Katibu wa NEC,  Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Kenan Kihongosi

................................................. 

KATIKA zama hizi ambapo siasa inahitaji sauti mpya, nguvu mpya na fikra mbadala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeonyesha tena upeo wake wa kiuongozi kwa kufanya mabadiliko muhimu yenye sura ya matumaini mapya.

Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imepitisha uteuzi wa kijana Kenani Kihongosi kuwa Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na mafunzo  wa chama, nafasi nyeti inayobeba mzigo mkubwa wa kuwasilisha sera, kueleza mafanikio ya Serikali na kuimarisha mawasiliano na wanachama na wananchi kwa ujumla.

Ni uteuzi unaothibitisha falsafa ya CCM ya kuwa chama cha mapinduzi kisichokoma kujiweka upya, chama kinachotazama mbele, na chama kisichohofu kuwapa vijana nafasi za kiuongozi. 

CCM IMEFANYA UAMUZI SAHIHI

Kupitia uteuzi huu, Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameonyesha tena hekima ya kiuongozi. Amethibitisha kuwa vijana wa Tanzania si nguvu kazi ya kesho pekee, bali ni viongozi wa leo wanaoweza kuaminiwa na kupangia majukumu makubwa.

Kenani Kihongosi ni mfano wa kizazi kipya cha viongozi wachapakazi, wazalendo na wenye dira. Uteuzi wake ni kielelezo cha jinsi CCM inavyoendelea kusoma alama za nyakati, kuhakikisha chama kinabaki chenye mvuto na chenye kuwakilisha matamanio ya kizazi kipya cha Watanzania. 

FAIDA KWA CHAMA NA TAIFA

Kwanza, kwa upande wa chama, nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi ni moyo wa mawasiliano ya CCM. Katika kipindi hiki tunachoelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, chama kinahitaji mtu mwenye nguvu ya kusimama majukwaani, kuwasiliana na umma kwa lugha rahisi na yenye mvuto, na kufikisha ujumbe wa chama kwa vizazi vyote. Hilo Kenani Kihongosi analiweza kwa urahisi.

Pili, kwa taifa, uteuzi huu unaimarisha taswira ya siasa ya kidemokrasia yenye usawa wa kizazi. Vijana wataona kuwa siasa siyo hadithi ya watu waliostaafu nguvu, bali ni jukwaa ambalo hata wao wana nafasi ya kushiriki na kushika nafasi za juu. Kwa maneno mengine, uteuzi huu ni chachu ya kuamsha ari na hamasa ya vijana kushiriki kikamilifu katika siasa na maendeleo ya taifa lao.

KIU YA VIJANA, BUSARA YA VIONGOZI

Hakuna shaka kuwa Kenani Kihongosi ni kioo cha matarajio mapya. Hata alivyokuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa muda mfupi, alionyesha uthubutu, maono mapya na weledi wa kiuongozi. Ingawa amekaa wa muda mfupi zaidi katika historia ya mikoa ya Tanzania, muda huo mfupi umekuwa wa thamani kwao na sasa unamweka kwenye ukurasa mpya wa kisiasa.

Kwa hatua hii, CCM imewajibu vijana waliokuwa wakiuliza: “Je, sisi tutapewa nafasi lini?” Jibu limekuja kupitia uteuzi huu.

UENEZICCMBLOG: MSHIKAMANO WA HABARI NA UONGOZI

Uteuzi wa Kenani Kihongosi pia unafungua ukurasa mpya wa ushirikiano katika uenezi wa sera na fikra za CCM. Taasisi yake na nafasi yake mpya ni chombo cha mawasiliano kwa Watanzania, na tayari wapo waandishi wazalendo waliokuwa mstari wa mbele kuandika na kueleza mafanikio ya chama na Serikali yake kwa umma.

Kupitia ueneziccmblog, ambayo kwa sasa inatambulika kama moja ya blogu zenye mchango mkubwa katika kuhabarisha umma kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa, tayari pamekuwa na urithi wa kazi nzuri katika kutangaza mazuri ya Serikali na chama. Waandishi wa blogu hiyo wamejipambanua kama wazalendo wa kweli, wenye mapenzi mema kwa nchi yao na chama chao.

Kwa hakika, uteuzi wa Kenani Kihongosi unawapa nguvu zaidi kuendelea kusimama bega kwa bega na chama, na bila shaka blogu hiyo itakuwa daraja la kuisaidia ofisi yake mpya katika kufikisha ujumbe kwa jamii pana. Katika mvua na jua, ueneziccmblog itaendelea kuwa chombo cha mshikamano, chenye hamasa na chenye uaminifu kwa kazi ya chama.

CCM YATIZAMA 2025 KWA UHAKIKA

Uchaguzi Mkuu unapokaribia, CCM inajipanga si tu kwa mikakati ya kisera na maendeleo, bali pia kwa mvuto wa kisiasa na uhalisia wa wakati. Kihongosi kama kijana anaweza kuwasilisha hoja, kufikisha ujumbe wa chama kwa lugha rahisi, na kusimama kama daraja kati ya kizazi cha jana na cha leo.

Kwa hakika, uteuzi huu ni ushindi mara mbili: ushindi wa chama kwa kupata mtu sahihi, na ushindi wa taifa kwa kupata kiongozi kijana anayeinua ari na matumaini mapya. 

HITIMISHO: CCM IMEPATA MTU WA WATU NA MTU WA KAZI

Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imeandika historia mpya. Kupitia uteuzi huu, chama kimewathibitishia Watanzania kuwa hakina hofu ya kupokezana mikoba. Kimeonyesha kuwa kipo tayari kuwekeza kwa vijana, kipo tayari kuendelea kuwa chama cha matumaini, na kipo tayari kuendelea kuwa dira ya taifa.

Kenani Kihongosi siyo tu kijana, bali ni mtu wa watu na mtu wa kazi. Kupitia uteuzi wake, kila mwanachama na kila Mtanzania anaona mustakabali wa siasa zetu ukiwa salama na thabiti. 

CCM imepiga hatua ya maana. Ni kweli, chama cha mapinduzi kimepata kiongozi sahihi, kwa wakati sahihi. 

Imeandaliwa na Victor Bariety -0757-856284