Kikwete: Uchumi wa Zanzibar Wapaa Chini ya Dk. Mwinyi, CCM Yaahidi
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
................................
Zanzibar, Jumapili, Agosti 12, 2025 — Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amesema Zanzibar imepiga hatua kubwa ya kiuchumi na kijamii chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar, Dkt.Hussein Ali Mwinyi, akiwataka wananchi kuwapigia kura wagombea wa CCM kuanzia urais, uwakilishi, ubunge hadi udiwani katika uchaguzi ujao.
Akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika Uwanja wa Skys Masingini, Jimbo la Welezo, Wadi ya Mtofaani, Shehia ya Hawaii, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi, uliovuta mamia ya wananchi, Dkt. Kikwete alisema takwimu za Serikali zinaonesha kasi ya ukuaji wa uchumi imeongezeka kutoka asilimia 1.3 mwaka 2020 hadi asilimia 7.4 mwaka 2024, huku Pato la Taifa (GDP kwa bei za sasa) likipanda kutoka Sh bilioni 4,780 mwaka 2021 hadi Sh bilioni 6,572.6 mwaka 2024.
“Haya ni matokeo ya ukusanyaji bora wa mapato, nidhamu ya matumizi, kuimarika kwa sekta ya huduma na uwekezaji, pamoja na amani na utulivu tulionao,” alisema.
Akiainisha vipaumbele, Dkt. Kikwete alieleza kuwa makusanyo ya mapato ya ndani yameongezeka kutoka Sh trilioni 0.856 (2020/21) hadi Sh trilioni 2.104 (2023/24), na bajeti ya Serikali kupanda hadi Sh trilioni 5.18 kwa mwaka 2024/25, “ishara kuwa miradi ya maendeleo inaweza kusukumwa kwa kasi zaidi.”
Aliongeza kuwa katika sekta ya afya, Serikali ya Awamu ya Nane imekamilisha hospitali 10 za wilaya na moja ya mkoa (Lumumba) zenye vifaa tiba vya kisasa, kuongeza ajira za watumishi wa afya kutoka 559 (2020) hadi 2,008 (2024), na kupandisha bajeti ya dawa kutoka Sh bilioni 17 (2020/21) hadi Sh bilioni 40 (2024/25). “Huduma za MRI, CT-
Scan, X-ray, dialysis, pamoja na ICU na NICU sasa zinapatikana kwa upana; upatikanaji wa dawa umefikia asilimia 95,” alisema.
Kwenye elimu, Dkt. Kikwete alisema bajeti imeongezeka hadi Sh bilioni 830 (2024/25) na Serikali imejenga/kupanua skuli 149 zenye madarasa 4,810, maabara, maktaba na TEHAMA, sambamba na kuajiri walimu 3,531 na kupanua utoaji mikopo ya elimu ya
juu. “Ufaulu wa kidato cha nne umepanda hadi asilimia 82 na kidato cha sita kufikia asilimia 99.9 mwaka 2024,” alibainisha.
Akigusia maji na nishati, alisema upatikanaji wa maji safi umeimarika katika shehia zote 388 kupitia uchimbaji visima, ujenzi wa matangi na mabomba, na sasa “mama ametua ndoo kichwani” kwa kiwango kikubwa. Aliongeza kuwa gharama za uunganishaji umeme zimeshushwa na vituo vya kuongeza nguvu vimejengwa Unguja na Pemba, “kurejesha imani ya wawekezaji na wananchi.”
Katika miundombinu, Dkt. Kikwete alisema zaidi ya kilomita 500 za barabara zimejengwa/kuimarishwa, flyover kwenye makutano makuu ziko hatua za mwisho, na
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume umeboreshwa—idadi ya abiria ikiongezeka hadi zaidi ya milioni 2 kwa mwaka 2024. Pia alitaja uboreshaji wa bandari za Mangapwani, Malindi, Wete, Mkoani, Shumba Mjini, Wesha na Fumba,
“ambapo muda wa meli kusubiri ukutani umepungua kutoka siku 40 hadi siku 4.”
Akiweka msisitizo kwenye Uchumi wa Buluu, alieleza kukamilika kwa diko la samaki Malindi, kiwanda cha kusarifu mwani Chamanangwe, na utoaji wa boti 1,077 kwa wavuvi na wakulima wa mwani, hatua zilizoongeza uzalishaji wa samaki na mwani na kipato kwa wananchi.
“Hii ndiyo maana ya uchumi shirikishi,” alisema. Dkt. Kikwete pia alizungumzia kasi ya uwekezaji kupitia ZIPA, akitaja usajili wa miradi 466 yenye thamani ya Dola za Kimarekani zaidi ya bilioni 6 na ajira maelfu kwa vijana,
“chini ya sheria mpya ya uwekezaji inayoweka mazingira rafiki, ikiwemo kwa wazawa na diaspora.” Kwenye utalii, alisema idadi ya watalii imeongezeka kutoka 394,185 (2021)
hadi 736,755 (2024), matumizi kwa mtalii yakipanda, na siku za ukaazi kuongezeka, “ikiibua fursa zaidi kwa wenyeji.”Katika ustawi wa jamii, alisema Serikali imepandisha pensheni ya wazee kutoka Sh
20,000 hadi Sh 50,000, kuweka vitambulisho maalum vya kupata huduma, kuimarisha vituo vya malezi na marekebisho tabia kwa watoto waathirika wa ukatili, na kuendeleza ujenzi wa nyumba za gharama nafuu.
“Miundombinu ya mahakama imefikia hatua ya juu ya ukamilishaji ili kuimarisha upatikanaji wa haki,” aliongeza, akitaja pia masoko ya kisasa, vituo vya daladala na mikopo isiyo na riba kwa wajasiriamali.
“Ilani ya CCM 2020–2025 imetekelezwa kwa kishindo; kilichobaki ni kuimarisha mafanikio haya,” alisema Dkt. Kikwete, akihitimisha kwa kuwataka wananchi “kurejesha CCM madarakani ili miradi ya kimkakati kama uwanja wa AFCON 2027, hospitali za mikoa, kiwanja cha ndege cha Pemba na kituo cha umahiri cha saratani vikamilike kwa wakati.”
Katika hotuba yake, Dkt. Kikwete aliwaombea kura wagombea wote wa CCM, akiwemo Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa nafasi ya Rais wa Zanzibar.
Aliwasifu viongozi hao akisema wamefanya makubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na ni wao pekee wenye nia, uzoefu na uwezo wa kuendeleza maendeleo ya nchi bara na visiwani kwa ufanisi mkubwa.
Aidha, aliwaombea kura na kuwakabidhi ilani ya CCM wagombea wa jimbo la Welezo akiwemo Hassan Hafidh “Diaspora”, anayewania uwakilishi, na Asma Ali Hassan Mwinyi, mgombea wa ubunge, Pamoja wagombea wa udiwani, akiwataja kuwa vijana wenye uwezo, weledi na dhamira ya kuinyanyua Welezo katika nyanja zote za kijamii na kiuchumi.
0 Comments