............................................
Na Mwandishi Wetu
Mkurugenzi wa Msama Promotions na kada mtiifu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) , Alex Msama Mwita amepongeza na kutoa maoni thabiti kufuatia ziara ya Mgombea Urais kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoani Mara na Kanda ya Ziwa kwa ujumla.
Msama amesema "Kwanza nimpe pole Dkt. Samia kwa uchovu wa mizunguko ya nchi nzima, akinadi sera za Ilani ya uchaguzi ya CCM kwa wananchi, lakini pia nimpongeze mno, amekuwa mahiri katika kutoa hoja nzito za namna gani CCM imejipanga kuwahudumia Watanzania.
"Wananchi wa Kanda ya Ziwa, wakiwemo wa Mkoa wa Mara ninakotoka mimi, waliaminishwa upuuzi wa eti Rais Samia hapendwi, ujinga huo wameukataa kwa kujitokeza kwa wingi mno katika mikutano ya Dkt. Samia, Mikoa yote ya Mwanza, Simiyu na Mara," alisema Alex Msama na kuongeza;
"Nichukue nafasi hii kumpongeza sana Dkt. Samia kwa sera nzuri alizozinadi Kanda ya Ziwa, hususan Mkoa wa Mara, mimi Alex Msama nilikuwepo Musoma, hakika nilifurahishwa mno na wingi wa Wananchi waliojitokeza kusikiliza sera nzuri za Dkt. Samia.
"Nimuombe Dkt. Samia aendelee hivi, kamwe asisikilize ngonjera za baadhi ya watu wanaotumiwa kutuharibia Amani ya nchi yetu, yeye ndiye Kiongozi wetu tunaye mtumainia kutupeleka katika nchi ya ahadi, iliyojaa maziwa na asali.
"Mwisho niwaombe na kuwasihi sana Watanzania wenzangu, kujitokeza kwa wingi mnamo Oktoba 29 mwaka huu, kukipigia kura za kutosha Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani wote wa CCM," alisema Msama.
0 Comments