Mgombea Urais kupitia CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa na m Mbunge za zamani wa Chadema Ezekia Dibogo Wenje,  baada ya kujiunga na CCM.
.....................................

Katika siasa, kuna wakati uamuzi wa mtu mmoja unaweza kuwa alama ya mwelekeo wa kizazi kizima. Hivi ndivyo ambavyo jina la Ezekia Dibogo Wenje, Mbunge mstaafu na kada wa zamani wa Chadema, limeibua tafakuri mpya katika medani za siasa nchini. Baada ya miaka 15 ya kupambana akiwa upande wa upinzani, sasa ameamua, kwa kauli zake mwenyewe, “kuhama Ligi Daraja la Kwanza na kujiunga na Ligi Kuu.”

Tangazo lake, lililotolewa Oktoba 13, 2025, katika mkutano wa kampeni za mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan huko Chato mkoani Geita, si tukio la kawaida. Ni ujumbe wa ishara — kwamba ndani ya jahazi la CCM bado kuna nafasi ya matumaini, dira na uthabiti wa kitaifa.

KUJIHAMI KABLA YA MELI KUZAMA

Kwa maneno ya kisanii, Wenje amejiokoa ndani ya meli ya Titanic kabla haijazama kabisa. Ni kama abiria mwenye macho ya ndani, aliyesikia milio ya barafu kabla haijagonga mwamba. Meli ya Titanic, iliyozama mwaka 1912, ilijulikana duniani kote kama “meli isiyoweza kuzama.” Wengine waliamini ni miujiza ya sayansi, wakaipamba kwa maneno ya majivuno — lakini dakika 160 tu baada ya kugonga barafu, fahari ya dunia ikazama ikiwa na zaidi ya roho 1,500.

Huo ndiyo mfano halisi wa siasa zisizo na dira. Wale waliokuwa ndani ya Titanic walijisifia, wakaamini maneno kuliko tahadhari, wakaendelea kucheza muziki hata maji yalipoanza kuingia. Wenje, kwa mtazamo wa kisiasa, ameona dalili hizo mapema — ameona nyufa kwenye ukuta, kelele za mabishano, woga wa kushindwa, na sasa ameamua kuruka ndani ya mashua ya uokoaji kabla mambo hayajawa mabaya.

Ameamua kujiunga na upande wa nchi unaosimama, siyo ule unaoelea bila dira. Kwa kauli yake kwamba “Taifa ni kubwa kuliko mtu ama taasisi yoyote,” Wenje amejitofautisha na siasa za majivuno zisizo na ramani ya mwisho. Amewaonya Watanzania kuwa makini na miito ya maandamano inayoongozwa na watu wasiokuwepo nchini, akisema: “Wapo wanaochochea moto huku wao na familia zao wakiwa mbali na joto hilo.”

Ni tahadhari yenye maana kubwa. Historia ya Titanic inatukumbusha kwamba wakati wengine walikuwa wakipiga muziki wa furaha, waliokuwa makini walikuwa wakitafuta njia ya kujiokoa. Wenje ameamua kuwa miongoni mwa wachache waliotambua kwamba siasa za jazba, chuki na visasi haziwezi kuifikisha Tanzania kwenye bandari ya salama.

CCM: MSAFARA UNAOKWENDA MBELE, SIYO KURUDI NYUMA

Wenje ameonyesha kuwa siasa ni chombo cha kuleta maendeleo, siyo jukwaa la visasi. Akiwa amepokelewa rasmi na Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Asharose Migiro, alionekana mwenye utulivu na faraja, ishara ya mtu aliyepata hifadhi baada ya safari ndefu ya baharini.

Ameweka wazi kuwa siasa za upinzani zimepoteza mwelekeo, zikiongozwa na hofu ya kushindwa katika uchaguzi mkuu ujao. Kauli yake kwamba, “Tulifanya kikao cha Baraza Kuu, tukapendekeza tusishiriki uchaguzi, lakini si kwa sababu ya CCM, bali kwa hofu ya kushindwa vibaya,” imeweka ukweli hadharani.

Ni kauli inayothibitisha kuwa Wenje hakuhama kwa tamaa, bali kwa tafakuri ya kina — kwa kuona meli aliyokuwa ndani yake inaanza kuzama taratibu, ikibanwa na mawimbi ya migongano, malalamiko na ukosefu wa dira.

CCM kwake imekuwa kama meli yenye dira, nahodha na ramani ya safari. Ni meli inayosimamia amani, umoja na maendeleo — na kama historia ya Titanic inavyofundisha, si kila meli inayong’aa ni salama, na si kila bahari yenye utulivu wa juu haina kina cha hatari.

SAMIA: MWENDELEZO WA NJIA YA MAGUFULI

Wakati haya yakitokea upande wa siasa za upinzani, Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kuandika ukurasa mpya wa maendeleo unaoheshimu urithi wa waliomtangulia. Akiwa Chato siku hiyo hiyo ya tukio la Wenje, alitumia jukwaa hilo kumuenzi Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, akimwita mwalimu na mlezi wa maono ya taifa.

“Kazi tuliyoianza katika Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Hayati Dkt. Magufuli nimeweza kuendelea nayo vizuri, kwa sababu alinielekeza vizuri na amenilea vyema, ndiyo maana nimeweza,” alisema kwa unyenyekevu mkubwa.

Kauli hiyo imeweka bayana dhamira yake ya kuendeleza pale ilipoishia awamu ya tano. Chini ya uongozi wake, miradi mikubwa kama Bwawa la Mwalimu Nyerere, Reli ya Kisasa (SGR), Daraja la Kigongo–Busisi, Magufuli City, na Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Chato imekamilika, ikiashiria mwendelezo wa matendo, si maneno.

Aidha, kupitia mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, serikali yake imeendelea kuwainua wananchi kiuchumi, ikihakikisha kwamba kila mwananchi ana nafasi katika safari ya maendeleo.

KUZIBA PENGO, KUSONGA MBELE

Katika elimu, miundombinu na huduma za afya, serikali ya Dkt. Samia imejidhihirisha kuwa siyo meli ya majaribio bali chombo cha uhakika. Amekamilisha Chuo cha Mafunzo na Usimamizi wa Fedha na VETA Chato, taasisi zilizoanzishwa na Hayati Magufuli. Haya ni matokeo yanayoonesha kuwa uongozi wa awamu ya sita unajengwa juu ya msingi wa uthabiti na maono endelevu.

Hivyo basi, si ajabu kuona viongozi wengi waliokuwa nje ya CCM wakianza kuona mwelekeo huo na kujiunga — si kwa sababu ya tamaa, bali kwa kutambua kwamba meli ya maendeleo bado ipo imara, inaendeshwa kwa dira, na haina dalili za kuzama.

TAFAKARI YA MWISHO: KABLA TITANIC HAITOWEKA

Historia ya Titanic inatufundisha kitu kimoja kikubwa — kwamba majivuno hayajengi, busara ndiyo huokoa. Walioamini kuwa meli yao haiwezi kuzama walipoteza maisha, lakini wachache waliokuwa wakiamini katika tahadhari waliokoka.

Katika siasa za Tanzania leo, Wenje ameamua kuwa upande wa tahadhari. Amepanda kwenye mashua ya matumaini inayoongozwa na nahodha anayeona mbali — Dkt. Samia Suluhu Hassan.
CCM, kama meli kuu ya taifa, inaendelea kusonga mbele ikibeba umoja, amani na maendeleo.

Na kwa kila anayejali mustakabali wa nchi hii, ni vyema kujiuliza: Je, tuko kwenye meli salama, au bado tupo kwenye Titanic inayogonga barafu kwa majivuno?

Kwa hakika, Tanzania inahitaji siasa ya upendo, ujenzi na umoja — siyo muziki wa Titanic unaopigwa huku maji yakijaa.

Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dkt. Asha-Rose Migiro akimkabidhi, fulana Wenje baada ya kuhamia  CCM.
Wenje akipiga saluti baada ya kuhamia CCM
Wenje akizungumza baada ya kupokelewa CCM.

Imeandikwa na: Victor Bariety-Geita  0757 856 284