Mgombea Mwenza wa nafasi ya Urais kupitia Chama Cha Mapindui (CCM) Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwahutubia wananchi wa Ngudu wilayani Kwimba mkoani Mwanza baada ya kuanza rasmi kampeni za uchaguzi Mkoa wa Mwanza.leo Agosti 29, 2025,

.......................................

Na Godwin Myovela 

Leo macho ya Watanzania na hususan wakazi wa Mwanza yanageukia kwenye sura mpya ya safari ya kisiasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). 

Ni siku ya kihistoria ambapo Balozi Dk. Emanuel Nchimbi, mgombea mwenza wa CCM, anaanza rasmi ziara yake ya kwanza ya kampeni jijini Mwanza. 

Ziara ambayo inaleta hamasa, imani na matumaini mapya kwamba Tanzania inaendelea kuandika ukurasa mwingine wa ustawi wa wananchi wote bila kubagua.

Balozi Nchimbi si jina geni katika medani za uongozi na utumishi wa umma. Ametumikia taifa katika nafasi mbalimbali zenye heshima na heshima yake imedumu kupitia uadilifu, uchapakazi na kujitoa kwake kwa dhati. 

Akiwa mbunge, waziri na baadaye balozi, ameonyesha uongozi wa maono unaoongozwa na nidhamu na imani ya dhati katika kusimamia maslahi ya wananchi. 

Huu ndio msingi unaomfanya leo kuwa chaguo sahihi la kumsaidia Mwenyekiti wa CCM na mgombea urais, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kasi kubwa zaidi.

Siku alipoteuliwa na chama chake, na baada ya mchakato wa uchukuaji fomu kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kupitia mapokezi rasmi viwanja vya Makao Makuu ya CCM Dodoma, Balozi Nchimbi alitoa kauli iliyogusa mioyo ya wengi. Kwa unyenyekevu wa hali ya juu alisema:

“Nakushukuru Mwenyekiti kwa kunipendekeza ili niwe mgombea mwenza. Lakini pia nashukuru Kamati Kuu ya CCM kwa kuunga mkono pendekezo lako, na Mkutano Mkuu wa CCM kwa kunithibitisha.

 Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kukuhakikishia wewe binafsi, chama changu na wanachama wote kuwa nipo tayari kuungana na wewe katika kukitafutia ushindi wa kishindo chama chetu nchi nzima," alisema na kuongeza;

Nimejiandaa kikamilifu kuwa msaidizi wako na si mshindani wako. Nitakusaidia kwa nguvu zangu zote, kwa uwezo wangu wote ili utekeleze ilani ya CCM na kutengeneza historia ya kipekee kwa nchi yetu ambayo haijapata kutokea.”

Maneno haya si ya kisiasa pekee, bali ni kiapo cha uaminifu na mshikamano. Ni ahadi ya utii, mshikamano na mshangao wa kipekee kwa taifa. 

Na jana wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa kampeni jijini Dar es Salaam, mbele ya hadhara kubwa kwenye viwanja vya Tanganyika Packers, Nchimbi alisisitiza tena uthabiti wake:

“Nipo tayari, nipo timamu kutekeleza maelekezo yako na ya chama chetu, na baadaye kufanya kazi kwa juhudi kutekeleza ilani ya CCM.”

Kauli hizi mbili kwa pamoja zinaunda picha ya kiongozi thabiti, mwaminifu na aliyejiandaa kwa dhati kushirikiana na Rais Samia kuiongoza Tanzania kwenye hatua mpya ya maendeleo. 

Ni ushuhuda kwamba safari hii ni ya mshikamano, si ya ushindani wa ndani. Ni safari ya ushindi na msaidizi wake, wanaoshirikiana kwa dhati kufanikisha ilani ya CCM na kuandika historia mpya.

Ziara ya leo Mwanza ni zaidi ya uzinduzi wa kampeni ya mgombea mwenza. Ni mwanzo wa safari ya matumaini mapya kwa Watanzania wote. 

Ni ujumbe kwa taifa kuwa Dk. Samia hakuwa peke yake, ana mshirika madhubuti—Balozi Dk. Emanuel Nchimbi—ambaye ameapa kusimama naye bega kwa bega, kuhakikisha dira ya CCM inatimia na Tanzania inakuwa kimbilio la faraja kwa wananchi wote.

Kwa maono yake, kiu yake ya kutumikia wananchi, na historia yake ya uongozi uliojaa heshima, Nchimbi anakuja kama alama ya mshikamano mpya ndani ya CCM na kati ya viongozi wake wakuu. 

Mwanza leo inaandika ukurasa wa kwanza wa safari hii, na kila Mtanzania anaitwa kuwa sehemu ya safari ya ushindi—safari ya kujenga taifa la matumaini, mshikamano na ustawi wa wote.

Wananchi wa Ngudu wakiwa kwenye mkutano huo.