Kila kona ya Tanzania inapogeuka uwanja wa kampeni, picha inayojitokeza ni moja: umati mkubwa wa wananchi wanaojitokeza kumlaki na kumsikiliza Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan. Kila alipofika, mapokezi yamekuwa ya kishindo kiasi kwamba matumaini ya wapinzani kuelekea Ikulu yanazidi kuyeyuka kama barafu juani.
Katika Kata ya Nyankumbu, mmoja wa makada wa CCM na mgombea udiwani, Paschal Kimisha Sukambi, aliweka bayana: “Wapinzani tuwaachie watalii, lakini ufunguo wa Ikulu anao Mama Samia.” Kauli hiyo imeungwa mkono na mwenyekiti wa UVCCM kata hiyo, Sengiyumva Leonard, ambaye alisema wimbi la wananchi linathibitisha kuwa safari ya CCM kuelekea ushindi wa kishindo imekwisha jengeka.
Samia: Tanzania Mpya Inayojitegemea
Akihutubia maelfu ya wananchi wa Mvomero mkoani Morogoro, Rais Dk. Samia alisisitiza dira yake ya kuijenga Tanzania isiyokimbilia mikopo mikubwa ya nje, bali nchi yenye kujitegemea kiuchumi huku huduma bora za kijamii zikifika kila Mtanzania. Alisema safari ya kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaanza na awamu yake ya pili ya uongozi, na wananchi wakimpa ridhaa Oktoba 29, 2025, basi Tanzania mpya yenye neema itawezekana.
“Tutafika mwaka 2050 tukiwa taifa lenye uchumi wa kipato cha kati ngazi ya juu, hakuna atakayekosa elimu, afya, wala huduma za umeme. Hatutategemea mikopo mikubwa kwa ajili ya maendeleo yetu, bali tutasimama kwa miguu yetu,” alisisitiza Dk. Samia.
Matunda Yanayoonekana
Katika Mvomero, Rais Samia aliwapongeza wananchi kwa kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara – ishara ya nguvu za sera za CCM. Kutoka tani 394,354 za mazao ya chakula hadi zaidi ya tani 400,000, na kutoka tani 400,000 za mazao ya biashara hadi zaidi ya tani 500,000, mafanikio haya ni kielelezo cha juhudi za serikali kupeleka pembejeo, mbegu bora na zana za kisasa za kilimo.
Aidha, kampeni ya Tutunzane imeondoa migogoro kati ya wakulima na wafugaji, minada ya mifugo imeongezeka, machinjio mapya yamejengwa, na mashamba darasa yamefika 42 kutoka shamba moja pekee. Ni taswira ya CCM inayotekeleza, si chama cha ahadi hewa.
Ahadi Mpya za Awamu ya Pili
Rais Samia aliwahakikishia wananchi kuwa serikali itakayoundwa baada ya uchaguzi huu itakamilisha ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, na vyumba vya madarasa; bima ya afya kwa wote itatekelezwa; na barabara za wilaya ya Gairo, kama vile Lubeho–Kiswiti na Gairo–Nongwe, zitatiwa lami. Aidha, machinjio manne mapya na chuo cha VETA vitajengwa Gairo, kutoa ajira na fursa kwa vijana.
Nchimbi Aunganishwa na Wimbi la Ushindi
Mgombea mwenza wa urais kupitia CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, naye ameendelea kupokelewa kwa shangwe katika mikoa mbalimbali. Akiwasili Mara, alihutubia wananchi wa Bunda na kusimama bega kwa bega na wagombea ubunge na udiwani wa CCM. Mapokezi yake yanaonyesha kuwa safu ya juu ya CCM ipo thabiti na umoja umeshashinda mioyo ya wananchi.
Mwinyi Azidisha Nguvu Zanzibar
Wakati bara kampeni zikiwaka moto, Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amechukua fomu ya kugombea urais wa visiwani humo, akiwa na nguvu kubwa ya wananchi na viongozi wa chama. Hii ni ishara kuwa ushindi wa CCM ni wa pande zote mbili za Muungano.
Umoja wa Ndani, Nguvu ya Nje
Katika kikao cha ndani cha UWT kilichoongozwa na Mwenyekiti wa UWT Taifa, Ndg. Mary Chatanda, viongozi waliagizwa kuvunja makundi na kujenga mshikamano, ili ushindi wa Dk. Samia uwe wa kishindo. Hii ni CCM ambayo imejifunza, imejipanga, na inasonga mbele kwa mshikamano na mshikikano.
Umati Wazungumza
Kila anapopita Dk. Samia – iwe ni Gairo, Mvomero, Kibaigwa au Dodoma – umati wa wananchi wanaoimba, kushangilia na kubeba mabango unazidi kuonyesha picha moja: wananchi wamempa ufunguo wa Ikulu. Katika kampeni zake, wananchi husema wazi kuwa CCM ndiyo injini ya maendeleo, na Samia ndiye chaguo la taifa.
Hitimisho
Wapinzani wanaweza kuzunguka nchi wakibeba sera zisizo na mizizi, lakini ukweli unabaki pale pale – wananchi wameshatoa uamuzi. Mapokezi ya kishindo, sera zinazotekelezeka, na uthibitisho wa kazi zilizofanyika ndizo zinazobeba ushindi wa CCM.
Hivyo basi, wapinzani watalii, lakini ufunguo wa Ikulu uko mikononi mwa Mama Samia Suluhu Hassan.Mwisho.
0 Comments