Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan
.................................................

Kuna simulizi ambazo haziandikwi kwa wino pekee, bali huchorwa kwenye mioyo ya watu kwa machozi, furaha na mshangao wa kweli. Kagera leo imeshuhudia historia hiyo—historia inayotufundisha kuwa kuna viongozi wanaoweza kuwa madaraka yao ni heshima ya kuwahudumia watu, si majivuno ya vyeo. Na jina linabaki moja tu: Samia Suluhu Hassan.

Katika jiji dogo la Bukoba lililopo mkoani Kagera, lenye kumbukumbu chungu ya mafuriko ya Mei 10, 2024, bado makovu ya maji yanayoangamiza makazi hayajafutika. Lakini katikati ya makovu hayo, imechipua tumaini jipya. Ni tumaini lililojengwa kwenye msingi wa maelekezo ya Rais Samia, tumaini lililofungwa kwa tofali na saruji, na leo likasimama kama kioo cha upendo wa kweli.

Ni nyumba. Lakini si nyumba tu. Ni kimbilio, ni hadithi, ni muujiza. Nyumba ya vyumba vitatu iliyokabidhiwa rasmi kwa Bibi Catherine Nathahiel—mama wa taifa hili kwa namna yake mwenyewe, anayelea wajukuu sita waliopoteza wazazi.

Machozi ya mafuriko, furaha ya upya

Mafuriko yaliyosababishwa na mvua kali siku tatu mfululizo yalibomoa nyumba ya Bibi Catherine kule Mtaa wa Migera. Ukuta ukaanguka, paa likasombwa, na ndoto zikayeyuka kama chumvi majini. 

Hakukuwa na kinga zaidi ya mikono midogo ya wajukuu sita waliokimbilia hifadhi. Walibaki bila chochote, isipokuwa matumaini mepesi kwamba dunia bado inaweza kuwa na nafasi ya rehema.

Hapo ndipo upepo wa huruma wa Rais Samia ukavuma. Si kwa maneno matupu, bali kwa maamuzi ya kivitendo. Mara baada ya kupokea taarifa kupitia viongozi wa Kagera, Rais Samia alielekeza: familia hii ipatiwe makazi mapya ya kudumu.

Moyo wa Rais, faraja ya wananchi

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, alipokabidhi funguo kwa Bibi Catherine, hakutoa hotuba tu bali aliweka kumbukumbu ya taifa:
“Rais Samia hakusita. Alisema watoto hawa hawatapelekwa kwenye vituo vya kulelea. Watakuwa nyumbani, kwenye familia, kwenye makazi salama.”

Ni kauli inayofuta machozi. Ni ushuhuda kwamba kiongozi huyu wa nchi anaona mbali zaidi ya ofisi yake. Anaona ndani ya mioyo ya watoto yatima, ndani ya huzuni ya bibi mzee aliyechoka, ndani ya familia ambayo dunia ingeweza kuisahau.

Shujaa asiyejulikana

Kabla ya msaada huu, familia ya Bibi Catherine ilihifadhiwa kwa huruma ya Adelina Wilson, mtumishi wa idara ya afya. Adelina aliona mateso ya jirani zake, akawakaribisha nyumbani kwake. Ni mfano hai wa mshikamano wa Kitanzania. Lakini huruma ya mtu mmoja ilipogongana na moyo wa Rais wa nchi, matokeo yakawa baraka ya kudumu.

Sauti za shukrani

Bibi Catherine mwenye machozi ya furaha alisema kwa sauti ya mzee aliyetua mzigo:

“Watoto hawa wamepoteza wazazi wao. Nimepoteza watoto wangu watatu. Nilidhani dunia imetusahau, lakini leo tumepata makazi mapya. Asante Rais Samia.”

Loveness Matungwa, mjukuu wake wa kidato cha pili, akachomeka kwa maneno yaliyotikisa ukumbi mzima:

“Tulikuwa hatuamini kama tena tutalala sehemu salama. Nyumba hii kwetu ni kama muujiza. Mungu ambariki Rais Samia.”

Taswira kubwa zaidi

Makala hii si simulizi la nyumba pekee. Ni somo la taifa. Ni kielelezo kuwa uongozi unaweza kuwa wa huruma. Kwamba siasa inaweza kushuka kutoka kwenye majukwaa ya hotuba na kugusa moja kwa moja maisha ya mnyonge.

Kwa kila tofali lililojengwa, kwa kila bati lililowekwa, si nyumba tu iliyosimama—bali imani ya wananchi kwa Serikali yao imeimarika.

Samia ametufundisha kwamba kiongozi wa kweli si yule anayehesabu kura, bali yule anayehesabu machozi yaliyofutwa.

Na kwa hili, historia ya Kagera  imeandika ukurasa mpya: Rais wa upendo, mtu wa watu, mama wa taifa.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, alipokuwa akiikabidhi nyumba hiyo kwa Bibi Catherine
Muonekano wa nyumba hiyo.

 Makala ay yameandaliwa na Victor Bariety namba ya simu 0757856284