kipato chao na kukuza uchumi wa familia na wilaya kwa ujumla.
Sembela pia alizungumzia ziara ya Waziri Mkuu, Dkt Mwigulu Nchemba, aliyoifanya katika Wilaya ya Kilindi, akisema kuwa ziara hiyo imeamsha ari mpya na kuleta matumaini kwa wananchi kwamba Serikali iko pamoja nao katika kutatua changamoto zao.
Alisema kuwa katika ziara hiyo, Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Nchemba alisikiliza kero za wananchi na kusisitiza umuhimu wa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
"Tumefurahi sana kwa ujio wake. Tunaamini ziara yake itaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi na maeneo yetu yatapata ahueni,” alisisitiza.
Kutokana na hali hiyo, Sembela aliwahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali yao, akieleza kuwa Serikali imeonesha utayari wa dhati wa kuwatumikia na kutatua kero.
Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya wananchi na viongozi ni msingi muhimu wa mafanikio ya miradi ya maendeleo.
Kwa upande mwingine, aliwasihi madiwani wenzake kuendeleza mshikamano na kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya Wilaya ya Kilindi.
Kwa upande wake mmoja kati ya Wamiliki wa leseni ya uchimbaji wa madini ya Wachapakazi Group kwenye mgodi wa Abeid Kaisi na Ibrahim Kuwasa ameishukuru Serikali kwa kutoa miongozo mizuri kwa wachimbaji.
Alisema,Serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imekuwa mstari wa mbele katika kuwapatia miongozo mbalimbali kwenye sekta hiyo ya madini hatua ambayo inasaidia tija kupatikana.
Ameiangukia Serikali kuwasaidia kutengeneza mazingira rafiki kwa wachimbaji akishauri eneo la Matanda ndogo kwenye kidongo chekundu kwenye uzalishaji mkubwa wa madini ya dhahabu kupatiwa umeme na miundombinu ya barabara kuimarishwa.










0 Comments