Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Tanga, Ramadhani Ndwatah, akizungumza na waandishi wa habari Mkoa wa Tanga wakati wa utoaji wa mafunzo ya mapambano ya rushwa kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu.

....................................

Na Mashaka Kibaya,Tanga

WANAHABARI mkoani Tanga, wametakiwa kutumia kalamu zao katika kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa, kwa maelezo kuwa wao wana nguvu ya ziada kutumia vyombo vyao kufikisha taarifa ya athari za vitendo vya rushwa kwa wananchi walio wengi.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa  Tanga, Ramadhani Ndwatah, ametoa wito huo jana kwenye semina ya mafunzo kwa Waandishi wa habari kuhusu nafasi ya wanataaluma hao katika kuzuia rushwa kuelekea uchaguzi wa oktoba,2025.

Ndwatah amewasihi wana habari kuhakikisha, kalamu zao zinasaidia katika upatikanaji wa viongozi waadilifu ambao hawatakuwa tayari kuona wananchi wakilala njaa.

"Tunapaswa kuunganisha nguvu lengo ni kuendeleza mapambano. Kila mmoja ananafasi yake, wanahabari wana nguvu ya ziada kutumia vyombo vyao kufikisha taarifa kwa wananchi walio wengi"alisema Ndwatah.

Katika kuelekea uchanguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani,Ndwatah alisema, hiki ni kipindi muhimu cha kutengeneza viongozi ambapo wananchi wanapaswa kujua thamani ya kura zao kuchagua pasipo mazingira ya rushwa.

"Rushwa ni adui wa haki na ni kikwazo cha maendeleo.Kwa sasa tuko katika mchakato muhimu wa kutengeneza viongozi.Hivyo kuna umuhimu kila mmoja kujua thamani ya kura.Pamoja na rushwa kuwa jinai pia ni jambo baya kwa imani zote za dini" alisema.

Ndwatah amewasihi waandishi wa habari kuwaelimisha wananchi namna ambavyo wanaweza kuwapata viongozi waadilifu kwa ajili ya Tanzania inayohitajika ambao watakapigiwa kura bila rushwa.

Pamoja na hayo, Ndwatah alisema Wananchi wanapaswa kuendelea kushirikiana kwa karibu na TAKUKURU wakihakikisha wanatoa taarifa mapema juu pindi wanapoona miradi inayoharibika, amesisitiza umuhimu wa kuunganisha nguvu kuondosha changamoto hizo za rushwa.

Hata hivyo Ndwatah, Amewasihi wanahabari katika uelimishaji na ufichuaji wahusika wa rushwa, kuepuka kumuonea mtu badala yake amewataka kutenda haki wakati wote.

"Chonde chonde msije kumuonea mtu, tenda haki siku zote" alisema akiwasihi wanahabari mkuu huyo wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU mkoani Tanga.

Jaspar Mmbaga ni afisa mchunguzi kiongozi msaidizi wa TAKUKURU mkoani Tanga,amesema taasisi hiyo ina majukumu makubwa ya kuzuia na kupambana na rushwa, akibainisha kuwa kwenye kuzia mtu anaweza kuelimishwa na hivyo kuchukia huku akikosa kushiriki rushwa.

Mmbaga ndiye aliyekuwa mwezeshaji wa semina hiyo akisema,kupambana na rushwa ni kipindi ambacho uchunguzi hufanyika na watuhumiwa kuweza kufikishwa Mahakamani.

Mmoja wa washiriki wa semina hiyo alikuwepo Mwandishi wa habari mkongwe Mashaka Mhando, ambaye ameshauri viongozi wa kisiasa kuonesha dhamira ya dhati katika kupambana na rushwa hatua ambayo itaaleta ustawi nchini.

Aidha Naibu wa mkuu wa TAKUKURU mkoani Tanga, Mariam Mayaya alisema kwamba, taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa inatambua mchango mkubwa wa waandishi wa habari katika kupambana na adui rushwa.

Semina hiyo ya mafunzo kwa Waandishi wa habari kuhusu nafasi ya wanahabari katika kuzuia rushwa kuelekea uchaguzi mkuu, ilijumuisha wanahabari zaidi ya 50 kutoka vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii.