Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis, akijibu maswali Bungeni Dodoma.

...................................

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.


Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akijibu maswali wakati wa kikao cha nane mkutano wa 17 wa Bunge jijini Dodoma leo Novemba 07, 2024.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumoikolojia Vijijini (EBARR) umefikia asilimia 95 ya utekelezaji wake kwa upande wa Zanzibar.

Amesema hayo leo Novemba 06, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Tamima Haji Abass aliyetaka kufahamu kuhusu utekelezaji wa mradi huo kwa upande wa Wilaya ya Kaskazini, Unguja.

Akiendelea kujibu swali hilo, Mhe. Khamis amesema jumla ya shilingi bilioni 1.4 zimetumika kutekeleza shughuli mbalimbali zikiwemo kuandaliwa kwa Mpango wa Matumizi ya Ardhi katika Shehia za Matemwe Kijini, Mbuyutende na Jugakuu ikiwa ni pamoja na uchimbaji na ujenzi wa visima sita na ujenzi wa vitalu nyumba (greenhouse) vitatu kwa ajili ya kilimo cha mbogamboga.

Ametaja shughuli zingine kuwa ni ununuzi wa boti sita za kisasa na vifaa vya uvuvi, ujenzi wa vituo vitatu vya ufugaji, utengenezaji wa sabuni na ushonaji, ununuzi wa vyerehani 42 kwa ajili ya vikundi vya ushoni.

Pia, ameeleza kuwa Mradi wa EBARR unaoratibiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa upande wa wilaya ya Kaskazini ’A’ umefanikisha ununuzi wa mizinga ya nyuki 200 na ujenzi wa nyumba za nyuki (manzuki), mafunzo ya ujasiriamali kwa vikundi vyote, kuanzishwa kwa vitalu vya miche ya miti 56,000 na utengenezaji wa majiko banifu kwa kaya 125.

Aidha, Naibu Waziri Khamis amesema mradi huo na miradi mingine inafanyiwa ufuatilaji ili kuona kama unatekelezwa kwa ufanisi na wananchi wananufaika nayo.

Akijibu swali la nyongeza la Mhe. Tamima aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha miradi inafuatiliwa, inawanufaisha wananchi, Mhe. Khamis amesema Ofisi ya Makamu wa Rais inawatumia maafisa viungo waliopo katika halmashauri na maafisa mazingira wa wilaya na mikoa katika ufuatialji.

Halikadhalika, amesema kupitia ziara za viongozi hususan Kamati za Kudumu za Bunge zinazosimamia Mazingira na viongozi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais ufuatiliaji wa ufanisi wa miradi unafanyika.

Ikumbukwe kuwa, Mradi wa EBARR unatekelezwa katika Wilaya za Mvomero (Morogoro), Simanjiro (Manyara), Kishapu (Shinyanga), Mpwapwa (Dodoma) Tanzania Bara na Kaskazini A – Unguja, upande wa Zanzibar. Mradi unaratibiwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.