.........................................
Na Mwandishi Wetu.
MMILIKI wa Shule za Msingi za Dimaks na Dynamic, Dickson Mwaijibe, amesema ameweka mazingira bora ili wanafunzi waweze kupata elimu kwa kiwango cha juu na afya njema.
Pamoja na mikakati yake hiyo, Mwaijibe alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kutoa fursa ya uwekezaji katika sekta ya elimu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam, Mwaijige alisema kuwa wamejipanga kuboresha mazingira ya shule ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora kwa kiwango cha juu.
Alisema shule hizo ambazo zinafundisha mchepuo wa kiingereza zinatilia mkazo somo la Hisabati la Lugha ya Kiingereza ambayo inaunganisha watu wengi katika dunia kidigitali.
Mwaijibe ambaye ni Diwani wa Kata ya Tambani, Wilayani Mkuranga, mkoani Pwani, alisema kuwa amefanikiwa kujenga shule mbili, ikiwamo ya Dimaks ambayo ipo Mbarali mkoani Mbeya.
Alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka jana, ilitanguliwa na Dynamic iliyopo Mbagala Maji Matitu jijini Dar es Salaam, ambayo imekuwa ikitoa matokeo mazuri katika mtihani wa Taifa kwa wanafunzi wake kupata alama A na B.
Mwaijibe alisema katika matokeo ya shule ya Dynamic yamemsukuma kwenda kuanzisha shule nyingine Mbarali.
Aidha, alisema ufaulu wa shule ya Dynamic unachangiwa na kuchukua wanafunzi 30 katika mkondo mmoja ambao unamwezesha mwalimu kumsimamia kwa karibu kila mtoto.
Mmiliki huyo wa shule alisema kitaaluma kuwa na idadi ya wanafunzi kama hiyo darasani inampandisha mtoto kielimu kwa sababu mwalimu anapata muda wa kumsikiliza shida ya kila mmoja.
Alisema kipaumbele cha mwaka 2026 ni kuboresha elimu kwa kiwango cha juu, kuweka mazingira rafiki na bora ya kusomea ambapo ametoa wito kwa wazazi kupeleka watoto wao katika shule hizo ili kuwawezesha kupata elimu bora.







0 Comments