Mbunge mteule wa Jimbo jipya la Mtumba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde, akizungumza na wanachama wa chama hicho baada ya kukabidhiwa fomu Agosti 26, 2025.

Na Godwin Myovela, Dodoma 

Dodoma jana iligeuka uwanja wa shamrashamra baada ya Mbunge mteule wa Jimbo jipya la Mtumba kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Anthony Mavunde, kuchukua fomu katika Ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) huku akisindikizwa na mamia ya wanachama na wafuasi wa chama hicho.

Safari ya Mavunde kutoka ofisi za tume ilitawaliwa na mbwembwe, nderemo, vifijo na nyimbo za kizalendo, mitaa ya katikati ya jiji ikibubujika rangi za kijani na njano, huku wananchi wengine wakifurika madirishani na juu ya majengo wakipunga mikono kuonesha mshikamano wao.

Akisimama katika Kata ya Makore, Mavunde aliwatuliza mamia  waliomzunguka na kutamka kwa msisitizo:

"Leo ilikuwa ni kuwaambia Dodoma na taifa kwa ujumla kwamba CCM ipo, na tumewaonesha mjini kuwa sisi tupo.”

Mavunde aliwashukuru wanachama wote kwa kujitokeza kwa wingi, akisisitiza kuwa maandalizi ya kampeni yamekamilika na wananchi wategemee hamasa kubwa wiki ijayo:

“Nataka niwahakikishie kwamba tumejipanga kikamilifu. Kampeni zetu za mwaka huu zitakuwa za kisasa, tutazunguka kata kwa kata kueleza kwa nini wachague CCM, kwa nini wamchague Rais wetu Samia, mbunge na madiwani wake. Dodoma mwaka huu tutaiweka yote kijani,” alisema kwa kujiamini.

Aidha, alibainisha kuwa baada ya uzinduzi wa kampeni kitaifa utakaofanywa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, jijini Dar es Salaam na baadaye Morogoro, ratiba itawaleta pia Dodoma kwa mkutano mkubwa wa hadhara.

"Ni desturi yetu, siku hiyo tutajitokeza kwa wingi kuujaza uwanja na kumlaki Mwenyekiti wetu kipenzi,” alisisitiza.

Mara baada ya hotuba yake, Mavunde akiwaongoza mamia ya wanachama, walielekea Makao Makuu ya CCM kwa maandamano ya nderemo na ngoma, wakijiandaa kumpokea Katibu Mkuu mpya wa chama hicho, Balozi Dk. Asharose Migiro, aliyekuwa anawasili jijini humo kwa mara ya kwanza tangu uteuzi wake.

Dodoma jana ilibaki na taswira ya kipekee-mji mzima kugeuka bahari ya kijani na njano, sauti za nyimbo za hamasa zikisikika kila kona, ishara kwamba kampeni za mwaka huu zitakuwa na upepo wa aina yake.


Mhe. Mavunde akikabidhiwa begi lenye fomu.
Mhe. Mavunde akionesha furaha yake baada ya kukabidhiwa fomu.
Msafara uliomsindikiza kuchukua fomu

Mhe. Mavunde akipunga mkono baada ya kuchukua fomu.
Mhe. Mavunde akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu.
Safari ya kuelekea kuchukua fomu ikiendelea,
Taswira ya tukio hilo la uchukuaji fomu
Waendesha bodaboda na Baiskeli wakishiriki katika tukio hilo la kumsindikiza Mhe. Mavunde kuchukua fomu.