Baba wa Taifa Hayati Mwalimi Julius Kambarage Nyerere

.......................................

Kuna mali nyingi duniani, lakini chache zina thamani inayopimika kwa moyo wa mwanadamu kama amani. Tanzania ni moja ya nchi chache barani Afrika ambazo zimeishi zaidi ya nusu karne bila kuguswa na majivu ya vita, bila kugawanyika kwa misingi ya dini, ukabila au siasa. Hii haikuwa bahati. Ni zao la hekima, falsafa na uongozi wa mtu mmoja aliyeliona taifa hili kwa jicho la mbali – Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Miaka 26 tangu alipoaga dunia (14 Oktoba 1999), kumbukumbu ya Mwalimu si tu historia ya uongozi, bali ni kioo cha kujitathmini kama taifa:

Je, bado tunaishi katika falsafa yake ya amani, umoja na utu? Je, tunamuenzi kwa vitendo, au kwa maneno matupu?

 Nyerere: Mwanadamu wa Amani, Mwalimu wa Utu

Mwalimu Nyerere hakuwa kiongozi wa kawaida. Alikuwa ni falsafa hai, kioo cha uadilifu na dira ya maadili. Alielewa kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kujengwa juu ya migogoro, ubaguzi au tamaa ya madaraka. Aliwahi kusisitiza kwamba:

 “Amani siyo kutokuwepo kwa vita, bali ni uwepo wa haki, heshima na maelewano.”

Uongozi wake uliweka msingi wa mazungumzo badala ya mapambano, maridhiano badala ya malumbano. Ndiyo nguzo iliyobeba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, uliolinda mshikamano wa Watanzania kwa zaidi ya nusu karne.

Kwa sababu hiyo, hadi leo Tanzania imebaki kisiwa cha amani katika bara lenye misukosuko mingi. Tulipata kiongozi aliyechagua watu wake kuliko madaraka yake — kiongozi wa roho, si wa nguvu.

 Umuhimu wa Amani: Nguzo ya Maendeleo

Katika kumbukizi ya mwaka huu jijini Mbeya, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango alisisitiza:

 “Amani ndiyo urithi mkubwa alioacha Baba wa Taifa, urithi unaotuunganisha bila kujali tofauti zetu.”

Amani ndiyo sababu wakulima wanalima bila hofu, wafanyabiashara wanafanya biashara kwa uhuru, na wanafunzi wanasoma wakiwa na matumaini. Bila amani, hata sera bora na miradi mikubwa inakuwa kama nyumba ya karatasi kwenye upepo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa naye alibainisha wazi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendeleza kwa vitendo maono ya Nyerere — kulinda amani, kukuza uchumi, na kuimarisha heshima ya Tanzania kimataifa.

 Amani Ikipotea: Ni Giza Linalotafuna Vizazi

Historia ni mwalimu mkali. Sudan Kusini, iliyoanza kwa shangwe za uhuru mwaka 2011, ndani ya miaka miwili ikazama kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. Maelfu wamepoteza maisha, wengine wamekimbilia nchi jirani, uchumi umeanguka, ndoto zikayeyuka.

Somalia nayo ni somo jingine. Wakati amani inapokimbia, shule hufungwa, biashara hufifia, na matumaini hufa. Hakuna anayeokoka — tajiri na maskini wote huungua moto mmoja.

Mwananchi mmoja wa Makambako aliongea kwa maneno mepesi lakini yenye uzito:

 “Nina familia ya kuitunza, braza. Sitajiingiza kwenye maandamano ya kuvuruga amani. Bila amani, hata haya mayai ya kienyeji ninayouza sitapata pa kuyaweka.”

Ni sauti ya wananchi wanaoelewa thamani ya utulivu kuliko fujo za siasa.

 Nyerere na Afrika: Amani Kama Sadaka ya Ukombozi

Wakati dunia ikiichora Afrika kwa rangi ya migogoro, Nyerere aliiona kama bara la matumaini.

Alipigania uhuru wa mataifa mengi — Msumbiji, Zimbabwe, Afrika Kusini na mengineyo.

Dkt. Salim Ahmed Salim anakumbusha:

 “Mwalimu Nyerere alituasa kuwa amani ni tunda la haki na uadilifu. Aliongoza mapambano kwa mazungumzo, si kwa mapanga.”

Kwa falsafa hiyo, Tanzania imebaki heshima ya upatanishi katika migogoro ya kikanda.

Urithi huu haukuletwa na bahati — bali na busara, maono na ujasiri wa Mwalimu.

 Kumbukumbu Hai: Amani na Samia

Leo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendeleza urithi huo. Mara kadhaa amesisitiza kuwa “siasa si vita.” Anaamini uchaguzi usiwe sababu ya kugawa Watanzania, bali jukwaa la kuonyesha ukomavu wa demokrasia na umoja wa kitaifa.

Chini ya uongozi wake, Serikali imeanzisha mpango wa kujenga Kituo Kikubwa cha Kumbukumbu cha Mwalimu Nyerere Dodoma, ili kizazi kipya kijifunze historia ya amani na utu.

Paul Kimiti, Mwenyekiti wa Taasisi ya Nyerere, alieleza kuwa kituo hicho “kitahifadhi historia na fikra za Mwalimu kwa manufaa ya Taifa lote – historia ya amani, utu na uzalendo.”

 Somo kwa Wanaotamani Kuvuruga Amani

Kwa wanaoamini machafuko ni njia ya mabadiliko, wajue hawajui historia ya nchi yao. Mapinduzi yoyote huacha vidonda vizito kuliko matunda.

Kuchochea mgawanyiko kwa mitandao si ujanja – ni usaliti wa urithi wa damu za mashujaa.

Kila kura ni silaha ya amani, na kila neno la uchochezi ni risasi ya uharibifu.

 Njia ya Kumuenzi Nyerere Kwa Vitendo

Kama kweli tunamuenzi Baba wa Taifa, basi tuthibitishe kwa matendo:

1. Tuheshimu maoni ya wengine bila chuki wala kejeli.

2. Tukatae lugha za uchochezi, hasa katika mitandao ya kijamii.

3. Tupige kura kwa amani na tukubali matokeo kwa ukomavu.

4. Tuwafundishe vijana historia ya taifa – kwamba Tanzania ya leo imejengwa kwa hekima, si kwa hasira.

5. Tudumishe majadiliano, si mashindano ya ubabe.

 Hitimisho: Urithi wa Amani Usio na Kikomo

Mwalimu Nyerere alituachia zawadi tatu kuu: Amani, Umoja na Utu.

Ni miguu mitatu ya meza ya Taifa letu – zikikosekana moja, meza huanguka.

Miaka 26 baada ya kifo chake, bado tunatembea juu ya urithi huo.

Kama tunataka vizazi vijavyo viishi katika Tanzania yenye matumaini, basi tulinde amani hii kwa ujasiri ule ule aliotuachia Mwalimu.

 “Amani haiji kwa miujiza, bali kwa juhudi za watu wanaoipenda.” — Mwalimu Julius K. Nyerere

 “Tuendelee kulinda amani kama urithi wa kizazi chetu kwa vizazi vijavyo.” – Dkt. Salim Ahmed Salim

 Amani, Umoja na Utu – Urithi wa Nyerere Usiochoka.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana akihutubia kwenye ibada hiyo

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiagana na na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mbeya Mhashamu Gervas Nyaisonga pamoja na Mapadre mbalimbali mara baada ya kushiriki Ibada ya kumuombea Baba wa Taifa Hayati Mwalimu. Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Francisko wa Asizi, Mwanjelwa Mkoani Mbeya leo tarehe 14 Oktoba 2025.




Imeandaliwa na Victor Bariety -0757-856284