............................
Na Onesmo Kapinga Dar es Salaam
MWENYEKITI wa Serikali ya Mtaa wa Kinyamwezi, Ilala jijini Dar es Salaam, Fahard Mlali, amekabidhi vifaa vya ujenzi kwa Katibu wa Chama Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tawi la Kinyamwezi B, Mariam Masoud kwa ajili ya umaliziaji wa ujenzi wa ofisi ya chama hicho.
Vifaa vya ujenzi alivyokabidhiwa katibu huyo wa CCM ni pamoja na saruji, nondo na matofali.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo, Mariam, alimshukuru mwenyekiti wao kwa kutimiza ahadi yake aliyotoa wakati ya kampeni ya uchaguzi wa Serikali ya Mtaa uliofanyika Novemba 28, mwaka jana.
Mariam alisema ni nadra kwa viongozi wanaochaguliwa kupitia chama hicho kukumbuka na kutimiza ahadi zao, wanazotoa wakati wa kampeni za uchaguzi.
Alisema kitendo cha mwenyekiti wao kutimiza ahadi yake kimeheshimisha chama hicho.
"Kwetu sisi kama ni heshima kubwa kupokea vifaa hivi ambavyo vitakamilisha ujenzi wa ofisi yetu," alisema Mariam.
Katibu huyo, alisema ujenzi wa ofisi hiyo ulianza miaka 10 iliyopita, lakini ulishindwa kukamilika kutokana na kukosa fedha.
Aliwataka wadau wengine wa chama hicho kuiga mfano wa mwenyekiti huyo wa mtaa wa Kinyamwezi wa kusaidia chama katika shughuli zake za maendeleo.
Kwa upande wake, Mlali amesema atahakikisha ofisi hiyo ya Tawi CCM inakuwa ya kisasa zaidi.
Mwenyekiti huyo, alisema vifaa ujenzi alivyotoa ni sehemu ya ahadi mbalimbali alizotoa wakati wa kampeni na ndani ya mwaka mmoja ameweza kutimiza zote.
Alisema anaamini ujenzi wa ofisi utaendelea kwa kasi na kumalizika ili shughuli za kichama ziweze kufanyika hapo.
"Nataka ofisi hii iwe ya kisasa, pia ya mfano kabisa," alisema Mlali.
Hata hivyo, Mlali amemtaka mkandarasi aliyepewa jukumu la ujenzi wa ofisi hiyo, Jafari Seif kukamilisha haraka ili shughuli za chama ziweze kufanyika katika ofisi hiyo.
Kwa upande wa mkandarasi huyo, alisema akiwezesha kupata vifaa vyote kwa wakati ndani ya mwezi mmoja ujenzi utakuwa umekamilika.







0 Comments