Mwenyekiti TBN, Beda Msimbe

................................................... 

Mtandao wa Wanablogu Tanzania (TBN) umewataka wagombea wa vyama vya siasa na wananchi kwa jumla kudumisha amani na mshikamano kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu, hususan katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi huo.


Taarifa iliyotolewa Agosti 28, 2025 na Mwenyekiti wa TBN Beda Msimbe, kwenda kwenye vyombo vya habari, imesema, TBN inasisitiza kuwa utunzaji wa amani ni jukumu la kila mmoja, huku akihimiza vyama vya siasa kuendesha kampeni bila kuhatarisha mshikamano wa kitaifa.


“Tunaomba vyama vyote vya siasa vitumie kipindi hiki kueleza ilani zao kwa wananchi kistaarabu na bila kuhatarisha amani tuliyonayo.


Ni wajibu wa kila chama na kila mgombea kuhakikisha kampeni zinabaki kuwa chachu ya kujenga mshikamano na maendeleo na siyo chanzo cha migawanyiko,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.


TBN imewahimiza wanachama wake zaidi ya 200 kutumia majukwaa yao ya Blog, kutoa habari sahihi na za uwajibikaji, ili kusaidia wananchi kuelewa vyema ilani za vyama na wagombea wao, na hivyo kufanya maamuzi sahihi wakati wa kupiga kura.


Mtandao huo umeihakikishia Serikali kuwa uko tayari kushirikiana nayo katika kulinda utulivu wa nchi na kupiga vita taarifa za upotoshaji zinazoweza kuhatarisha amani ya taifa. 


Pia umetoa tahadhari kwa wananchi na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuepuka kusambaza habari za uchochezi au za uzushi.


Kwa mujibu wa TBN, Blogu na mitandao ya kijamii vina nafasi muhimu ya kudumisha amani na mshikamano, hivyo wadau wote wanapaswa kutumia majukwaa hayo kuimarisha demokrasia, kuhimiza mshikamano na kuilinda Tanzania dhidi ya siasa hatarishi.