Mgombea wa Nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Morogoro katika mkutano wa hadhara wa Kampeni za Uchaguzi za Chama hicho katika uwanja wa Tumbaku mkoani Morogoro tarehe 29 Agosti, 2025.

.............................

Ngerengere leo imeshuhudia historia mpya ikichongwa – historia ya matumaini, mshindi na suluhu ya kweli kwa kila Mtanzania. Maelfu kwa maelfu walimiminika kwa shangwe, vigelegele na nyimbo za hamasa kumpokea Mama Samia Suluhu Hassan, mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM. Ndani ya macho na nyuso za wananchi wale, alionekana siyo tu mgombea, bali dawa ya changamoto zao, suluhu ya matatizo yao, na dira ya maendeleo mapya. Huu haukuwa mkutano wa kawaida – ulikuwa ni tamasha la ushindi, tamasha la matumaini mapya.

Afya Inayogusa Maisha

Mama Samia alisimama mbele ya umati na kuwakumbusha jinsi CCM ilivyopeleka huduma za afya kwa wananchi. Miaka michache iliyopita Ngerengere walikuwa na vituo vya afya vitano pekee na zahanati chache zisizotosha. Leo hii, idadi hiyo imeongezeka mara mbili – zahanati 97 na vituo 11 vya afya, huku chumba kipya cha kuhifadhia maiti kikiokoa familia kutokana na mateso ya kusafiri mbali. Kwa macho ya wananchi, hii ni CCM inayogusa maisha ya kila mmoja, si kwa maneno bali kwa vitendo.

Elimu Bila Malipo – Zawadi kwa Kila Mtoto

Samia aliwakumbusha wananchi kuwa ahadi ya elimu bure si kauli hewa. Ni shule mpya, ni madarasa mapya, ni watoto wanaoingia darasani bila mzigo wa ada. Ngerengere sasa inang’aa kwa shule saba za msingi zilizojengwa, madarasa 120 mapya, na sekondari zilizoongezeka. “Hii ndiyo maana ya kusema CCM ni Mama na Baba wa Watoto wa Kitanzania,” alisisitiza.

Umeme Vijijini – Mwanga wa Maisha Mapya

Kupitia mradi wa REA, kila kijiji na kila kitongoji cha Halmashauri ya Morogoro kimeguswa na umeme. Vijiji 149 na vitongoji 417 sasa vimeunganishwa. Mama Samia aliweka wazi kuwa nishati ni daraja la maendeleo: “Tunapowasha taa vijijini, tunawasha ndoto za vijana wetu, tunawasha matumaini ya kila familia ya Kitanzania.”

Uchumi Unaosonga Mbele

SGR imeibadilisha Morogoro. Wananchi sasa wanaona faida ya treni ya kisasa, huku serikali ikipanga kujenga ghala kubwa la kuhifadhia mazao ili wakulima wauze kwa faida. Barabara ya Zomozi–Ngerengere yenye urefu wa kilomita 11.6 iko njiani kukamilika, ikithibitisha kuwa serikali ya CCM inatembea na wakati, inakimbia na ndoto za wananchi.

Kilimo – Msingi wa Uchumi

Miche 80,000 ya tikiti maji imetolewa bure, mbolea ya ruzuku imefika kwa wakulima, na maafisa ugani sasa wanapiga kazi kwa pikipiki mpya 68. Ni kilimo chenye tija, ni mapato yanayoongezeka, ni tumaini jipya kwa wakulima. “Hapa Ngerengere sasa siyo hadithi za njaa, bali ni hadithi za mavuno,” Mama Samia alibainisha.

Ajira Kupitia Viwanda

Kiwanda kikubwa, viwanda vya kati viwili na vidogo zaidi ya 50 vimezaliwa ndani ya Ngerengere. Hapa ndipo vijana wanapata ajira, ndipo uchumi wa familia unajengwa, ndipo Tanzania ya viwanda inapata uhalisia.

Maji – Kipaumbele cha Kesho

Licha ya changamoto za uharibifu wa mazingira, CCM imefanikisha miradi 15 ya maji na kuongeza upatikanaji kutoka asilimia 51 hadi 57. Mama Samia aliwaahidi wananchi kuwa katika miaka mitano ijayo, maji yatakuwa kipaumbele cha juu zaidi.

Wananchi waliondoka Ngerengere wakiwa na shauku, nyuso zikimekaa tabasamu, mioyo ikibubujika matumaini. Huu ulikuwa mkutano wa ushindi, mkutano wa mshindi, na ushuhuda wa kwamba CCM ndiyo dira, Samia ndiye suluhu ya matatizo ya Watanzania.

Kwa sauti moja, wananchi wa Ngerengere walitangaza: “2025 ni SAMIA, kura ni CCM, Tanzania inaendelea!”

Matukio mbalimbali kwenye mkutano wa hadhara wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika viwanja vya Tumbaku mkoani Morogoro tarehe 29 Agosti, 2025.





Imeandaliwa na Victor Bariety  0757-856284