Katibu Mwenezi wa Siasa na Itikadi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Nyang’wale, Said Madoshi, akizungumza na wananchi na wana CCM katika mkutano  wa hadhara wa kampeni za Mgombea Ubunge wa Jimbo la Nyang’wale, Hussein Amar Kassu, uliofanyika Kijiji cha Nyaruguguna, Kata ya Nyijundu mkani Geita.

..............................................

Mwenezi wa CCM Wilaya ya Nyang’wale, Said Madoshi, amesema wazi kuwa maendeleo hayajengwi kwa maandamano bali kwa kazi na umoja. Kauli yake ilitolewa wakati wa mkutano wa hadhara wa kampeni za Mgombea Ubunge wa Jimbo la Nyang’wale, Hussein Amar Kassu, uliofanyika Kijiji cha Nyaruguguna, Kata ya Nyijundu.

Kauli ya Madoshi imekuja siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kusisitiza amani, na Jeshi la Polisi kuwatoa hofu wananchi, akisisitiza kwamba wananchi wanapaswa kuendeleza kazi badala ya kushiriki machafuko.

MWENEZI MADOSHI: “MAENDELEO HAYAJENGWI KWA MAWE YA MAANDAMANO”

Kwa sauti ya uzalendo, Madoshi alisisitiza kuwa wale wanaotaka kugeuza uchaguzi kuwa machafuko wanaipotezea nguvu Tanzania:

 “Maandamano hayajengi darasa, hayaleti umeme, hayaleti maji wala hospitali. Kelele hazijengi nchi, kazi ndiyo msingi wa ustawi. Maendeleo haya si ajali — ni matokeo ya uamuzi sahihi wa wananchi wa Nyang’wale.”

Aliongeza kuwa wale wanaopandikiza chuki wakati wa kampeni hawana nia njema:

“Wanataka tufanye fujo, sisi tunataka tufanye kazi. Wanataka kugawa, sisi tunataka kuunganisha. Maandamano siyo shida ya Nyaruguguna — shida yetu ni namna ya kuongeza maendeleo.”

 RAIS SAMIA SULUHU HASSAN: AMANI KWA UCHAGUZI

Mwenezi Madoshi aliunga mkono kauli za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo na utulivu:

“Rais ameshatuambia wazi: uchaguzi si vita. Ni haki ya kidemokrasia ya kila Mtanzania. Tuheshimiane, tuchague kwa amani, maana maendeleo hayawezi kuishi bila utulivu.”

Aidha, Jeshi la Polisi lilihakikisha wananchi kuwa hofu hazina nafasi:

 “Polisi wamesema wazi — hatutavumilia mtu yeyote atakayejaribu kuvuruga utulivu. Tanzania ni kisiwa cha amani, na Nyang’wale tutalinda heshima hiyo kwa kura zetu, si kwa mawe.”

 MATOKEO YA KAZI — SI MANENO

Madoshi aliwakumbusha wananchi kuwa yote wanayoyaona leo ni matokeo ya uamuzi wa busara wa mwaka 2020, walipoiamini CCM:

 “Mwaka ule tulikuwa na sekondari 11, leo tunazo 20. Shule za msingi zimeongezeka kutoka 67 hadi 74, madarasa kutoka 715 hadi 1,003, nyumba za walimu kutoka 370 hadi 389, maabara kutoka 21 hadi 41. Hii ndiyo maana ya kazi. Hii ndiyo maana ya amani.”

 AFYA, MAJI NA UMEME — USHUHUDA WA UAMUZI SAHIHI

Katika sekta ya afya:

Zahanati zimeongezeka kutoka 15 hadi 35

Vituo vya afya kutoka 1 hadi 4

Hospitali ya wilaya sasa inahudumia mamia ya wananchi kila siku

Kituo cha afya Busolwa kimepatiwa zaidi ya shilingi milioni 250, huku upatikanaji wa dawa ukiimarika hadi asilimia 85.

 “Mama mjamzito wa leo hatembei tena kilomita kumi. Anahudumiwa kijijini kwake. Huu ndiyo ushindi wa amani — si wa maandamano.”

Upatikanaji wa maji umeongezeka kutoka 39% hadi 77%, na zaidi ya vijiji 62 sasa vinawaka umeme.

SAUTI ZA WANANCHI: “TUNACHOONA NDICHO TUNACHOTIKI”

John Magulu, dereva wa bodaboda:

 “Hawa wanaotaka maandamano hawajui tulikotoka. Tulikuwa tunapita matopeni, sasa tunapita barabara. Leo biashara zinaenda, umeme unawaka, shule zimejengwa. Mimi nitaitikia kwa tiki, si kwa jiwe.”

Helena Bujiku, mama wa watoto watatu:

“Watoto wanatembea umbali mfupi kwenda shule, maji yapo, zahanati ipo karibu. Mimi maandamano hayanihusu — ninahusu kazi.”

MWENEZI: “TIKI YAKO NI RISASI YA MAENDELEO”

Madoshi aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba:

 “Kura yako ndiyo risasi ya maendeleo. Ukiipiga vibaya, unaua ustawi. Ukiipiga kwa akili, unaimarisha taifa. Tuchague amani, tuchague kazi, tuchague CCM.”

Alimalizia kwa maneno yaliyochochea hisia za kizalendo:

 “Hatutadanganywa na kelele. Tumejionea matokeo ya kazi, tutaendelea kuchagua kazi. Maandamano siyo shida ya Nyaruguguna — tunakwenda kutiki!”

 HABARI KUU: AMANI KWANZA, KAZI MBELE

Nyang’wale leo ni shule ya kizalendo. Ni wilaya inayofundisha kwamba maendeleo hayajengwi kwa jazba bali kwa umoja na kazi. Rais Samia ameshapanda mbegu ya amani, na wananchi wa Nyang’wale wanaimwagilia kwa kura zao.

“Hapa kazi inaendelea, tiki ndiyo silaha ya mafanikio, na amani ndiyo uwanja wa ushindi.”

Ili kumalizia, Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza:

 “Watanzania wote, tushirikiane kudumisha amani wakati wa uchaguzi. Uchaguzi ni fursa ya kidemokrasia, si vita. Amani ndio msingi wa maendeleo na mshikamano wetu wa taifa.”

Shamra shamra kwenye mkutano huo zikiendelea.
Mkutan ukiendelea.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano huo.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Nyang’wale, Hussein Amar Kassu, (katikati) akiserebuka kwenye mkutano huo.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Nyang’wale, Hussein Amar Kassu, akicheza na wana CCM.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano huo.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Nyang’wale, Hussein Amar Kassu, akiwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mkutano huo.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Nyang’wale, Hussein Amar Kassu, akiwa na viongzi mbalimbali wa kata hiyo. 

Imeandaliwa na Victor Bariety 0757856284