Rais na Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, akipunga mkono kuwasalimia wananchi na wana CCM wakati akiwasili kuzindua kampeni za uchaguzi wa chama hicho Agosti 28, 2025 uliofanyika Viwanja vya Tanganyika Packers Kawe Jijini Dar es Salaam
......................................
Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam
Leo ni siku ya kihistoria kwa mkoa wa Morogoro na taifa kwa
jumla. Rais na Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia
Suluhu Hassan, ameanza rasmi ziara ya kitaifa ya kampeni za uchaguzi mkuu wa
mwaka 2025. Ziara hii si ya kawaida, bali ni mwanzo wa safari mpya ya mageuzi
yanayolenga kuibadilisha Tanzania kwa maslahi mapana ya kizazi cha sasa na
vizazi vijavyo.
Katika hotuba yake ya uzinduzi wa kampeni jijini Dar es
Salaam jana, Rais Samia alieleza kwa uwazi dira ya Serikali atakayoiongoza
endapo atachaguliwa, akianzia na mpango wa siku 100 za mwanzo. Hizi si ahadi za
kisiasa tu, bali ni ahadi za matumaini ya kweli.
Miongoni mwa mambo ya
mwanzo ni kutoa huduma za bure za afya kwa wazee, wajawazito na watoto kupitia
mfumo wa bima ya afya kwa wote—hatua ya awali ya kuijenga Tanzania yenye usawa
katika huduma za afya.
Zaidi, Serikali itapiga marufuku hospitali kuzuia miili ya
marehemu kwa madai ya madeni ya matibabu. Hatua hii inalenga kulinda utu wa
binadamu na kurejesha heshima katika familia wakati wa majonzi.
Sambamba na hilo,
ajira mpya 5,000 kwa wauguzi na wakunga zitatolewa, huku pia serikali
ikigharamia vipimo ghali vya moyo, figo, mishipa ya fahamu na mifupa kwa
wananchi wasio na uwezo.
Sekta ya elimu nayo imepewa kipaumbele cha juu. Rais Samia
amesisitiza kuwa kila mtoto wa darasa la tatu atakuwa na uwezo wa kusoma na
kuandika pasipo shida, huku walimu 7,000 wa masomo ya sayansi na hisabati
wakiandaliwa kuajiriwa mara moja. Hii ni dhamira ya kuandaa taifa la kesho
lenye ushindani wa kitaifa na kimataifa.
Vijana na wajasiriamali wadogo hawajasahaulika. Serikali
itatenga Shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mitaji, kurasimisha mama lishe,
bodaboda na wafanyabiashara wadogo. Hii ni fursa ya kuwaingiza kwenye mfumo
rasmi wa uchumi wa taifa, na kuwainua kutoka kipato cha chini kwenda kwenye
hatua ya ujasiriamali endelevu.
Katika siku hizo 100, Serikali pia itazindua mpango wa
pamoja wa kushirikisha vyuo vya ufundi, vyuo vikuu na waajiri ili wanafunzi wa
VETA wapate nafasi za kufanya mazoezi viwandani. Aidha, mpango wa mitaa ya
viwanda wilayani utaanza kwa lengo la kuongeza ajira kupitia kilimo, uvuvi,
madini na mifugo.
Mageuzi makubwa yanakuja pia kwenye sekta ya maji. Serikali
itaanza ujenzi wa gridi ya taifa ya maji ikihusisha vyanzo vikuu kama Ziwa
Viktoria, Tanganyika, Nyasa na mito mikubwa, kuhakikisha kila Mtanzania anapata
maji safi na salama. Vilevile, jitihada za nishati safi kupikia zitaimarishwa
ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.
Katika utawala mpya, uwajibikaji utakuwa ni wa moja kwa
moja. Mawaziri na wakuu wa mikoa watalazimika kutoa taarifa na kujibu maswali
ya wananchi kwa njia ya moja kwa moja, hatua itakayojenga uwazi na kuimarisha
imani kwa serikali.
Na zaidi ya yote, Rais Samia ameahidi kuendeleza mashauriano
na wadau wa siasa, sekta binafsi na taasisi za kiraia, ikiwemo kuunda tume
maalum ya kuandaa mazingira ya mchakato wa katiba mpya—ndoto kubwa ya
Watanzania wengi.
“Tunajenga taifa lenye utu, mshikamano na fursa kwa wote.
Kila Mtanzania ataguswa na mageuzi haya kuanzia kijijini hadi mjini. Huu ni
wakati wa mshikamano wa kitaifa na safari hii si yangu peke yangu—ni safari ya
Watanzania wote.”
Ziara hii ya Morogoro ni ishara ya mwanzo wa safari ya
matumaini mapya. Ni wito wa mshikamano na mshikikano wa maendeleo.
Dk. Samia akiwa
Morogoro na Balozi Dk. Emanuel Nchimbi akiwa Mwanza wote wanabeba dira ya
taifa—dira ya afya bora, elimu imara, uchumi shirikishi, heshima ya utu, na
Tanzania yenye mshikamano wa kweli.
Huu ni wakati wa Watanzania wote, bila kujali mkoa, kabila
au nafasi ya kijamii, kuungana na kuunga mkono juhudi hizi.
Safari imeanza leo
Morogoro, itafuata Dodoma, kisha nchi
nzima. Lakini safari hii ni ya Watanzania wote. Ni safari ya kujenga taifa la
haki, mshikamano na ustawi—taifa la matumaini mapya.
Hapa chini ni matukio mbalimbali ya picha wakati wa uzinduzi wa kampeni hizo.
0 Comments