Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, akiwa amepanda treni ya mwendokasi leo Agosti 29, 2029, wakati akienda Morogoro kuana kampeni za uchagui.

........................................

Ni nadra kwa kiongozi wa taifa kutumia mradi mkubwa wa kimkakati kama jukwaa la mawasiliano ya moja kwa moja na wananchi. Lakini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, amevunja ukuta huo leo Agosti 29, 2029, baada ya kuamua kusafiri kwa treni ya mwendo kasi ya SGR akitokea Dar es Salaam kuelekea Morogoro kwa ajili ya kampeni zake za uchaguzi mkuu.

Tukio hili, ambalo lilianza mapema asubuhi katika Stesheni Kuu ya Dar es Salaam, limekuwa na ujumbe mzito wa kisiasa na kimaendeleo. Sio tu safari ya kawaida, bali ni taswira ya dhahiri kwamba miradi mikubwa ambayo serikali ya awamu ya sita imewekeza kwa nguvu zote sasa si ndoto – bali ni uhalisia unaopimika.

SAMIA NDANI YA MRADI WAKE

Kwenye mkakati wa siasa, hakuna silaha kubwa kama kuonyesha matunda ya uongozi kwa vitendo. Rais Samia aliposhuka katika kituo cha Ngerengere tayari alikumbusha wananchi kwamba SGR sio simulizi ya majukwaani bali ni reli inayosafirisha Watanzania, uchumi na matumaini yao. Baada ya kumaliza mkutano wake wa kampeni eneo hilo, alirejea tena ndani ya SGR kuelekea Morogoro Mjini, akitumia usafiri ule ule wa kimkakati ambao serikali yake imeukamilisha.

Hii ni picha yenye nguvu: Rais akitumia huduma anayoiwekea nguvu, akiweka alama kwamba miradi mikubwa ni mali ya wananchi wote, si miradi ya majedwali ya kiufundi pekee.

SGR KAMA NGUZO YA UCHUMI

Katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wa Rais Samia, SGR imekuwa mfano wa usimamizi makini wa miradi mikubwa ya kitaifa. Hatua ya kwanza ya reli hiyo kati ya Dar es Salaam na Dodoma imekamilika, huku ujenzi ukiendelea kuelekea Tabora hadi Mwanza, na mkakati wa serikali ukiwa ni kuipeleka hadi Kigoma.

Hii si reli ya kawaida. Ni uti wa mgongo wa uchumi mpya wa Tanzania – unaopunguza gharama za usafirishaji, kuongeza kasi ya biashara na kuimarisha unganisho kati ya mikoa na nchi jirani. Katika lugha ya kampeni, SGR si mradi wa saruji na chuma pekee, bali ni daraja la ajira, maendeleo ya viwanda, na urahisi wa maisha ya kila Mtanzania.

BOMBA, SGR NA MKAKATI WA SAMIA

Mbali na reli, Rais Samia pia ameweka msisitizo katika mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania) – mradi ambao unaiweka Tanzania katika ramani ya kimataifa ya usafirishaji wa nishati. Bomba hilo, pamoja na SGR, vinaashiria upeo wa kimkakati wa serikali ya awamu ya sita: kuibadilisha Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji Afrika Mashariki.

Kampeni ya Samia imejengwa juu ya hoja hii – kwamba miradi mikubwa si mizigo, bali ni injini za uchumi wa kisasa. Kwa pamoja, SGR na Bomba ni alama mbili zinazochora picha ya Tanzania mpya yenye misingi ya usafiri wa kisasa, nishati thabiti na biashara yenye ushindani wa kikanda.

UJUMBE KWA WANANCHI

Wananchi wa Morogoro waliohudhuria mkutano mkubwa wa hadhara walishuhudia si maneno tu, bali pia vitendo. Waliona Rais wao akitumia usafiri wa treni aliyowekeza ili kuharakisha maendeleo yao. Ni ujumbe mzito wa kampeni: kwamba kiongozi huyu hayupo mbali na wananchi wake, bali yupo ndani ya maisha yao ya kila siku.

HITIMISHO: AHADI YA KESHO YENYE MWENDO KASI

Safari ya Rais Samia kwa kutumia SGR ni hadithi ya Tanzania mpya. Ni hadithi ya kiongozi anayeamini kwamba maendeleo hayapaswi kusimama majukwaani, bali yaonekane kwenye barabara, kwenye reli, kwenye mabomba na kwenye tabasamu la wananchi.

Kwa kutumia miradi hii mikubwa kama nyenzo ya kisiasa na kimaendeleo, Samia amejenga hoja ya msingi ya kampeni yake: kuwa Tanzania ya leo ni ya mwendo kasi, na Tanzania ya kesho ni ya mafanikio yanayoonekana.

Na Victor Bariety -0757-856284