Rais mstaafu na Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho Agosti 28, 2025 Viwanja vya Tanganyika Packers Jijini Dar es Salaam.
....................................
Na Dotto Mwaibale
Rais mstaafu na Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ameendelea kujidhihirisha kama kiongozi
asiyechoka kushauri, kuelekeza na kukemea pale inapobidi, bila woga, hila wala
chuki.
Ni nadra katika historia ya Tanzania kumpata kiongozi mwenye
mvuto wa kipekee na hulka ya kiungwana kama aliyo nayo Kikwete—mtu wa watu,
mcheshi, anayejua kuyageuza makali ya maneno kuwa hekima, na mwenye moyo wa
kuzungumza ukweli bila kuficha.
Katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi za CCM
kuelekea Oktoba 29, 2025, uliofanyika Viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar
es Salaam, Kikwete alitoa kauli nzito ya kutafakari.
Akijibu hoja za baadhi ya watu waliodai mchakato wa
kumuidhinisha Dkt. Samia Suluhu Hassan kugombea Urais kupitia CCM haukufuata
utaratibu, alisema wazi:
“Wanaosema utaratibu
umekiukwa ama hawaujui utaratibu wa chama chetu, au wanajifanya hamnazo. Tangu
enzi za Mkapa, mimi, hadi Magufuli, utaratibu umekuwa ni mmoja tu. Rais aliyeko
madarakani akitaka awamu ya pili hupewa nafasi yake. Kwanini leo iwe tofauti
kwa Rais Samia?”
Ni kauli inayodhihirisha uthabiti wa Kikwete katika kulinda
misingi ya chama na pia kukemea upotoshaji unaoweza kuvuruga mshikamano wa
kisiasa.
Katika hili,
ameonesha mara nyingine kwamba hata akiwa mstaafu, hajastaafu hekima, busara na
mapenzi kwa nchi yake.
Lakini kilicho bora zaidi kwa Jakaya Kikwete si tu maneno
yake ya busara, bali ni hulka yake kama binadamu. Anajulikana kwa tabasamu lake
la kudumu, kwa jinsi asivyo mtu wa hasira za haraka, na namna anavyoweza
kutaniana hata pale ambapo anatukanwa au kusemwa vibaya.
Kwa wengi, hulka hii si udhaifu bali ni uthibitisho wa
kiongozi aliyepevuka, asiyeona haja ya kushindana na watu wasiyo na hoja.
Katika mchango wake wa kutafakari safari ya CCM na taifa,
Kikwete mara zote amesisitiza umuhimu wa kuenzi taratibu na uamuzi wa vikao
vya chama.
Katika mkutano mkuu maalumu wa CCM mapema mwaka huu,
aliposhiriki kujadili hoja ya kumuidhinisha Dkt. Samia na Dkt. Mwinyi kugombea
kwa muhula mwingine, Kikwete alisema kwa sauti ya busara;
“Kama mkutano mkuu umeshasema hakuna mwingine isipokuwa
Samia kwa Tanzania Bara na hakuna mwingine isipokuwa Mwinyi kwa Zanzibar, basi
ndivyo ilivyo. Tuweke azimio maalum ili tusije tukajikuta tunaonekana tumekiuka
taratibu. Huu ndio utaratibu wa chama chetu, na ukiheshimiwa hakuna
kitakachotusumbua.”
Kauli kama hii haziwezi kupuuzwa. Ni mashairi ya kiongozi
ambaye hata akiwa nje ya madaraka, bado anaona wajibu wa kulinda misingi
ya chama na heshima ya taifa.
Kikwete ameendelea kuwa mwalimu wa siasa, siyo kwa maandiko
makali, bali kwa kuonesha mfano wa kivitendo.
Aidha, alitumia jukwaa hilo kumpongeza Rais Samia kwa “kushika kijiti” na kutekeleza miradi ya maendeleo aliyoirithi kwa mtangulizi wake Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, huku akiongoza mageuzi makubwa
na kukamilisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa Kikwete, haya yote ni uthibitisho kwamba Samia ni
kiongozi mwenye maono ya mbali, anayestahili kuungwa mkono na kila Mtanzania.
Katika siasa za Tanzania na hata Afrika kwa ujumla, si kawaida kwa viongozi wastaafu kuendelea kuwa na sauti yenye ushawishi bila kutia doa taswira ya chama au taifa. Lakini Kikwete amebaki kuwa mfano bora wa “mzee wa taifa”—anayeweza kushauri bila kukashifu, kukemea bila kubeza, na kucheka hata pale maneno mazito yanapotupwa kwake.
Kila kizazi kinapewa zawadi ya kipekee ya hekima. Kwa
Tanzania, zawadi hiyo katika zama hizi ni uwepo wa Jakaya Mrisho
Kikwete—mwanasiasa, kiongozi, na zaidi ya yote, mlezi wa hekima za kitaifa.
Kuna kila sababu Watanzania wakazirejea kauli zake, wakazitafakari, na kuchukua
hatua.
Kwa kufanya hivyo, tutakuwa sio tu tunaenzi urithi wake, bali pia tunajifunza kwamba siasa inaweza kuendeshwa kwa ustaarabu, mshikamano na upendo pasipo kunyosheana vidole.
Makala haya yameandaliwa na Dotto Mwaibale namba ya simu (0754362990)
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati) akiwa na viongozi mbalimbali wakati wa Mkutano Mkuu Maalum ulifanyika mapema mwaka huu.Wajumbe wakishiriki mkutano mkuu maalum wa chama hicho Jijini Dodoma.
Rais mstaafu na Mwenyekiti mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa chama hicho Dkt. Samia Suluhu Hassan katka moja ya matukio ya kikazi
0 Comments