Waziri Mstaafu wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jimbo la Ilongero uliofanyika Septemba 3, 20025 mkoani Singida.
......................................

 Dotto Mwaibale na Philemoni Mazalla, Singida

Waziri Mstaafu wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ameonesha dhamira ya kweli ya kuimarisha chama chake CCM kwa kujitolea mali na nguvu zake kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao.

Licha ya kwamba  hakupitishwa kuwania ubunge kwenye Jimbo la Ilongero, Nyalandu hakukata tamaa wala kuvunjika moyo, badala yake amezidi kuonyesha msisimko wa kipekee kwa namna anavyoshiriki kikamilifu kwenye harakati mbalimbali za kurahisisha ushindi wa CCM mkoani hapa.

Juzi akihutubia mamia ya wanaccm kwenye ufunguzi wa kampeni za kijimbo kwa jimbo la Ilongero alichangia Sh. Milioni 15 kwa madiwani 21 wa jimbo hilo kusaidia kufanikisha kampeni.

Pia aliahidi kuongeza nguvu na ushirikiano kwa wagombea wote wa CCM kwa kampeni za kisasa kabisa za nyumba kwa nyumba, ili hatimaye Singida iingie kwenye historia kwa kuongoza kitaifa kwa kura za CCM.

Kauli hiyo sio tu imeleta hamasa bali pia ni ishara ya ustawi wa mshikamano wa kweli uliojengwa kwa sasa ndani ya chama hicho

Kuwapo kwake mstari wa mbele katika kampeni si jambo jipya, bali ni uthibitisho wa imani yake kuwa CCM ni chama kikubwa zaidi ya mtu mmoja. 

Akizungumza katika uzinduzi huo, Nyalandu alisema mkoa huo utahakikisha kura za CCM zinakuwa nyingi kuliko mikoa yote, na dhamira yake ni kuhakikisha wagombea wote wa chama hicho kuanzia diwani, mbunge hadi rais wanapata ushindi wa kishindo.

“Tunataka Oktoba 29, kura za CCM Singida ziwe za kwanza kitaifa. CCM ni chama ambacho kimetutoa mbali, tunataka kura za madiwani, wabunge na rais zikiongoze kote nchini,” alisema

Kwa upande wake, Mbunge mteule wa Jimbo hilo CCM Haiderali Gulamali, alipongeza dhamira ya mshikamano uliopo baina yake na viongozi mbalimbali wa chama hicho, wakiwemo wastaafu, huku akisisitiza kitendo hicho ni kielelezo cha hekima, umoja na uzalendo wa kweli.

“Huu ndiyo mshikamano tunaoutaka ndani ya chama chetu. Madiwani na viongozi wengine wastaafu wameonesha mfano wa uongozi unaoweka mbele maslahi ya CCM kuliko binafsi," alisema Gulamali na kuongeza;

Kwa mshikamano huu, Ilongero itakuwa ngome imara ya ushindi wa chama chetu."
 Waziri Mstaafu wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, akisalimiana na wagombea nafasi ya udiwani wa Jimbo la Ilongero wakati wa uzinduzi huo.
Basi kubwa la Mama Samia ambalo Nyalandu analitumia kwa ajili ya kampeni za chama hicho kusaka kura za ushindi.

Taarifa hii imeandikwa na Dotto Mwaibale namba ya simu (0754362990)